Thursday, 10 September 2015

Wanaokodisha helkopta wamepataje huo ukwasi?          Hivi karibuni mgombea ubunge wa jimbo la Singida Kaskazini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Lazaro Nyalandu aliwaacha wengi hoi. Aliingia kwenye eneo mojawapo la jimbo lake kwa helkopta jambo lililovuta umati wa watu wengi si kuja kumsikiliza bali kuishangaa helkopta. Ilifikia pagumu hadi mgombea akalazimika kuwaita watu waache kushangaa helkopta waje kumsikiliza. Huu ni ushahdi kuwa jimbo hili lina watu wengi maskini ambao hawajawahi kujaliwa kuiona ndege wala helkopta.
Kwa wanaokumbuka kilichowaponza mgombea wa sasa wa UKAWA Edward Lowassa na swahiba wake wa zamani Jakaya Kikwete mwaka 1995 hakikuwa kingine bali kukodisha ndege tena toka Dar kwenda na kurudi Dodoma kuchukua fomu za urais. Marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere alitaka kujua walikokuwa wamepata fedha za kukodisha ndege.
          Siku hizi helkopta zimeanza kugeuka kama magari ambapo –kama tulivyobainisha hapo juu –hata wagombea wa ubunge ima wanazimilki au kuzikodisha na kuzitumia kwenye majimbo ambayo wameyaongoza lakini wakashindwa kuyapa miundo mbinu muhimu kama barabara.
Je hawa wanaozikodisha au kuzimilki helkopta wamechumaje kwenye nchi iliyokuwa jana na ya kijamaa?  Ni vizuri wakaeleza walivyochuma huo ukwasi lau tujue kama ni halali au haramu.
           Wamechumaje haraka bila kushukiwa kwenye nchi inayosifika kuwa njia na kichaka kikuu cha mihadarati?
Wamechumaje wasistukiwe kwenye nchi ambayo ufisadi umegeuka namna ya wakubwa kutajirika?
          Nyalandu ambaye hivi karibuni alitinga na helkopta akajikuta pekee kwenye sehemu aliyopanga kufanya mkutano baada ya wananchi wake kuizunguka helkopta wakiishangaa anatia shaka hasa ikilinganishwa muda aliohudumu kwenye ngazi kubwa serikalini na uwezo wa kifedha anaoonyesha kwa sasa. Ni kituko hasa ikizingatiwa kuwa Nyalandu mwenyewe anaongoza moja ya majimbo maskini nchini. Hii inaweza kujenga dhana–iwe ya kweli au potofu–kuwa mtu kama huyu pesa ya kukodisha helkopta anaipata wapi kama siyo kutumia cheo alichokuwa nacho serikali kujipatia pesa kinyume cha sheria na maadili?
          Kama nchi yetu ingekuwa ina nia ya dhati ya kupambana na ufisadi watu kama hawa walipaswa wabanwe watoe maelezo walivyopata utajiri huu wa haraka wanaouvuja na kujidai nao kila siku.
Kwa malipo halali ya mbunge wa Tanzania sitegemei kama mshahara na marupurupu yake yanatosha kumpa mtu uwezo wa kifedha kukodisha helkopta. Huyu atarudishaje fedha hii?  Hatuna nia ya kumhukumu Nyalandu japo ushahidi wa mazingira unaonyesha kuwa anazo. Na kama kiongozi wa umma ambao umechoshwa na ufisadi na uroho wa watu wachache wenye madaraka ingekuwa vizuri akaeleza alivyochuma huu utajiri anaoonyesha kwenye uchaguzi tena wa ubunge tu. Je angeteuliwa kugombea urais angemwaga fedha kiasi gani?
          Kwa rais ajaye anapaswa kuwaepuka watu kama hawa kuwapa nafasi za uwaziri kwani watataka wautumie kurudisha mabilioni wanayofuja kwenye kukodisha ndege vinginevyo watoe maelezo juu ya utajiri wao na utetezi wao uwekwe wazi kwa umma ndipo uwaamini.
          Kwa mtu kama Nyalandu aliyekuwa waziri wa Maliasili na Utalii kuonyesha jeuri ya kupiga kampeni kwa kutumia helkopta akiwa anasimamia wizara ambayo inasifika kwa kuuza nyara za taifa nje kunaweza kutoa ushahidi wa kimazingira kuwa kuna namna alifanya.  Wapo wanaoweza kumuona kama mnufaika wa jinai hii ambaye anapaswa kuwekwa chini ya uchunguzi.
          Tumalizie kwa kuwataka wananchi wasikimbilie kushangaa helkopta bali wawaulize wanaozitumia jinsi walivyopata ukwasi wa kuweza kukodisha zana hii aghali. Badala ya kushabikia manjonjo ya wakwazi, wajiulize wao–kama jamii inayowapo kijiko cha kuchumia ukwasi–wamenufaika kwa kiasi gani chini ya uongozi wa watu kama hao ambao wanaonyesha dhahiri kuneemeka binafsi huku umma ukiendelea kuteketea kwenye umaskini wa kutengenezwa na kundi dogo la watu wanaotumia dhamana vibaya na binafsi huku wakiutelekeza umma.
Chanzo: Dira Sept., 10, 2015.

No comments: