Tuesday, 29 September 2015

Kipindupindu na wagombea urahis

   Baada ya kuona kampeni zikiendelea huku kila mgombea akija na sanaa zake za kuwaahidi wachovu neema wakati mwisho wa siku ni maafa, Kijiwe kimejitoa kimasomaso kuwataka waongelee gonjwa hili la uchafu liitwalo kipindupindu.
            Mijjinga ameingia akiwa na laptop yake leo kuonyesha kuwa mambo anayaweza. Anaiweka mezani, kuamkua na kutoa mpya, “Wazee mna habari kuwa mgombea mmojawapo amekumbwa na kipindupindu kiasi cha kuwa anakatiza hotuba kwenda msalani?”
            Kila mmoja anastuka. Mgosi anasema, “Una maana kipindupindu cha ubongo au? Maana tinaona wagombea wakisema vitu visivyoiinga akiini kiasi cha kuhisi wanakabiiwa na kipindupindu cha ubongo?”
            “Haswa. Kumbe nawe ni mwanafalsa Mgosi,” Anajibu Mijjinga huku akifuta fumbi laptop yake.
            “Hii mpya na kali! Yaani kipindupindu kimekuwa tishio hadi kukabili ubongo!” Mbwamwitu anachomekea.
            Mipawa anakwanyua mic, “Nadhani kuna ukweli usiopingika. Kuna kipindupindu cha ubongo kimekumba kampeni hizi. Maana sisikii wahusika wakiongelea katiba mpya iliyouawa na mafisadi, kupambana na ufisadi na kuondoa uoza unaoachwa na huyu anayeondoka kiasi cha kugeuka kipindupindu.”
            Msomi Mkatatamaa anatia guu, “Nakubaliana nanyi mia kwa mia. Hata kipindupindu chenyewe ambacho ni alama ya uchafu na umaskini hakiongelewi. Badala yake utasikia wasanii wakiongopa kuwa watatoa elimu bure. Kwanini msitoe elimu ya kipindupindu kwanza? Kwanini hawaongelei uchafu uliokithiri tena kwenye lisirikali ambapo wezi wanajiibia watakavyo kana kwamba kaya hii ni shamba la bibi? Nilitegemea majina kama Jimmy Rugemalayer, Singasinga, Ni zero Kadamage, Kisehna, Idd Lion na mengine yakitajwa na jinsi watakavyoyashughulikia.”
             Kapende anampoka Mgosi mic, “Mkuu hapa umewashika pabaya. Ulitegemea CcM waongelee escrow wakati waliianzisha wao na kupunyua uchache kwa ajili ya kampani ya kampeni? Ulitegemea Mr. Richmonduli aongelee uchafu wakati yeye ndiye bingwa wa kuutenda? Sidhani kama kuna mwenye ubavu wa kuongelea masuala nyeti kama vile katiba mpya au kupambana na ufisadi wakati wahusika wanaogelea kwenye uchafu huo. Ziko wapi nyumba za kaya zilizouzwa na Ben Tunituni Makapu wakati Dk Kanywaji alipokuwa waziri mhusika?”
            “Du mzee unapiga huku na kule bila kupindisha!” anachomekea Mchunguliaji.
            Kanji naye anaamua kukamata mic, “Dugu zangu hii pindupindu natisha sana. Sasa kama siasa kuba naharisha hadi nakimbia hotuba sisi vatu dogo takufa.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu, “Ni kweli Kanji. Sisi wadogo tutaangamia hasa ikizingatiwa kuwa tunakunywa maji ya visima vilivyojaa kinyesi. Hivi unategemea nini wakati visima vyenyewe vimechimbwa jirani na vyoo?  Huko chini maji yanaingiliana na hii ndiyo sababu kubwa ya wengi kuugua kipindupindu. Pia hatuna uwezo wa kwenye Ugabacholini kutibiwa kama wao.”
            Mpemba anashika mic, “Yakhe mie nshangaa hii roho mbaya ya hawa wasanii wetu wallahi. Waongelea vitu vya ndotoni wakati matatizo ya wazi wayaona na kujifanya hawayaoni. Heri hicho kipindupindu kingewakamata si ubongoni pekee hadi kwenye matumbo yao ili waonje joto ya jiwe wallahi.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anakamua mic, “Dua la kuku halimpati mwehe kaka yangu Mpemba. Nadhani tatizo la kipindupindu ni la wachovu wenyewe. Wanapaswa kuanza kuchukua hatua za usafi ambazo si lazima wafundishwe. Hapa lazima tujilaumu wenyewe kwa kuingiliwa na gonjwa hili.”
            Mgosi Machungi anarejea, “Da Sofia nakuheshimu sana. Kama kuingiiwa si sote bali nyinyi mnaokii kuingiiwa. Nadhani wangeiingiwa wao kwanza ili kuonyesha kuwa viongozi wako mstai wa mbee ingekuwa poa.”
            Mzee Maneno anakula mic, “Waingiliwe mara ngapi wakati wameishaanza kuonyesha jinsi wanavyoharisha majukwaani? Hukumsikia aliyedai ataondoa umaskini kwa njia ya kutenda ufisadi kama ule wa Richmonduli? Hukumsikia mwingine aliyesimamia wizara ya ardhi akisema kuwa lisirikali liligawa ardhi vibaya utadhani yeye hakuwa kwenye lisirikali hilo? Hawa sidhani kama wana jipya zaidi ya kueneza kipindupindu cha kisiasa.”
            “Mzee Maneno una maneno kweli kweli. Umekumbusha habithi anayetembelea mashangingi kusema eti ataondoa mashangingi na kutumia hiyo njuluku kwenye kutoa elimu. Angekuwa serious si angepanda bajaj kam alivyofanya papa Francis kwa Joji Kichaka alikopanda bajaj na kukataa Beast la Obamiza? Wasanii, wanafiki na waongo watupu. Huwezi kuwa ndani ya Nambari Wani au UKAUA ukawa na jipya zaidi ya kipindupindu cha ubongo.” Anachombeza Kapende huku akibofya ki-Sumsung Galaxy 6 chake.
            Mpemba anarejea, “Mie naona walougua kipindupindu cha tumbo na ubongo ni wale waniodanganywa kwa ahadi hewa huku wengi wao wakiwaomba rushua wagombea ulaji. Kwani hatuoni mitaani ambapo nshiko watembezwa? Kama hawa waniodanganywa hawana kipindupindu sehemu zote inakuwaje wakubali hadaa na urongo wa nchana kana kwamba hawana akili?”
            Kanji anakatua mic, “Dugu yangu Pemba mimi penda veve sana. Nasema kweli tupu dugu yangu.”
            “Angalia Kanji. Eti umisema unampenda sana ii iweje dugu yangu? Veve napenda yeye vipi na kwanini. Hebu tieeze tieewe.” Anachomekea Mgosi huku akiangua kicheko.
            Mijjinga anyakua mic, “Tuache utani. Bila kuuondoa huu mfumo wa kifisadi hata aje malaika atatuambukiza kipindupindu cha ubongo kama hawa wanavyofanya. Sioni mstakabali wa kaya kwenye kampeni hizi zinazolenga kuamuliwa kwa kuangalia watu na siyo sera. Wengine wakiongea utadhani wamemeza chura.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si kunguru aliyeugua kipindupindu akatuharishia!
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 30, 2015.

No comments: