Saturday, 26 September 2015

Matokeo ya uchaguzi yalete mabadiliko


          Hakuna ubishi. Kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba zimetawaliwa na watu na si masuala. Wagombea wanajinadi kwa sifa binafsi na si sera wanazotegemea kutekeleza. Masuala muhimu kwa watanzania yamewekwa kando. Ni bahati mbaya kuwa –kutokana na mfumo mbovu tuliorithi toka chama kimoja –wapiga kura hawana uwezo kisheria kuhoji.
          Si chama tawala wala upinzani, hakuna anayejikita kwenye sera zitakazoondoa matatizo ya watanzania ambayo yamekuwa yakiterekezwa na kila serikali inayoingia. Kwa mfano, watu wanajadili wagombea wenye ushawishi yaani mgombea wa Chama Tawala (CCM) Dk John Pombe Magufuli na mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) Edward Lowassa. Hata ukiangalia hiki kinachoitwa UKAWA kimeondoka kwenye misingi iliyokiunda, yaani kutetea katiba ya wananchi. Wakati mwingine unashangaa kuona wale waliopinga na kuua katiba husika kuwa vinara wa kambi iliyokuwa ikikumbushia na kupigania katiba mpya.
          Kuna mambo mawili ambayo wapiga kura na wanaotaka kuchaguliwa wameyatelekeza au tuseme kuyaua. Mosi, ni katiba mpya. Na pili, ni namna ya kubadili mfumo wa kikale na mgando uliowaweka mateka watanzania kiasi cha mgombea, kwa mfano, wa chama tawala kutaka kubadili hali ukiwa ni ushahidi kuwa serikali ya chama anachowakilisha ilivuruga. Je serikali inayoondoka haikuvuruga? Jibu wanalo wasomaji na wapiga kura kwa ujumla. Kama ingekuwa ilifanya vizuri, basi mgombea wake asingeikosoa.
          Swali linalosumbua wajuzi na wachambuzi wa mambo ni: Je rais ajaye ataweza ku-deliver wakati mfumo wa kutomwajibisha haujaondolewa? Kwa mfano, rais ajaye hawezi kupambana na ufisadi au kutoushiriki wakati mfumo unamlazimisha kufanya hivyo. Kuweka suala hili kwenye picha rahisi, hebu angalia baadhi ya wagombea wanavyotoa ahadi za kuwapa watu vyeo kana kwamba vyeo hivyo ni mali yao binafsi. Wapo wanoona kama hii ni rushwa ya kitaasisi.
          Japo Dk Magufuli amekuwa akisema kuwa atapambana na ufisadi, je sheria au nyenzo inayompa mamlaka yaliyojitenga na utashi wa mtu binafsi viko wapi?  Magufuli amekuwa akiahidi kupambana na ufisadi huku akijua wazi hakuna mfumo sahihi wa kumwajibisha kama hatafanya hivyo kama alivyofanya rais anayeondoka. Kimsingi, ni hatari kutegemea utashi binafsi wa rais badala ya utashi wa kisheria na kimfumo. Jakaya Kikwete alipoingia madarakani, hata hakusumbuka kujiapiza kuwa angepambana na ufisadi. Na kweli hakupambana nao zaidi ya kuupamba kiasi cha mafisadi papa wengi kuwa washirika na marafiki zake. Rejea madai kuwa Kagoda kampuni iliyohusishwa na mshirika wake Rostam Aziz ilikwapua mabilioni ya fedha kwenye fuko la madeni ya nje EPA. Je mtuhumiwa alichukuliwa hatua gani zaidi ya kuamriwa –yeye na wenzake –warejeshe baadhi ya fedha hata bila kuhojiwa na polisi? Je wezi wa wizi wa kutisha wa hivi karibuni –hata kudaiwa walimshinikiza rais kwa njia ya email asiwachukulie hatua bila yeye kunanusha –wamechukuliwa hatua gani? Je rais ajaye ataweza kuwachukulia wahalifu hawa ambao ni serikali ndani ya serikali bila kuwa na nguvu ya kisheria? Hapa ndipo mantiki ya kuwashauri wananchi washinikize wagombea wajadili sera hasa suala zima la katiba mpya ya wananchi unapokuwa muhimu. Wananchi wakiendelea na usingizi huu wa kupumbazwa na ahadi hewa wataishia kulia sana hata baada ya kuwa na serikali mpya ambayo haitakuwa na jipya lolote zaidi ya business as usual.
          Hakuna awezaye kuleta mabadiliko –hata angekuwa malaika –bila kuwa na nyenzo ya kufanya hivyo kama vile sheria na mfumo unaolenga kuleta mabadiliko. Hivyo, kwanza, tuseme kuwa wagombea wanafanya usanii ili kupata madaraka. Na si kwamba hawajui umuhimu wa kujadili masuala badala ya personalities. Wanajua fika sema wanataka wapate madaraka yatakayowawezesha kuwa miungu watu kama hawa wanaotaka kuwarithi. Sidhani kama mtuhumiwa wa ufisadi au mgombea ambaye chama chake kimelea ufisadi anaweza kuongelea ufisadi. Akifanya hivyo, atakuwa anajitia kitanzi kisiasa. Laiti wapiga kura wangeliona hili na kulishupalia. Kama wapiga kura na watanzania kwa ujumla wataendelea kupumbazwa na ahadi lukuki na maneno matupu, wataishia kujilaumu watakapogundua kuwa kumbe walitapeliwa. Wakati muafaka wa kudai mageuzi ya kweli kwa kushinikiza kubadili mfumo ilikuwa sasa. Kama watanzania wangekuwa makini wangegomea hata uchaguzi au kutaka uchaguzi uendane sambamba na mkakati wa kufufua mchakato wa kupatikana katiba mpya iliyouawa kwa hofu ya waliotenda ufisadi wakiwa madarakani kufikishwa mahakamani. Je mtu binafsi tena aliyeteuliwa au kupitishwa au kuenguliwa na watuhumiwa wakuu ataweza kuwachukulia hatua waliomuumba? Kinachofanyika ni kituko kama kitachukuliwa kama harakati za kuleta ukombozi, mapinduzi na mabadiliko ya kweli katika maisha ya mwananchi wa kawaida wa Tanzania.
          Tumalizie kwa kuwaonya watanzania kuwa –kama wataendelea na mfumo huu –wasitegemee mabadiliko yoyote bila kujali nani watamchagua. Kimsingi, ni kama wanachagua baina ya pombe na mvinyo. Vyote ni vilevi na tofauti yake ni majina tu.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 27, 2015.

No comments: