The Chant of Savant

Monday 14 September 2015

UDART hujuma ndani ya hujuma


          Hivi karibuni mradi wa mabasi yaendayo kasi umezinduliwa japo nyuma ya pazia bado kuna maswali mengi. Kwa wanaokumbuka sakata la kutwaliwa kinyemela na kifisadi kwa lilokuwa Shirika la Usafiri Dar Es Salaam (UDA) watakumbuka fika kuwa serikali pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam walishindwa kutoa maelezo ya kina na yanayoingia akilini juu ya uuzwaji wa shirika hili.
          Hata kabla ya vumbi kutua, tunaletewa zengwe jingine ambapo UDA hii–ilioyouzwa na kutwaliwa kinyemela na kifisadi–eti imeungana na Dar Es Salaam Rapid Transit (DRT) kuunda UDART. Hakika ndoa hii ni ya mashaka sana na ni hasara kwa umma. Inashangaza na kutia shaka ambapo makampuni haya mawili yanavyoweza kuungana huku mojawapo likiwa halieleweki uhalali wa upatikanaji wake. Je kuna wazito nyuma ya hujuma hii? Kwani wakati wa uzinduzi wa mradi husika, mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mecky Said Mecky alisikika akisema kuwa kitendo cha kuwakasimisha mradi wazawa ni ushahidi kuwa serikali inawajali watu wake. Je ni ya kweli haya au kuna maslahi binafsi yanayolindwa hapa? Kama ni kujali wazawa tulidhani basi hata viwanda na migodi vingechukua hatua hiyo. Ukiachia hili, Tanzania–kwa sasa–haina sera ya uzawa bali uwekezji wa kichukuaji na uchuuzi. Hivyo, madai kama haya yanakinzana na hali hali na ukweli halisi.
          Swali linalosumbua vichwa vya watu wengi ni kwanini serikali imeharakisha ukasimishaji wa mradi kwa mojawapo ya kampuni yenye kutia shaka bila kutoa maelezo ya uuzwaji wa UDA kwanza? Je dili hili lina maslahi kwa taifa au kundi dogo la watu fulani wanaotumia mamlaka yao kuwahujumu wananchi kwa kisingizio cha kuwajali? Sijui Mecky alimaanisha nini kusema kuwa Tanzania inawajali wazawa kinyume na sera husika? Je ni kwanini serikali imeingia ubaguzi huu kama hakuna namna?
          Kwa hali ilivyo–kama wananchi watakuwa makini–kuna harufu ya rushwa, ufisadi na hujuma kwenye mradi huu wa UDART. Kinachoshangaza zaidi ni ile hali ya serikali ile ile ambaye waziri wake aliwahi kukanusha kuwa hisa zake katika UDA ziliuzwa kutumia jumla ya shilingi 39.6bn ambazo zililipwa kwa kampuni ya kichina Beijing International Engineering Group (BCEG), kujenga miundombinu ya kutumiwa na UDART bila maslahi wala kumaliza mgogoro wa kwanza juu ya uuzwaji wa UDA. Bila shaka hii ni pesa ya umma ambayo inapaswa kutolewa maelezo ya kina juu ya ni vipi itarejeshwa, kulipwa na umma utanufaika vipi na fedha yake. Je kwanini serikali imewajengea uwezo watu binafsi chini ya kisingizio cha uzawa? Wengi walitarajia mwekezaji kwenye mradi huu awe na uwezo wa kujijengea miundo mbinu na kuendesha mradi husika bila kutegemea fedha ya umma. Hii ndiyo biashara. Sidhani kama inaingia akilini eti tu aje kuchimba madini–kwa mfano–apewe mtaji na nyenzo toka kwa serikali. Kama mtu wa namna hii ni muhimu, kwanini serikali isijiendeshee mradi wake au kuuza kwa njia ya tenda au mnada? Je hapa serikali zaidi ya kujichanganya na kubabaisha inatoa ishara gani? Je kuna serikali ndani ya serikali hadi serikali kuu inaendelea kuingia mkenge hivi? Tunashauri rais ajaye afumue ndoa hii na kujua kilichoko nyuma ya pazia kabla ya umma kupigwa tena kama ilivyozoeleka.
          Ukiangalia hata hiki kinachoitwa UDART na nani ni nani katika mradi huu, unagundua mazingaombwe ambapo mkurugenzi mtendaji mwenye kutia shaka wa UDA Robert Kisena eti ndiye mkurugenzi mkuu wa UDART. Hatuambiwi wala kupewa mchanganuo wa ugawanaji madaraka baina ya UDA na DRT. Hili nalo linaleta shaka jingine juu ya mradi mzima na wahusika wake. Je nani anasimamia hisa za serikali ambazo UDA ilichukua kifisadi na kinyume cha serikali? Je serikali imeamua kutoa sadaka hisa zake kwa Kisena na ili iweje na Kisena kama  nani? Wananchi wa Dar Es Salaam wanapaswa kuacha kupewa matumaini na maneno mazuri. Badala yake wahoji utawaliwaji wa shirika zao na uchezeaji wa fedha za serikali katika kuendesha biashara binafsi. Ndiyo, watanzania wanahitaji usafiri wa haraka. Hata hivyo, hawahitaji haraka inayosababisha fedha na mali zao kuibiwa na watu wachache wenye madaraka. Nadhani mradi wa UDART kama utafukunyuliwa na wapinzani wakajenga hoja imara, unaweza kuizamisha CCM. Tunashauri wananchi watake majibu sahihi kabla ya uchaguzi mkuu ili waamue nani wamuamini nchi yao. Je UDART si hujuma ndani ya Hujuma?
Chanzo: Dira Sept., 14, 2015.

No comments: