Wednesday, 2 September 2015

Ndata waunde chama au wajiunge Ccm


          Kumeanza kutokea uhuni kuelekea uchakachuaji kiasi cha kuwaudhi wanankijiwe ambao bila kificho wameudhika na wanalaani upuuzi huu wa mingurumbili iliyoapa kulinda wachovu wote kuwabagua huku ikiwapendelea baadhi ya kuwaonea wengine.
          Mijjinga ameingia akiwa amefura utadhani atameza mtu. Haamkui zaidi ya kuanza, “Hivi hawa wanadhani sisi ni mataahira kiasi cha kutuamria na kutuchagulia ukiachia mbali kutupachikia ngurumbili wao?”
          “Yakhe mbona waweweseka kunani chakutata ndugu yangu? Hao waniowageuza nyinyi mataahira akina nani na kwanini?” Mpemba anauliza.
Mijjinga anajibu, “Ami hukusikia haya mauzauza ya ndata kuwazuia wapingaji kufanya kampeni wakati lisirikali lenyewe ndiyo limeruhusu waanze kampeni? Sijui hawa matwahuti wanataka kutupeleka wapi yarabi?
          Mgosi Machungi anakamua mic, “Tinapaswa kueewa. Kinachowasumbua hawa jamaa na ndata zao ni woga hasa ikizingatiwa kuwa kwa miaka waiyokaa kwenye ulaji waifanya kazi ya kuiba na kutanua wasijue siku ya siku itafika na wataahiika kama unavyoona. Kwanini ndata wasivue magwana na kuanzisha chama chao cha siasa kama wao waume kwei?”
          Msomi Mkatatamaa anakula mic, “Umesema vyema Mgosi. Ukiachia woga na usanii, hakuna kinachowasumbua hawa jamaa kama kuona vigogo wao wakiwatupa mkono na kujiunga na wapingaji tena kwa mpigo kama mlivyoshuhudia. Ingawa hawasemi, kitendo hiki licha ya kuwadhoofisha sana na  bila shaka, kimewachoma kweli kweli. Hivyo, wana hasira na visasi. Mara hii mmesahau bwana Cheka Cheka na visasi vyake? Sasa ameungana na Tunituni bingwa wa kuongea maneno machafu kama mlivyomsikia akiwaita wapingaji wapumbavu na malofa asijue ukweli ni kinyume. Kama yeye mlume kweli aongelee kashfa yake ya Kiwila na familia na marafiki zake. Ama kweli mzee Mchonga alijua kutuachi kinyago cha mpapure!”
          Kapende anakatua mic, “Msomi umeniacha hoi kusema eti wamechomwa. Na bado, watachomwa zaidi na zaidi hasa kwenye uchaguzi ujao kutokana na kuharibu kaya kwa kuruhusu mafisadi waitawale. Huyu Tunituni hanipi tabu hasa ikizingatiwa kuwa yeye kwa upumbavu wako alipotoshwa na Delila kiasi cha kujiingiza kwenye ukwapuzi wa kitoto na kipumbavu.”
          “Jaribuni kupima maneno kabla ya kuyatamka na kutukana watu bila sababu. Sijui wengine wana matatizo gani. badala ya kujadili hoja sasa mnajadili watu. Mheshimiwa hakukosea alipowaita wapingaji wapumbavu na malofa.” Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kumwaga utetezi.
          Mpemba anarejea, “Da Sofia hapa sikubaliani nawe. Wewe waona haki kwa wakubwa kutukana wadogo wasijibiwe? Kama Tunituni katunisha misuli ya matusi basi atajatukanwa sana wallahi. Mie maneno ya kitwahuti ya Tunituni hayanitishi kwa vile atajajibiwa. Kinionikera ni ndata kuanza kuonyesha upendeleo wa dhahiri shahidi dhidi ya wapingaji utadhani nao wanasiasa.”
Mheshimiwa Bwege anakula mic, “Hapa kinachoandaliwa ni uchakachuaji baada ya jamaa kugundua kuwa maji yamezidi unga. Hata hivyo, sijui kama mwaka huu watafanikiwa kufunga hayo magoli yao ya mkono ya akina Mapepe tunaye. Natabiri kama watafanya huu uhalifu kuna watu wataishia kunyea debe kule The Hague lau wakale ugali na akina Gbagbo na Chaz Taylor. Tuombe wakubali ukweli kuwa wameisha na kuishiwa vinginevyo tujiandae kulianzisha.”
          Mbwamwitu aliyekuwa akibofya kisimu chake alichopata hivi karibuni aliamua kula mic,” Msiandikie mate wakati wino upo tena tele.” Anageukia upande wangu na kusema, “Mzee Mpayukaji ni mwanasheria aliyekubuhu. Kwanini tusimuombe aanze kuandaa kesi ya kupeleka Hage?” Mheshimiwa Bwege anadakia, “Siyo Hage, Ni The Hague.” Mbwamwitu anajibu, “Nilikosea makusudi nione kama mnainyaka The Hague ambako nimewahi kuzamia miaka fulani nikarejeshwa kwa nguvu.”
          Kila mwanakijiwe anamuangalia mwenzie kuonyesha kuwa alichosema Mbwamwitu ni kamba tu za vijiweni.
          Mipawa ambaye alikuwa kimya akisoma gazeti anaamua kutia timu, “Nashauri kijiwe kilaani jinai hii rasmi na kutoa onyo kuwa kama upuuzi huu utaendelea kitahamasisha wachovu waingie mitaani kabla ya kuwapa kura ya kula wapingaji.  Haiwezekani wahuni wachache hata kama wana madaraka wakaanzisha matusi huku wakiwahujumu wenzao. Kama hawataki kupingwa walianzisha vyama vingi vya nini?”
          Sofi anarejea, “Kwanini watu wengine hawataki kuelewa. Kuanzishwa vyama vingi siyo waranti ya baadhi ya watu kujifanyia wanavyotaka kama kusababisha mikusanyiko isiyo na ulazima.”
          Kabla ya kuendelea Msomi anamchomekea Sofi, “Mikusanyiko isiyo ya lazima ni ipi na iliyo ya lazima ni ipi? Hebu da Sofi fafanua kidogo lau tukuelewe.”
          Mbwamwitu anachomekea, “Kweli da Sofi fafanua na upanue kwani sijakupata vizuri.”
          Kanji aliyekuwa amechelewa kuingia naye anaamua kukamua mic, “Hata mimi iko sangaa sana. Hii vatu hasa data nasema kusanyiko ya lazima nachanganya mimi. Veve hapana ona siku yote vatu nakusanyika kwa dalalada, kwa dukani, feri na hata kwa hakama? Data napaswa fafanua zuri sana kama nataka sisi eleva yeye.”
          Wakati kijiwe kinaendelea si walitokea ndata wakiwa na vya moto vyao. Kuona wakikaribia kijiwe tuliamua kujiweka sawa kuwatia adabu. Bahati yao waliingia mtaa mwingine kabla ya kufika kijiweni. Vinginevyo kungechimbika bila jembe. Si kama wanataka siasa waanzishe chata basi waone kuwa mzoea vya kunyonga vya kuchinja havideku?
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 2, 2015.

No comments: