Monday, 14 September 2015

Lowassa, Paulo, Yuda na Umar


          Baada ya waziri mkuu wa zamani aliyeondolewa madarakani na kashfa ya Richmond, Edward Lowassa kujiondoa kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) mengi yamesemwa na kuandikwa. Wapo waliomuona kama Lowassa anahangaika kupata urais kwa gharama yoyote. Wapo waliompongeza kwa kuachana na utumwa wa chama. Pia wapo waliomuona kama mkombozi. Wengine walimuona kama salata wa kawaida anayetafuta ulaji. Pia wapo waliomuona kama mwanasiasa komavu aliyeamua kutimiza haki yake kufanya anachoamini.
          Mawazo haya kinzani yametukumbusha kisa cha watu maarufu katika dini mbili kuu duniani yaani Ukristo na Uislamu. Katika kudurusu sintofahamu hii tumeonelea tutumie wahanga wa dini waliokuwa wasaliti wa dini husika lakini baadaye wakaishia kuwa mashujaa wa dini hizi.
          Kwanza, tumdurusu mtume Paulo ambaye kwenye Ukristo anaweza kuchukua namba mbili kwenye umaarufu baada ya Yesu Kristo tokana na maandiko na mawazo yake. Mwanzoni, Paulo alisifika kwa kuwakamata na kuwasulubu wanafunzi wa Yesu. Vitabu vinatuambia kuwa kipindi fulani Paulo–bingwa wa kuua na kusulubu wanafunzi wa Yesu–aliona mwanga na kujiunga na Yesu na kuwa mtu muhimu katika kueneza injili aliyohubiri Yesu.
Pili ni Yuda ambaye naye alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Yesu. Huyu–tofauti na Paulo–kwa tamaa zake, aliamua kumsaliti Yesu hasa pale alipowaonyesha watesi na wauaji wake nani ni Yesu.
          Mwingine ni sayyidna Umar Ibn al-Khattab al Faruq. Umar–kama Paulo–alisifika kwa kuwatesa na kuwaua wafuasi wa Mtume Muhammad (SAW). Baada ya kuingiwa na ujumbe, Umar aliamua kuachana na kuwatesa na kuwaua wafuasi wa Mtume Muhammad na kujiunga naye katika kueneza Uislam.
          Tukirejea kwa Lowassa, si siri kuwa alikulia na kufikia mafanikio yake kwenye CCM. Kama Paulo na Umar, aliona mwanga; na kuamua kujiunga na upinzani baada ya kutoswa na CCM. Tofauti na watajwa hapo juu, Lowassa alifikia hatua ya kuachana na CCM baada ya kubwagwa kwenye kinyang’anyiro cha urais. Hivyo, anaonekana kama Yuda Iskarioti, mwanafunzi wa Yesu, aliyekisaliti chama kilichomtengeneza na kumlea kutokana na tamaa zake binafsi. Je mtu wa namna hii–sisi walioko nje ya ulingo wa siasa–tumhukumu vipi kwa kulinganisha na wahusika tajwa hapo juu? Je Lowassa ni msaliti, askari aliyeuona mwanga au muumini aliyeingiwa na ujumbe? Swali hili ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa wapo wanaotaka CCM iangushwe baada ya kuwaangusha kwa muda mrefu. Kwa hawa, yeyote anayeweza kufanikisha kuanguka kwa CCM anafaa bila kujali historia yake kama ilivyokuwa kwa Paulo na Umar. Kwa wana CCM, kosa alilotenda Lowassa–kama Yuda–halisameheki. Je tunaotetea maslahi ya taifa tushike na kuacha lipi? Jibu la swali hili–mara nyingi–linategemea uko upande upi.
          Ukisiliza wapenzi wa kambi husika katika kipindi cha baada ya Lowassa kuondoka CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaweza kushawishika na misimamo na hoja za wahusika. Inahitaji kuwa makini kuamua ni kipi uchukue na kipi uache katika kuamua ni wapi uegemee hasa kipindi hiki tunachoelekea kwenye uchaguzi mkuu. Lowassa amewachanganya wengi. Wapo waliompenda kwa vile alikuwa CCM na wapo walioanza kumpenda baada ya kuingia upinzani. Je kinachofuatwa hapa ni mtu au sera? Je Lowassa ameleta sera gani au jipya gani kwenye upinzani ukiachana nafsi yake? Je Lowassa ni msaliti, aliyeona mwanga au mchumia tumbo anayetafuta mkate wake popote pale bila kujali kama aliyeyashikilia ni shetani au mtakatifu? Wapo wanaoamini kuwa kama Yuda Iskarioti asingemsaliti Yesu basi ukombozi kwa njia ya kumwaga damu usingefanyika. Ukiangalia visa vya Paulo na Umar–kadhalika–navyo vilifanikisha kuenea kwa dini husika. Kuepuka kula hasara, wahusika tunapaswa kuchagua kati ya mtu na maslahi ya taifa, maslahi binafsi na ya taifa na pia kuangalia dhana nzima ya ukombozi (mabadiliko) tokana na nguvu au mtafaruko alivyoleta Lowassa kwenye siasa za Tanzania.
Dira Sept., 14, 2015.

No comments: