The Chant of Savant

Tuesday 8 September 2015

Kijiwe chamkaribisha Dk Silaha












Baada ya Daktari Willy Silaha kufanya maamuzi magumu na kujivua gamba akiachana na siasa chafu za vyama, Kijiwe kina mkakati wa kumvuta ili aje kuongeza nguvu na kufichua uchafu mwingine unaofanywa na mafia wa kisiasa wawe tawala au tegemewa.
          Mijjinga ndiye anaanzisha mada hii, “Waheshimiwa, baada ya daktari Silaha kumwaga mtama na upupu kiasi cha kuwaacha hoi wapingaji, mnaonaje? Si tumchukue aje hapa kuongeza timu lau tukiunda chama cha kisiasa tuwe ndiyo warithi wa UKAUA?”
          Mgosi Machungi anadakia, “Hii azima tiunge mkono. Tina kia sababu ya kumtaka daktai huyu mkwei sawa na poofwesa Pumba ambaye naye ameachana na siasa za majitaka. Sijui wengine mnaiongeeaje hii?”
          Kapende anakwanyua mic, “Msemayo nayaunga mkono, lazima tumnyakue njomba Silaha kabla ya manyang’au kumuiba. Huyu bwana amenikuna kweli kweli. Maana aliponitajia akina Roast Tamu la Aziz wanavyovuta kamba nyuma ya pazia ili kuweka fisadi mwenzao, nimenkubali.”
          Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu, “Japo nakubaliana na kuvuta huyu daktari mwenzangu, kitendo chake cha kutufunga kamba kuwa ameachana na siasa za vyama kinanitia shaka. Je anataka kufanya siasa za vijiwe au atawezaje kufanya siasa bila vyama? Je anataka kuwa mwangalizi na mchambuzi kama mzee Mpayukaji au mshangiliaji asiye na timu ili mradi yake ni timu inayoshinda?”
          Mipawa aliyekuwa akinong’ona jambo na da Sofia Lion aka Kanungaembe anakwanyua mic, “Kimsingi lazima hapa kuwa na mgawanyiko. Lazima wawepo wanaomuona daktari mwenzetu Silaha kama shujaa na wengine watakaomuona kama michosho. Cha msingi hapa ni kukubaliana kuwa baadhi ya hoja zake zina mashiko sana. Mfano alipodai kuwa Luwasa alikwepa kujisafisha na kutoa utetezi, hapa alimaanisha uwajibikaji uwazi na ukweli.”
          Kabla ya Mipawa kuendelea, Sofia anakula mic, “Nawaonea huruma wapingaji. Sasa ona wanavyoumbuana. Wakishaadhirika wanaanza kuna mkono wa mtu wakati mchawi wao ni wao wenyewe na tamaa zao.”
          Anakohoa na kubwia kahawa yake na kuendelea, “Sisi tulishawambia kuwa huyu jamaa tuliyemkataa hakubaliki na kama akikubalika si kwenye urahis jamani. Hivi kweli mtu anayeogopa hata historia yake anaweza kuifanyia nini kaya kama siyo kuiuza?”
          Mheshimiwa Bwege anaamua kumchomekea da Sofi. Anakula mic, “Da Sofi acha nikuchomekee kwanza. Nadhani hapa suala la kuuzwa na kununuliwa liko wazi. Awe Luwasa au Makomeo wote watatuuza tu. Mimi kimsingi sioni tofauti ya wawili hawa. Sana sana kinachonivutia ni majukwaa wanayotumia. Luwasa anatumia jukwaa safi la mageuzi na Makomeo anatumia jukwaa chafu la ukale.”
          Mbwa Mwitu aliyekuwa akitaniana na Kanji anaamua kula mic, “Mheshimiwa Bwege unataka kutwambia kuwa kwenye uchakachuaji huu tumeliwa tena? Maana ukichagua Luwasa unaambiwa ni mchafu. Ukichagua Makomeo unaambiwa ni msafi lakini chata lake chafu usipime. Sasa tumchague nani wajameni?”
          Kanji anaamua kula mic huku akitabasamu, “Veve hapa jua mambo? Kwanza kula iko siri ya mtu. Kama naona Luvasa au Komeo faa chagua yeye. Veve kama naona Komeo faa basi chagua yeye. Nyingine tajua bele ya safari bwana.”
          Msomi anaamua kurejea tena, “Hapa si suala la kuangalia nani anafaa tu. Tuangalie na sera. Tuhoji sera na ahadi lukuki wanazotoa wagombea ambapo kila mmoja anaonekana kuahidi mema mengi kuliko uwezo wake. Laiti yanayoahidiwa kwenye kipindi hiki cha kulana, kuuzana, kuchuuzana na kuliwa yangetimilika, mbona tungekuwa kaya ya peponi na si motoni kama ambayo imekuwa. Maana kila muongo huja na uongo wake na ahadi zake hewa na kupata kura ya kula huku akiwaacha wachovu wakizidi kuwa wachovu. Hivyo, mimi sidhani kama kuna kitu cha muhimu kuangalia kama sera na matamko ya wahusika.”
          Mzee Maneno anatia guu, “Msomi usemayo ni kweli tupu. Ukisiliza ahadi zinazomwagwa, unaweza kuzani umaskini kayani ndiyo bai wakati ndiyo unaanza. Nilimsikia mmojawapo akisema kuwa atatoe elimu bure. Hivi kweli hili linawezekana usawa huu? Je hiyo njuluku ataipata wapi?
          Inaonekana maswali ya mzee Maneno magumu kweli. Kwani hakuna anayekula mic.
          Msomi anaamua kurejea kutoa majibu, “Uko sahihi kuhoji na kustukia ahadi ya kutoa elimu ya bure kwa wote. Nadhani hii  ni maisha bora kwa wote iliyofinywa kwenye elimu. Kwa sera za sasa za kiliberali mamboleo zinazodhaminiwa na vyombo vya fedha vya kimataifa kama shirika la mshiko la dunia au Benki ya Dunia, si rahisi kaya kapuku kama hii kutoa elimu bure wakati lisirikali lenyewe linaendeshwa kwa kukopa na kubomu. Hivyo, huu ni uongo wa wazi wazi.”
          “Mie sasa mwanchanganya wallahi. Kumbe hawa waweza jisemea lolote kama wale ma MC wa harusini wasijue watu wana akili tena ziniochemka?  Mie nshagaa sana watu kujadili mipango hewa wakati hiyo fedha wala hawana. Je kwanini watutenza hivi na tuwafanyeni?
          Kapende anakwanyua mic, “Nadhani ndiyo maana tunataka daktari Silaha ajiunge nasi tutoe mwelekeo mbadala. Maana wote wameshindwa.”

          Kijiwe kikiwa kinanoga tulipokea simu ya mchunaji na askopo, Jose Gwaijimia akitaka tusimpake mtu wake.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 8,2015.

No comments: