Saturday, 19 September 2015

Gwajima: mkeo akikupiga utatangaza?


          Sina haja ya kumtetea Dk Wilbrod Slaa katibu wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo. Ila maneno ya hovyo, kuudhi na yaliyovuka mipaka yaliyotolewa na anayejiita askofu Josephat Gwajima yamenilazimisha kuandika haya ninayoandika.
          Gwajima alikaririwa kwenye mitandao akisema kuwa aliyesababisha Dk Slaa kuachana na Slaa ni mkewe na siyo mapenzi yake. Japo madai kama haya licha ya kuwa ya kizushi na kitoto, yanavuka mipaka.  Hapa Kanada wananchi wana usemi mmoja kuwa the government has no right to know what is done in our bedroom yaani serikali haina mamlaka ya kuingia kwenye vyumba vyetu vya kulala. Wakanada walitoa kauli hii baada ya baadhi ya wanajamii kutaka kujua kila kitu kuhusiana maisha ya raia na wakazi wa hapa.
          Kinachoshangaza ni ile hali ya mtu anayejiita askofu tena mwanandoa kushindwa kujua mipaka yake kama binadamu, kiongozi wa kiroho hata kama anatia shaka na kama mwanandoa. Hapa ndipo najiuliza: Je Gwajima akipigwa na mkewe atatangaza au atapenda mtu yeyote atangaze? Je kufokewa kwa Dk Slaa –kama alivyokutengeneza na kukuzusha Gwajima –kunamsaidia nini mtanzania wa kawaida?
Je Gwajima anamshambulia na kumdhalilisha Dk Slaa kama nani? Kwanini hakujibu madai yaliyotolewa na Dk Slaa kuwa Gwajima ni mshenga wa Edward Lowassa mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Je hii mikakati ya kijinga na kizamani anayotumia Gwajima imebarikiwa na Lowassa au tuseme amemtuma? Je kwa alivyovuka mipaka, anadhani anawasaidia UKAWA?
          Tangu Gwajima ajitokeze baada ya kumkosea adabu askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam mhashamu Polycarp Kardinali Pengo, wengi wanashinda kumwelewa kama ni mwanasiasa au mchungaji. Kwa wanaojua sifa na hadhi ya uaskofu, wanaona kama anachofanya Gwajima ni kutukanisha hicho cheo. Hata hivyo, ana hasara gani kama amejipachika chake?
Kitendo cha Gwajima nadhani kimemshushia yeye heshima kuliko mhanga wake ukiachia mbali kuzidi kuivua nguo UKAWA. Inashangaza viongozi wa UKAWA ambao wengi wao wamekwenda shule kuruhusu siasa za matusi na kashfa kama hizi.
          Tunashauri Gwajima –hata kama ni mshenga wa mgombea wa UKAWA–ajitahidi kujua na kukubali kuwa uchaguzi ni suala la muda. Kuna maisha baada ya uchaguzi. Hakuna haja ya kutukana wakunga na uzazi ungalipo au kumtukana mamba kabla hujavuka mpya. Hakuna madai ya kushangaza kama Gwajima kudai kuwa Dk Slaa anatumika. Hii inaweza kujenga dhana kuwa kwa vile Gwajima ameshindwa kukanusha au kukiri kutumiwa na Lowassa, hivyo basi anadhani kila mtu anatumiwa kama anavyotumiwa.
          Kuna vitu vingine hata ukiwaambia ndege watakucheka. Inashangaza mtu kama Gwajima kusimama hadharani akatoa madai kuwa amemwekea walinzi Dk Slaa. Kama nani? Kimsingi, Gwajima anapaswa ajitahidi kuachana na maigizo anayofanya kwenye biashara yake ambapo huwaaminisha watu kuwa ana uwezo wa kufufua. Atofautishe suala la Dk Slaa na madai kama yale aliyotoea kuwa angeweza kumfufua marehemu Amina Chifupa.
          Hata hivyo, kuna haja ya kuilaumu serikali ambayo imeruhusu kila msanii na msakatonge kusema na kufanya atakavyo hata kama anachofanya hakiwezekani au utapeli. Nani anaweza kumfufua hata inzi leo kama tutakuwa wakweli?
          Japo Gwajima anaweza kujiridhisha kuwa amefanya kazi ya wale wanaomtumia waliyomtuma kuifanya, kama Dk Slaa ataamua kushitaki –kama ilivyotokea kwa mhashamu Pengo –anaweza kujikuta pakanga. Kuna haja ya serikali kuanza kuchunguza madai hasa kuhusiana na nyadhifa fulani kujiridhisha kuwa wanaodai kuwa nazo wamezipata kihalali na kwa kufuata tararatibu ukiachia mbali kuchunguza kama wanazimudu. Sikutegemea askofu–kama kweli mhusika ni askofu wa kweli aliyetimiza vigezo–kusema aliyosema tena mbele ya vyombo vya habari.
          Pia tuchukue fursa hii kuwashauri UKAWA kuachana na siasa za kihuni zinazoweza kujenga hata dhana za udini ukiachia mbali kuumizana kuzishiana na kukashifiana. Pia UKAWA wachunguze washenga wao. Sijui inajenga picha gani kwa wapiga kura wanapomuona askofu au shehe akipigia debe chama fulani wakati hapaswi kuwa shabiki wa chama chochote? Je wanakwazwa vipi kusikia kuwa askofu anayepaswa kuwa mshenga wa Yesu anakuwa mshenga wa mwanasiasa tena mwenye kutia shaka?
          Tumalizie kwa kuwashauri wapiga kura kuwaepuka watu wasiojua mipaka ya uhuru wao. Si hao tu, hata hao wanaowatuma wanapaswa kuogopwa kama ukoma hivyo kutopewa kura. Maana wakipata madaraka hawa wataumiza wengi kutokana na upogo na uroho na ubinafsi wao. Je Gwajima, kama mkeo akikupiga utatangaza au kupenda mtu mwingine atangaze? Inadhalilisha sana hasa mambo kama haya ambao licha ya kuwa dhambi na jinai yanapotendwa na mtu anayejiita askofu au kiongozi wa kiroho.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 20, 2015.

2 comments:

Katu said...

Kosa alilianzisha doctor Slaa baada ya kusema kisichojiri na kutaja majina. Hivyo ulitaka Gwajima aendelee kunyamaza kimya ili umma wa watanzaniawamuone Slaa kama masiha na wakati yuda wa kuwahadaa wapiga kura.. ..kwa maslahi. Gwajima kumjibu ilikuwa ni sahihi maana hata mimi nilishawishika kuamini maneno ya Slaa lakini baada kumsikiliza kwa nikapata majibu yote ya maswali niliyokuwa najihoji kuhusu Slaa kumbe ni msaliti.

NN Mhango said...

Katu nakushukuru, una haki ya kuamini utakacho na kuacha usichotaka japo unapaswa kuamini kinachotakiwa. Je ungekuwa wewe ndiye Slaa ungefanyaje? Nadhani Gwajima alikosea maana one two wrongs never make a right.