Saturday, 26 September 2015

Usalama mitaani: Fungeni tunguli si kamera

          Nilimsikia rahis Njaa Kaya akisema ana mpango wa kuhakikisha miji yote mikubwa kayani inafungwa kamera kudhibiti wizi na maafa mengine. Japo napiga mibangi na ulabu, naunga mkono wazo la kuhakikisha walevi wanatanua bila kusumbuliwa na mijambazi, mipaka hata mifisadi.
           Hata hivyo, nina ushauri tofauti. Badala ya kufunga kamera mitaani, kwanza, funga hizo kamera kwenye vituo vya kupigia na kuhesabia kura ili kuepusha uchakachuaji. Kwani, vidokozi si tatizo zaidi ya mfumo.  Wengi wanaamini kuwa tatizo la vibaka si kubwa kama lile la mafwisadi tena wanaolindwa na wazito walioahidi wangewalinda walevi ukiachia mbali kuwapunyua kodi za kutanulia kuiba kama vile ni shamba la bibi.
          Tunadhani tatizo ni wazito hasa mzito na wateule, marafiki na washirika zao kama vile akina Kagoda, escrow, EPA na wengine wengi.  Wakati tuliposikia hii kitu mlevi mmoja alisema eti hiki nacho ni kituko cha jamaa kuondokea. Kwani muda wote alikuwa wapi ukiachia mitaa yetu mingi kujengwa na kupangwa hovyo .  Walevi wanadhani fweza ambayo ingetumiwa kwenye usanii ingeelekezwa kubomoa mijengo iliyojengwa kinyume cha sheria na chini ya viwango kama ule wa uhindini. Au mijengo ya wanene iliyojengwa sehemu zilizokatazwa kama ule mhekalu wa Mchunaji Rwakatarehe na mingine mingi huko Ukwasini.
            Hata hivyo, jamaa pamoja na ulevi na mibangi yake, alikuwa na pwenti. Umeme wenyewe wa kuendeshea hizo kamera uko wapi?  Hivi kweli umeme wa mgao unaweza kuwaahidi ulevi usalama tokana na mikamera hii hewa au ni sanaa kama kawa? Kama kamera hizo ni dili basi fungeni Masaki na kote wanapoishi binadamu na siyo Uswazi wanakoishi wanyamawatu. Mitaa haina hata taa za barabarani wala za pembezoni mwake. Mijumba yenyewe imejengwa kama magugu na haina namba. Hizo Kamera zitafungwa wapi? Heri mfunge tunguli na si kamera wataziiba kama siyo kuzihujumu.
          Walevi tunapinga kwa nguvu zetu kufungiwa kamera mitaani kwetu. Zinaweza kutuchungulia hasa kwenye vyoo vyetu vya uswazi zitatuchungulia tunaoga na kunonihino. Pili, mnaweza kutupandishia kodi jambo ambalo litawanufaisha wezi wazito kwenye lisirikali.
          Tatu zinaweza kusababisha mabalaa mengine hasa wale wanaopenda kusimama mitaani na washikaji zao wa pembeni. Nasikia hata ndata wanalalamika kuwa zikufungwa kamera zinaweza kuwaacha bila nguo hasa wale wanaosindikiza mizigo ya wizi nyakati za usiku.
           Hata wenye gesti bubu nao wanalalamika kuwa kufunga kamera mitaani kunaweza kuharibu biashara yao ya chapchap. Na kama kweli mko serious basi mtavunja ndoa kibao. Mie mwenzenu nshafunga ndoa na ulabu na bangi. Sina wasi wasi wala kizuizi. Ila msinilaumu kama mtapuuza ushauri wangu.
          Kama kuna haja ya kufunga kamera basi zifunge kwenye vituo vya kupigia kura kwenye uwanja wa ndege, mipakani ili kuzuia mibwimbwi, madini na nyara zetu kutoroshwa nje. Tena kama ingewezekana kwenye maeneo nyeti kama haya tungeshauri zifungwe darubini ili tuwabaini wanaotugeuza mabwege. Pia tungeshauri zana hizi zifungwe kwenye ofisi zote za TRA, Bandari, Uhamiaji, Tanesco, TIC, hospitalini ili kuona wanaopunyua rushwa na kufanya kaya yetu iwe ombaomba wakati uchumi inao lakini inaukalia.  Hata Mjengoni kungefaa kufungwa zana hizi ili kubaini waishiwa vilaza na wanaoupiga usingizi ukiachia mbali wengine kuchangamkia posho bila kufanya lolote.
          Kama kweli jamaa ana maanisha basi ningemshauri afanye kitu moja ya nguvu. Yaani, afunge tunguli. Najua vidokozi na majambazi wengi walivyozoea ushirikina na upuuzi mwingine kama huo basi watazigwaya kuliko hata ukoma. Taarifa; Maswihiba zetu Saleh, Omari,na Hussein Assagaf wa Gerezani wamefiwa na dada yao mwezi uliopita. Salamu ziwafikie washikaji wote wa Gerezani, Kidongo Chekundu, Msimbazi na Lumumba. Nasikia mnakamata Nipashe ili kumsoma mshikaji wenu mlevi kama hamna akili nzuri. Msichunguliane. Kila mmoja anunue nakala yake na kufunua.
Chanzo: Nipashe Sept., 26, 2015.

No comments: