Saturday, 12 September 2015

UKAWA jibuni hoja za Slaa kwa hoja


          Baada ya Katibu mkuu wa zamani wa CHADEMA Dk Wilbrod Slaa kujing’atua toka kwenye kile alichokiita siasa za vyama, wamejitokeza watu wengi kujibu mapigo japo bila mafanikio.
          Alianza mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia aliyekaririwa akisema kuwa matamshi ya Dk Slaa yalilenga kuligawanya taifa kwa vile aliwataja maaskofu ambao Mbatia hakuwataja majina. Hata hivyo, wakati akielezea mtafaruko juu ya namna mgombea wa UKAWA Edward Lowassa alivyojiunga nao, Dk Slaa alisema baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutompitisha Lowassa kwenye tano bora, askofu Josephat Gwajima alimpigia simu Dk Slaa akitaka wampokee Lowassa.
          Sijui kama kueleza namna Gwajima ambaye ni askofu wa kujipachika alitumika kama mshenga wa Lowassa ni kuligawa taifa. Ni bahati mbaya kuwa Mbatia hakueleza namna ambavyo Slaa anataka kuligawanya taifa, kwa namna gani na ili iweje na apate nini. Kwanini Mbatia ameamua kutoa vitisho na uongo mwingine kwa mlango wa nyuma?  Je anayeligawa taifa ni yule anayesema kuwa fulani alitumika au aliyetumika au kutumiwa? Kwanini baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaongea na watanzania kama vile ni watu wasio na akili? Je hapa kugawa taifa kunaingiaje iwapo baadhi ya wanasiasa na baadhi ya wanaojiita viongozi wa kidini wamefunga ndoa haramu?     
          Kimsingi, wote wanaomshutumu na kumlaumu Slaa licha ya kumkosea adabu, kubabaisha na kuongopea umma, wanazidi kuanika uhovyo wao. Wanapaswa kujibu madai aliyotoa kwa hoja zinazoingia akilini. Wakanushe kama aliyosema si kweli na waeleze ukweli ni upi zaidi ya aliosema Slaa. Hakuna haja ya kutoa visingizio kuwa Slaa analigawanya taifa. Kama wahusika hawana la kusema heri wanyamaze kuliko kuendelea kujivua nguo. Je si kweli kuwa Lowassa aliingia UKAWA bila kujisafisha kama alivyotakiwa? Je Lowassa na wapambe zake wako tayari kujibu tuhuma? Kama hapakuwa na tatizo, ilikuwaje wahusika wakapinda kanuni na kujiweka rehani kwa Lowassa na marafiki na wafadhili zake walioko nyuma ya pazia?
          Wapo waliosikika wakihoji kama Lowassa ni fisadi na wa hovyo ilikuwaje akateuliwa na rais Jakaya Kikwete kuwa waziri mkuu wake. Nadhani CCM na Kikwete wanaweza kutoa jibu rahisi kuwa baada ya kugundua kutofaa kwa Lowassa walimlazimisha kuachia nafasi hiyo kama alivyofanya hapo tarehe 7 Februari 2008 baada ya kutokuwa tayari kujieleza wala kujitetea kama alivyofanya hata wakati akijiunga na UKAWA. Na hii si mara ya kwanza Lowassa kutokujieleza au kujitetea. Hata mwaka 1995 marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere alipomtuhumu kuwa fisadi mwenye ukwasi wa kutisha asioweza kuutolea maelezo, Lowassa aliamua kujikalia kimya. Sijui alitumia ile falsafa ya kuwa kama kusema ni dhahabu kunyamaza ni almas au vinginevyo. Mara ya pili ni mwaka 2008 alipolazimika kuutema uwaziri mkuu. Mara nyingine ni sasa ambapo wengi wa wapinzani na wabaya zake wangetaka aeleze anachojua kuhusiana na Richmond, ile kashfa ya mabilioni iliyomtupa nje ya madaraka asifanye hivyo, badala yake Lowassa anasikika akitoa ahadi lukuki kama kutoa elimu bure kutajirisha watanzania na mengine mengi bila kugusia ufisadi ambao ndilo tatizo kubwa kwa taifa kwa sasa.
          Wapo wanaoona kama anakwepa kugusia upinzani ingawa na hao wanaomkosoa hasa CCM hawazungumzii huo ufisadi kwa kinagaubaga. Wapo wanaodhani kuwa kama Lowassa ni fisadi na mchafu basi alikotoka CCM ndiyo usiseme kama alivyosema Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe wakati akimkaribisha Lowassa kuwa hata Malaika akiingia CCM ndani ya mwezi mmoja atakuwa shetani.
          Tumalizie kwa kushauri viongozi wa UKAWA kuheshimiana na kuthaminiana. Ingawa Dk Slaa amejing’atua, si vizuri kupuuzia wala kusahau mchango wake katika kuifikisha CHADEMA na UKAWA hapo walipo. Kufanya hivyo ni ukosefu wa fadhila na ni tishio hata kwa akina Lowassa hasa pale watakaposhindwa kupata kile wanachopigania. Uchaguzi ni kamari. Hakuna anayejua wanachotaka watanzania hapo Oktoba. Hivyo, badala ya kupoteza muda kuzushiana na kushutumiana, viongozi wa UKAWA wanapaswa kujikita kwenye kuzijua shida za watanzania na kuwapa majibu ya matatizo yao kama yalivyotengenezwa na CCM. Hivyo, Slaa asigeuke sera wala punching bag wala kuondoka kwake kusiwe chanzo cha kuvuana nguo hadharani. Kwani ametimiza haki yake kama ambavyo viongozi wa UKAWA walifanya kwa kumkaribisha na kumpokea Lowassa.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 13, 2015.

No comments: