The Chant of Savant

Thursday 3 September 2015

Kila mwenye akili na mapenzi na nchi yetu asome makala hii

Mtikisiko

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, amevunja ukimya kwa kueleza kile kilichomsukuma kujiuzulu wadhifa huo, sambamba na kujivua uanachama wa chama hicho. Katika kuvunja kwake ukimya huo, Dk. Slaa aliweka hadharani namna viongozi wenzake ndani ya Chadema, akiwamo mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Profesa Abdallah Safari walivyoyumbisha kusimamia misingi ya namna ya kumpokea Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond, Edward Lowassa. Mbali na hayo, mengine aliyoweka wazi ni namna Lowassa alivyoratibu mipango yake ya kuhamia Chadema akiwa bado CCM, akifanya hivyo kwa kumtumia Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima. Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Gwajima ndiye “mshenga” wa Lowassa kwa Chadema na kati ya hoja alizozitumia kumshawishi Dk. Slaa kumkubali Lowassa ni kwamba, mwanasiasa huyo aliyeokosa urais CCM, anaungwa mkono na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na ndani ya Kanisa Katoliki, maaskofu 30 kati ya 34, wamehongwa na wamemkubali Lowassa. Ilivyokuwa Kama ambavyo wahenga wanasema kimya kingi kina mshindo, ndivyo ilivyokuwa kwa kimya cha Dk. Slaa. Mshindo wa kimya hicho ulianza kujidhihirisha mapema, katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, alikofanyia mkutano huo, ambapo mpaka saa saba mchana idadi kubwa ya waandishi wa habari walikuwa tayari wamefika katika eneo hilo, kushiria kuwa tukio hilo litakuwa na ukubwa wa aina yake. Dk. Slaa aliyewasili ukumbi wa mkutano saa 8:05 mchana, jana, Jumanne, aliweka bayana uamuzi wake wa kuzungumza na waandishi wa habari, akisema, kwa kuwa ikifika mahali ukweli unatakiwa kusemwa ni lazima usemwe, kutokana na upotoshwaji uliofanywa na watu mbalimbali wakiwamo baadhi ya viongozi wakuu wa Chadema, kwamba alikuwa amepumzishwa (likizo) na viongozi wa chama hicho. “Nataka nianze na kusema mimi sikuwa likizo, sikupewa na mtu yeyote, niliamua kuachana na siasa Julai 18, 2015 usiku saa tatu, baada ya kuona yanayofanyika ndani ya chama changu sikubaliani nayo,” alisema Dk. Slaa. Alisema alishiriki katika majadiliano ya kumakribisha Lowassa ndani ya Chadema lakini kwa kuweka misingi ambayo chama kilitakiwa kwanza kuizingatia kabla ya kufikia uamuzi wa kumkaribisha, baada ya kukatwa katika mbio za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). “Baada ya tarehe 11 Julai, Lowassa alipokatwa mshenga wa Lowassa, Askofu Josephat Gwajima alinipigia simu kuniambia sasa kule Dodoma mambo yameisha, nikamwambia awasiliane na Mwenyekiti (Mbowe), tukawasiliana na naye baadaye tukakutana naye, nikawaeleza msimamo wangu kwamba ni lazima kusikia mtu ana nini, tukakutana na vijana wake ili tujue ana nini,” alisema na kuongeza; “Nikasema msingi wa kwanza ni lazima atangaze kutoka CCM, akijiondoa aseme anakwenda chama gani, na atumie nafasi hiyo kujisafisha na tuhuma zote zinazomkabili katika nchi hii, kwa sababu Chadema kimeaminika, ukipokea mtu ambaye hajajisafisha unakuwa unapokea na uchafu wake. Hilo halikufanyika mpaka alipopokewa Julai 28. Siwezi kumsafisha mtu ninayekaa naye meza moja.” Dk. Slaa anasema msingi wa pili aliokipa chama chake kabla ya kumpokea ni kupima kama Lowassa ni rasilimali (asset) au mzigo (liability) kwa chama hicho, kwa kuwa walikuwa wameambiwa kwamba angekuja na viongozi wengi kutoka CCM. “Nikawauliza anakuja na nani, yeye peke yake au na wafuasi, na kama wafuasi ni wa aina gani, vijana wa boda boda wanaoshabikia tu au ni viongozi serious (makini). Nikaambiwa anakuja na wabunge 50, wenyeviti wa CCM mikoa 22 na wenyeviti wa wilaya 88, nikakiri hili litakuwa tetemeko, nikahitaji kupewa majina, Katibu Mkuu makini hawezi kupokea idadi tu, na tulikuwa tunakwenda kwenye uchaguzi wa kura za maoni, ilikuwa lazima nijue nani anagombea wapi, vinginevyo uta – destabilize (utayumbisha) chama,” alisema na kuongeza kwamba; mpaka chama hicho kinampokea Lowassa hakuna hata moja kati ya misingi hiyo iliyotekelezwa. Kuhusu ushiriki wake katika kikao cha kumpokea Lowassa, alisema aliombwa kuitisha kikao cha Kamati Kuu ya dharura, lakini akaeleza msimamo wake kwamba hajapata jibu la upembuzi kama Lowassa ni mtaji au mzigo. “Asubuhi ya Julai 27, Mwenyekiti alinipigia simu kunieleza sijaridhika akaomba tukutane asubuhi tuzungumze ili tusije tukatofautiana na Mwenyekiti, kwangu mimi tangu mwaka 2004 sijawahi kutofautiana na mwenyekiti, tulifika pale akiwepo Tundu Lissu, na mshenga wake Gwajima, tukabishana tangu saa 3 asubuhi mpaka saa 9 alasiri, wapo hapa waseme kweli, mimi sikukubaliana nao tangu mwanzo, nawaomba viongozi wangu wawe wanyoofu na wenye hofu ya Mungu,” alisema. Kwa mujibu wa Dk. Slaa, baadaye walitakiwa kwenda nyumbani kwa Lowassa lakini alikataa akisema hawezi kwenda nyumbani kwa mtu wa CCM katika mazingira ya u-Katibu Mkuu wa Chadema. Aliongeza kwamba baada ya hapo, iliundwa kamati ya watu wachache kumshawishi (Slaa), ambayo ilikaa tangu saa 9 mpaka saa 12 jioni lakini akawapa masharti yale yale. “Tuliporudi kwenye kikao taarifa ya kikao kile haikutolewa. Nikaandika barua ya kujiuzulu nikampa Makamu Mwenyekiti Profesa Safari akaichana, nikaandika nyingine nikampa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, akaniambia Dokta usihangaike mambo haya yamepangwa,” alisema. Akizungumzia watu waliokuja Chadema, alisema wote wamekuja wakiwa makapi baada ya kuwa wameshindwa kwanza kwenye mchakato wa awali wa CCM (kura za maoni) na hata huko walikotoka si wasafi. “Watu kama Sumaye hawakuwa safi, mimi mwenyewe nilimwita fisadi bungeni, alichukua Shamba la Magereza Kibaigwa, na yeye mwenyewe alifikia hatua ya kusema CCM wakimteua Lowassa yeye atahama chama, sasa yuko naye, najua dhambi haihalalishiwi na dhambi nyingine, lakini maneno hayo yalitamkwa na nani, Watanzania walimwita Sumaye ziro,” alisema. Aliendelea kuwaponda wana CCM waliohamia kuwa ni kama makapi ambao hawataongeza thamani yoyote kwa chama hicho akiwataja Mgana Msindai na Matson Chizii kuwa ni sehemu ya makapi ambayo hayataongeza thamani yoyote kwa Chadema. “Kuna watu wanasema ondoa CCM kwanza hata ikiwezekana kuweka mkataba na shetani, mimi ni Padri Mkatoliki, hata kama nimestaafu, nikubali kuweka mkataba na shetani mradi tu niondoe CCM. Unaondoa CCM kwa program serious na watu makini au unaondoa na watu wale wale?” alihoja Dk. Slaa. Chadema na tuhuma za ufisadi Mbali na kuhoji endapo waliohamia Chadema kutoka CCM wameongeza thamani yoyote kisiasa; Dk. Slaa aliyesimama imara akizungumza kwa saa 1.32 alisema; “Chadema iliaminika miongoni mwa Watanzania kwa kutoyumbishwa na kusimamia uadilifu. Sasa leo Chadema wanathubutu kusema etu usimtuhumu mtu? Upuuzi mtupu! Kama tusingemtuhumu Mramba (Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba) leo angekuwa Segerea? “Kama tusingemtuhumu Yona (Waziri wa Viwanda wa Nishati na Madini, Daniel Yona) leo angekuwa Segerea? Ni lazima tuhuma zitolewe ndipo serikali iwajibike. Kwa kawaida binadamu lazima kwanza awe na ‘reasonable doubt’ sio ‘absolute doubt’,” alisema Dk. Slaa. Alinukuu kifungu kimoja cha Biblia kinachosisitiza kuwa ni makosa na dhambi kupotosha watu huku akiitupia lawama Serikali ya CCM kwa kumlea Lowassa kwa miaka mingi bila kumshughulikia akisema: “CCM ni waoga na ndio maana wamlea mtu huyu na leo wanatuletea matatizo.” Dk. Slaa ambaye alisema hajawahi kutofautiana na Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, vikaoni tangu mwaka 2004, aliwashangaa viongozi wa Chadema kwa majaribio yao ya kuwapotosha Watanzania kwa kutaka waamini kuwa kwa Lowassa na watu wake kuhamia Chadema, wamekuwa watu wasafi. “Ni kama vile choo; kwetu Watanzania choo ni sehemu chafu ingawa kwa wenzetu ukiingia chooni unakuta kuna glasi ya ‘wine’. Samahani kwa mfano huo lakini sina mfano mwingine. Sasa leo mtu aende chooni achote kile kilichomo ndani ya choo na kukihamishia chumani anakolala, utasemaje? Ni kwamba choo kimehamia chumbani. “Na kwa kuwa ili aweze kuchota kinyesi kilichomo chooni atalazimika kwanza kukikoroga, basi kile kilichomo chumbani kitakuwa kinanuka zaidi ya hata choo chenyewe,” alisema Dk. Slaa. Suala la kashfa ya Richmond Kuhusu kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond, kashfa ambayo aghalabu Lowassa na wapambe wake hawapendi kuisikia hata kidogo, Mbunge huyo wa zamani wa Karatu alisema yeye na wabunge wengine wa Bunge la Tisa wanalifahamu zaidi kwa kuwa waliiishi kashfa hiyo. Dk. Slaa aliwatupia lawama wabunge wa CCM kwa kutopenda kusoma nyaraka mbalimbali huku pia akiwalaumu waandishi wa habari kwa kutokufanya utafiti na kuandika habari za kina. “Hebu mwambieni Lowassa aache kulalamika. Ajitokeza hadharani na kusema Richmond ni ya nani? Amtaje hadharani huyo mkubwa anayedai kuwa alimzuia kuvunja mkataba, ni nani. Juu ya Waziri Mkuu kuna Makamu wa Rais na Rais, sasa ni nani kati ya hao? “Juzi juzi hata leo walikuwa wakinitisha eti nisizungumzie masuala haya wakidai kuwa nitapotea kisiasa; nini kupotea kisiasa, niko tayari kupotea katika siasa za Tanzania hata nipotee kabisa duniani kuliko kuikana dhamira yangu. “Msingi wa Richmond ukitaka kuujua ni ripoti ya Kamati ya Mwakyembe (Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk. Harrison Mwakyembe),” alisema Dk. Slaa. Alisema kamati hiyo iliomba ridhaa ya Rais iweze kupitia nyaraka za Baraza la Mawaziri na kufahamu kwamba katika Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoketi Februari 2, 2006 (takriban mwezi mmoja na nusu tangu Lowassa ateuliwe kuwa Waziri Mkuu), kilitoa mapendekezo ya namna ya kushughulikia kwa dharuala tatizo la umeme lililokuwa limeikumba Tanzania. Alisema suala hilo lilianzia tangu wakati wa Rais Benjamin Mkapa ambapo Baraza la Mawaziri lilielekeza namna ya kulitatua, kisha suala hilo likarithishwa kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete. “Kwa mujibu wa kifungu cha 112 cha Katiba, Waziri Mkuu ndiye mwenye nguvu katika utendaji wa serikali na baada ya kikao cha Februari 2, 2006, saaa 10 jioni ya siku hiyo hiyo, Ibrahim Msabaha (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo), akafuta mchakato ulioanzia kwenye Serikali ya Mkapa na kubarikiwa na Baraza la Mawaziri. “Tujiulize Msabaha alipata wapi nguvu ya kufanya hivyo kama si kwa bosi wake (Waziri Mkuu)? Mimi mwenyewe, Februari 5 au 6 mwaka 2008 wakati wa kashfa ya Richmond, nililetewa rushwa hotelini kwangu saa 12 asubuhi. Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu Februari 8, 2008. “Nililetewa Sh. milioni 500 ili ripoti isipitishwe. Nikamuuliza aliyeniletea, kama mimi unanipa Sh. milioni 500, wewe una shilingi ngapi?” alisema huku akihoji Dk. Slaa na kumtaka Lowassa ajitokeze na kueleza jinsi ripoti ile ilivyoibiwa, ingawa hakufafanua zaidi akisema hizo ‘ni silaha za akiba’. Alisema amewahi kuwaambia wote wawili, Lowassa na Sumaye kwamba rushwa huanzia kichwani, moyoni kabla ya kutolewa mikononi na kwamba katika sakata la Richmond, Lowassa aliingilia mchakato kwa kumtumia msaidizi wake binafsi kupeleka maelekezo kwa Msabaha. “Leo anasema mwenye ushahidi apeleke mahakamani la sivyo afunge mdomo wake; mimi ninasema Lowassa anatafuta urais wa nchi hii nafasi ambayo hawezi kupewa mtu mwongo; mwongo hakubaliki kuwa Rais,” alisema. Dk. Slaa alikumbushia pia ufisadi wa Kampuni ya Meremeta iliyodaiwa kuwa ni mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kabla wajanja ‘hawajaidaka’ na kuitumia kuibia fedha za umma akisema Lowassa alimuonya akimwambia nyaraka anazoziandika na kuziwasilisha bungeni zinaiaibisha serikali. “Nikamjibu, nikasema hapana. Tuwatafute kwanza wanaoiba Meremeta hapo itatusaidia hata kufahamu nani alisababisha mradi wa magari wa Nyumbu ukafilisika. “Baadaye akaniita kule Speaker’s Lounge bungeni, tukawa wawili, akaja na mtu mwingine ambaye leo sitamtaja, wakaanza kunitishatisha na nikawaona na wale vijana wao, nikaogopa. Nikawaambia nyie ni mafisadi vichwani, moyoni na ndani ya nafsi zenu. “Baada ya hapo nikafungua mlango nikakimbia kuokoa maisha yangu. Nani anaweza kumwambia Lowassa wewe ni fisadi? Ni watu wachache sana wenye ujasiri huo lakini mimi nilimwambia,” alisema. Dk. Slaa aliwashangaa wananchi wanaoshabikia ujio wa Lowassa kutaka urais kupitia Chadema akidai kuwa atawasaidia kutatua shida mbalimbali, akisema: “Nendeni Monduli (Jimbo la Lowassa), hakuna maji kule! Sasa atawaletea vipi maji Watanzania wote? Nendeni Karatu (Jimbo ambalo Slaa alikuwa Mbunge kwa miaka 15) mfananishe na Monduli. “Watu wa Karatu watakwambia ukweli kuwa akiwa Waziri Mkuu, alibadili hata mpaka wa Monduli na Karatu na hadi leo kuna ugomvi. Mtu kama huyo atawezaji kutatua matatizo ya wakulima na wafugaji kama yeye mwenyewe ni chanzo?” Dk. Slaa pia liponda ujenzi wa shule za kata ambao wapambe wa Lowassa huutumia kama kete ya mafanikio yake kiuendaji, akisema mpango huo ulibuniwa mwaka 1990 nchini Thailand naye akiwa ni mmoja wa wajumbe walioshiriki wakati huo ukiitwa Education For All (EFA). Urafiki wa Lowassa na Lawrence Masha Kuhusu uhusiano uliopo kati ya Lowassa na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, ambaye naye kwa sasa yupo Chadema, Dk. Slaa alisema ulianzia wakati wa mchakato wa kuhalalisha zabuni ya Richmond. Alisema Lowassa, Msabaha na Masha walishiriki kikamilifu kusimamia mchakato uliorudiwa zaidi ya mara tatu kuiwezesha Richmond kupata zabuni ya kufua umeme wa dharura nchini kinyume cha sheria ya ununuzi. Alisema kampuni nane zilizoomba zabuni hiyo zote hazikuwa na sifa lakini wakubwa hao wakalazimisha Richmond kupewa mkataba ndani ya siku 10 badala ya siku 45, kwa mujibu wa sheria na kwamba uetetezi wa Lowassa kwamba alichukua hatua, si kweli na mtu mwongo hafai kuwa Rais. Alisema hata baada ya kashfa ya Richmond kujulikana, Lowassa na Rostam Aziz walishinikiza kampuni hiyo irithiwe na Dowans, kampuni nyingine feki kutoka Costa Rica. “Kamati ya Mwakyembe ilipotaka kuifahamu Dowans ya Costa Rica, iliambiwa kuwa Mkurugenzi wake aitwaye Zamora aliisajiri siku moja pamoja na kampuni zake nyingine 99 huku pia akiwa ni mwenyekiti wa kampuni nyingine 52 tofauti. “Hadi leo Dowans wanalipwa Sh. milioni 153 kila siku. Lowassa aje kutuambia ni nani anayepokea fedha hizo. Ninafahamu kuwa hata fedha za kampeni sasa zinatolewa na Rostam Azizi, mtu aliyewahi kunipigia simu akiniambia; ‘dokta, omba Mungu ndani ya dakika tano hautakuwapo duniani’. “Lowassa aje atuambie kwa nini Scotland Yard wanamtafuta kwa utoroshaji wa Pauni milioni 400. Mtu huyu leo anataka kuwa Rais! Haikubaliki na niseme wazi kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote lakini ni Mtanzania na nitapiga kelele watu hawa wajulikane. “Lowassa aje hadharani aseme ana hisa kiasi gani kwenye kampuni mbalimbali nchini ambazo hakuziandikisha kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,” alisema. Alihoji uadilifu wa Sumaye aliyepora eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Wilaya ya Mvomero huko Morogoro na kuihodhi ardhi ambayo hadi leo haitumiki na sasa makao hayo makuu yamejengwa pembebi ya Barabara ya Dodoma – Morogoro. Ahitimisha hoja zake Katika kuhitimisha hotuba yake hiyo ya saa moja na nusu, Dk. Slaa aliwasihi vijana aliowaimarisha ndani ya Chadema kutopiga kura kwa ushabiki bali watafakari na kufanya uamuzi sahihi huku akiponda hoja za kufunguliwa kwa babu Seya na watuhumiwa wa ugaidi Zanzibar, akisema si za msingi kwa Watanzania wa sasa. “Nilisema tangu awali kuwa nimestaafu siasa. Kwa sasa sina chama, bali nina nchi. Nimeombwa na vyama vitano tofauti nijiunge nigombee uraisa, lakini nikasema hapana, tatizo la Watanzania si urais wa Dk. Slaa; ni uadilifu wa viongozi. “Ndio maana nitaendelea kupiga kelele nje ya vyama vya siasa kwa kuwa kuna viongozi ambao si waadilifu wanataka kuchukua taifa letu. Kwa mfano mshenda wa Lowassa (Askofu Gwajima) alikuja kwangu, akaniambia ninapaswa kumuunga mkono Lowassa kwa sababu anaungwa mkono na wengi. “Nikamuuliza akina nani hao? Akanijibu kuwa kuna fedha kutoka kwa Rostam Aziz, anaungwa mkono na KKKT na kwamba kati ya maaskofu 34 wa Katoliki, 30 wamehongwa! “Nikamwambia akili yake imepumbazwa. Nikawasikitikia maaskofu wangu kwamba kama ni kweli wamehongwa, basi taifa letu linaangamia. Mshenga (Gwajima) akaniambia kuna askofu alitaka gari zuri la kiaaskofu, ndani ya dakika 20, akapewa. “Nikajiuliza hawa watu wanatoa wapi fedha? Inamaana hata hawaziweke benki kwa sababu huwezi ndani ya dakika 20 ukanunua gari la Sh. milioni 60,” alimaliza Dk. Slaa hotuba hiyo huku akisisitiza kuwa zipo silaha nyingine za akiba atazitumia mara baada ya Lowassa na Sumaye kujibu hoja hizo. Dk. Slaa alisema huenda maneno yake yakaonekana kuegemea upande fulani kwa sasa, lakini hiyo ni kutokana na ukweli kuwa ukweli lazima utakuwa upande tofauti na uongo. 
Chanzo: RAIA MWEMA

3 comments:

Anonymous said...

Huyu dokteri maslahi ni adui wa mabadiliko na demokrasia yeye kama katibu kusema ameshindwa kuhimili watu wanne halafu anatuonesha udhaifu wake wa ukiongozi kwa kuongea vitu alivyovianzisha yeye mwenyewe huo ni usaliti wapenda mababiliko ya kwa ajili ya maendeleo badala ya mazoea.

Anonymous said...

Lowassa ni rasilimali (asset) au mzigo (liability) kwa chama hicho,sasa
kwani ungeambiwa ni asset ungemkubali? kwa hivo ungelifuta madhambi yake yoye.

Anonymous said...

Hapa kazi tuu