Saturday, 12 September 2015

Msimu wa kula kuliwa na kulana

Baada ya msimu wa kutafunana, kugeuzana majuha, kuuzana, kutalikiana, kusalitiana hata kumalizana kufunguliwa, kila msanii amejiandaa na sanaa zake kuhakikisha anachuma. Hapa walevi ndiyo walengwa wakubwa wakiwamo mafisi na mafisadi na wanasiasa wenye mshiko waliouchapa kwa walevi. Kila msanii anataka apige aondoke na chake.
            Juzi mzee mwenyewe ilibidi nipige bangi na kanywaji kama sina akili nzuri baada ya kumuona msanii mmoja akitangaza eti ana mpango wa kuendesha sala na matamasha ya kuombea uchakachuaji!
            Kwa vile ni rahisi kuwaliza wadanganyika, napanga kuandaa tamasha na mikesha ya kuombea hotuba ya mgombea mpendwa ipendwe na nambari wahedi waendelee kuwa kwenye ulaji hata kama hawafai. Ili kuwaingiza kisawa sawa nina mpango wa kuombea hata magari na microphone hoteli na viwanja watakavyotumia wa wagombea wapendwa wa chama pendwa viwe salama. Nitaandaa mkesha na matamasha mengine ya kuomba wapingaji washindwe na kunyong’onyea.
            Funga kazi nitaandaa mikesha na matamasha ya kuhamasisha wazazi wawalazimishe watoto wao kupigia kura chama pendwa. Wasipofanya hivyo wawaachie laana. Pia katika mikesha hii nitaombea ndata wafanikiwe kutoa vitisho kwa wapingaji wasiseme baadhi ya mambo wakashtakiwa.
            Unajifanya unaombea uchakachuaji, amani maendeleo na mengine wakati ukishuhudia siasa za shari, ujambazi, ufisadi na jinai. Kama tutakuwa wakweli, hapa amani itapatikana wapi bila haki? Maendeleo yatapatinaje bila uwajibikaji na uchapakazi? Hata tungeomba miaka milioni na kudhukuru uchi, Mungu si bwege. Hatatoa hizo baraka na vyote tunavyoongopa kuwa tunaombea. Jisaidie nikusaidie. Ukipanda mbigiri usitegemee kuvuna maua aina ya rose au jasmin. Ukichagua ufisadi utegemee ufisadi. Ukichagua mabadiliko utegemee mabadiliko. Simple.
            Hebu tuwe serious kidogo. Hivi lipi la maana, kumwambia mwanao akapige kura au akadai haki? Hawa wachovu wa kiakili wanaokuja na usanii kama huu kwa vile usanii umewashinda sasa wanataka siasa kweli ni wabunifu au wana ndoto za kubuni? Tusiombee uchakachuaji. Badala yake tupiganie haki. Tulaani ufisadi, uzembe, usanii, ushenzi na upuuzi wa kila aina kama kila mtu kujifanya anaipenda kaya wakati anaihujumu. Hivi hawa wavivu wa kufikiri wanaowekeza katika kuomba badala ya kuamba ukweli wana maana kweli? Tumekuwa kaya ya wasanii watupu!
            Nilimuona yule binti aitwaye Ubaya (the opposite) Koleo aliyekataa kuleleka akijinadi kuwa anawahamasisha akina mama wawambie watoto wao wakapige kura. Well, mbona ameanzisha ubaguzi? Kwanini asiwaombe wazazi wote wawili badala yake awaombe wanawake? Shame on you! Usitake kutubagua na mamisahib wetu.
            Ngoja niongee kama kidhabu huyu wa kike apendaye kuchanganya kikameruni ka kiswa akitaka aonekane amebukua wakati hovyo.  By the way, why are you openly discriminating againt the opposition? My understanding is that you are supposed to be neutral as an artist. Njaa nyingine bwana!
            Sitashangaa kusikia kesho wajalaana fulani wenye njaa kama fisi wakiandaa kila aina ya upuuzi kuunga mkono upuuzi na jinai nyingine. Kaya yetu ahitaji kuombewa bali kuambiwa ukweli kuwa inanuka ufisadi na kutawaliwa na wasanii, wachovu na mafisadi wanaopaswa kufungashiwe virago wakaenda kumalizi maisha lupango. Kama mnaipenda kaya na si kuiponda kwanini msiwaombee walevi wazinduke na kuwatimua watesi wao? Haya masuala ya kuomba washitiri wenu wasifumaniwe au kutimuliwa kwenye ulaji yanaboa kuchosa na kukera only God knows. Shame on you! May you perish with them this time around! Wahenga walijisemea: Wajinga ndiyo waliwao. Acha nipanue: Wadaganyika ndiyo wadanganyikao.
Chanzo: Nipashe Sept., 12, 2015.

No comments: