Saturday, 5 September 2015

Mlevi alaani wakumbafu na waropokaji

          Pamoja na kupiga tubangi na kanywaji bado mzee mzima najua mipaka yangu. Najua kuwa ninapotaka kuongea lazima kuhakikisha kuwa kichwa na mdomo vinafanya mawasiliano. Huwa nahakikisha sijambi au kunonihino kwa mdomo tena usawa huu wa umri huu hata kama kufanya hivyo kunawavutia na kuwafurahisha inzi. Ninapoongea huwa nahakikisha sipayuki, situsi, sikebehi, wala kusingizia bali kutongoa ukweli.
          Mfano, hata ninapoandika kuhusu hawa wababu waropokaji na watukanaji kama Beni Tunituni wa Kiwila bado siwezi kuwaita wakumbafu hata kama ni malofa wa kimawazo na heshima bado siwezi kuwaita malofa japo kweli ni malofa. Nikiwaita malofa, wenye akili watashindwa kutofautisha kati ya lofa na tajiri wa fikra. Kwa wanaojua sayansi ya tabia na mikakati ni kwamba dalili ya kwanza ya ulofa wa kimawazo na ukumbafu ni kutumia mitusi tena ya nguoni kama silaha au namna ya kupata ulaji.
          Pamoja na kupayuka kwake, nakubaliana na Beni kuwa wapingaji ni malofa kweli kweli. Kwani kwa ulofa wao wameweza kuvua papa wawili toka chama Cha Maulaji (cCM). Si hilo tu, ukilinganisha utajiri utokanao na ufisadi na ujambazi mwingine, uwezekano wa wapingaji kuwa malofa ni mkubwa japo hakuna kipengele hata kimoja kinachowaonyesha kuwa wakumbafu. Nadhani wangekuwa wapumbavu wasingeweza kuvuna vigogo na mibuyu toka cCM.
          Sometimes, nyani haoni kundule. Sijui kama tutaanza kutafutana uchawi kati ya wapingaji na wale waliowabinafsisha wenzao nao wakajibinafsisha nani atakuwa lofa kimawazo na mkumbafu wa kweli? Sijui hawa wanaowaita wenzao wakumbafu wanamaanisha nini iwapo wao wamekaa kwenye ulaji na kuruhusu kila aina ya kibaka toka nje na ndani kuwaibia walevi? Je huu si ukumbafu wa kupindukia? Kama siyo, inakuwaje wale walioko ndani wanakosa la kusema na kuwaonyesha walevi badala yake wanakimbilia mitusi, kutumia ndata kuwatisha na kuwazuia kufanya kampani zao? Inakuwaje kama si ukumbafu wa kukaa kwenye mjengo na jumba lenyewe wakashindwa kutimiza walichoahidi hadi sasa wanaanza kutegemea mitusi, vitisho na uchakachuaji?
          Laiti hawa wanaowaita wakumbafu wenzao wangewauliza mafisadi kama akina Rugemalayer na Singasinga na wengine waliowatumia huko nyuma wangejua ni wapumbavu kiasi gani. Hivi majambazi kama wale wa RITES waliopewa reli zetu wakajiibie watakao wanadhani wanawaona washitiri wao kama wajanja au wakumbafu tu wa kawaida?
          Kawaulize wahalifu wote waliokingiwa kifua kuanzia wale walioghushi, waliofilisi mashirika ya walevi na wengine wanaouza pasi zetu na kutumia mipaka yetu kama vitega uchumi wao wanawaonaje hawa wanowaachia wakafanya uhalifu kama huu wa kuhujumu kaya. Before all benefeciaries of crimes against boozers those who allowed them to rob boozers are but goons and halfwits. Loo! Naona mibangi kanywaji na usongo vinapanda hadi naanza kuongea kikameruni bure.
          Tena kabla ya kusahau, lazima niseme wazi na kwa herufi na sauti kubwa: WALAANIWE MABINGWA WA MITUSI. Walaaniwe wakumbafu wote wanaoleta upumbavu wa kuita wenzao wapumbavu wakati wao ndiyo. Tatizo na fyatu wengine ni kwamba wakiharibikiwa wanadhani kila mlevi ameharibikiwa. Kama wewe ni mvuta bangi au mlevi basi si wote waliokuzunguka ni walevi. Kama wewe ni kibaka usidhani wote ni vibaka. Kama wewe ni lofa usidhani kila mlevi ni lofa. Kama wewe ni mkumbafu, usidhani kila mlevi ni mkumbafu.
          Kwa vile nina usongo na wakumbafu na ukumbafu, naona leo niishie hapa kwa kuwataka wakumbafu wasituletee ukumbafu na mitusi yao. Wasitujazie mbu. Watuache na amani yetu vinginevyo kuna wakumbafu watajikuta The Hague wakila ugali na wakumbafu wengine kama akina Gbagbo na Taylor. 
Maneno magumu
Ukumbafu-kufanya ndiyo siyo au bila kutumia bongo zote

Mkumbafu-yule anayefanya ukumbafu
Chanzo: Nipashe Sept., 5, 2015.

No comments: