The Chant of Savant

Sunday 2 August 2015

Rais ajaye ajifunze kwa Kikwete


     Japo si rahisi kutabiri nani ataibuka mshindi kwenye uchaguzi ujao na kuwa rais wa Tanzania atakayechukua ukanda baada ya miaka kumi ya hasara ya rais Jakaya Kikwete, kilicho wazi ni kwamba hapo Oktoba lazima Tanzania ipate rais mpya. Pia hakuna ubishi kuwa rais anayeondoka Kikwete ameacha legacy kubwa hata kama ni yenye kutia walakani. Kwa miaka kumi–si haba–Kikwete ameacha mengi ya kusimulia. Kama watanzania watajifunza tokana na makosa waliyofanya kumchagua Kikwete huku wakijua hakuwa na sera zaidi ya umaarufu tata, controversial popularity, watafaidika toka kwa Kikwete kwa kutorudia makosa. Badala ya kuangalia sifa uchwara tena za kuchongwa, wataangalia sera na kile wanachohitaji huku wakiangalia taasisi badala ya mtu binafsi.
Kitu kingine ambacho rais mtarajiwa anapaswa kusoma sana ni ile tabia ya Kikwete kupenda kusafiri sana kuliko kukaa ofisini. Watanzania hawakulipenda hili. Kwani kufanya hivyo kumeliingiza taifa hasa kubwa. Rejea kuumka kwa deni la taifa bila maelezo ya kina. Rais ajaye awe mchapakazi anayekaa ofisini na si mzururaji. Asikubali kupewa majina ya kejeli kama vile mtalii, mzururaji au           Vasco da Gama na mengine mengi. Pomoja na kwamba Kikwete na wapambe na waramba makalio wake walitanua na kufaidi, waliwaumiza sana watanzania maskini ambao wangetaka rais mwenye nidhamu ya matumizi ili kuwapunguzia mzigo.
Sifa nyingine ambayo Kikwete wala hakuionea aibu ni kuombaomba, kwani kila watu walipolalamika kuhusu uzururaji wake, alisema kuwa anafanya hivyo ili kuomba misaada. Wengi walihoji mantiki ya nchi yenye raslimali na uongozi uliowaaminisha ungefanya mabadiliko kuombaomba wasipate jibu. Kwa ufupi ni kwamba watanzania hawakulipenda hili kutokana kulidhalilisha taifa hasa lenye raslimali nyingi lakini bado likaishi kwa kubomu.
Kuunda serikali kubwa na kuongeza idadi ya mikoa bila sababu za msingi zaidi ya za kisiasa na kujuana.
Kikwete atakumbuka kama rais aliyewahi kutoa ahadi nyingi hewa huku asitekeleze hata moja. Yako wapi maisha bora kwa wote? Kuko wapi kufumua na kuunda upya mikataba ya kijambazi ya uwekezaji? Badala ya kuifumua na kuisuka upya –kama alivyokuwa ameahidi –aliingia mingine kama vile Richmond. Kuko wapi kukuza uchumi, kubana matumizi na kutumia kwa busara? Sana sana alichofanya Kikwete ni kutumia bila nidhamu ya matumizi huku akipoteza muda mwingi ugenini. Hata mawaziri wake wengi walikuwa wakifanya kama alivyokuwa akifanya bosi wao. Kumbuka. Jongoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani. Wengi waliuita mchezo huu usanii. Rais ajaye asiwe msanii. Hili lilijihidhirisha wazi baada ya Kikwete kuwapenda na kuwajali wasanii wenzake kuliko wengine. Rejea uteuzi wenye utata wa majaji, mabalozi, wakuu wa mikoa na wilaya. Kikwete ameteua watu wengi wenye utata ama kwa kulipa fadhila au tokana na kujuana.
Kikwete p ia aliahidi kuwa serikali yake ingepambana na ufisadi, rushwa, ujambazi, mihadarati na mengine. Hata hivyo, ukiangalia jinsi maafa haya yalivyozaliana na kuongezeka huku Kikwete akijfanya kama hayaoni wala kuyajua, unagundua ni kwanini Kikwete ameacha sifa mbaya ambayo inapaswa kumchukiza rais ajaye.
 Ahadi nyingine aliyoitoa Kikwete ni ya kuandika katiba mpya. Muulize. Je aliandika au kuichakachua huku taifa likiingia hasara bila sababu yoyote.
Kitu kingine ambacho watanzania watamkumbuka Kikwete kwa uchungu na chuki ni matumizi mabaya ya ikulu. Rejea kuundwa kwa NGO ya ulaji ya mke wa Kikwete na mwanae kujiingiza kwenye biashara na siasa si kwa sifa bali jina la baba yake.
Ukiachia mbali hayo hapo juu, Kikwete atakumbukwa kama rais aliyewakingia kifua mafisadi na walioghushi sifa za kitaaluma. Nani hajui kuwa baraza la mawaziri la Kikwete lilijaa watu wengi walioghushi huku wengine hata walipokataliwa kwenye majimbo yao akawateua mabalozi kama Dodorus Kamala. Kikwete ataondoka na kukumbukwa na mafisadi kama wale wa EPA, Richmond, Kagoda na Escrow ambao wengi wao watam-miss sana. Rejea kuendelea kulipwa marupurupu na mafao kwa waziri na swahiba na mshirika wake Kikwete, Edward Lowassa ambaye hakustaafu ukiachia mbali kutomfikisha mahakamani.
Kitu kingine ambacho rais ajaye anapaswa kujifunza toka kwa Kikwete ni matumizi ya vyombo vya dola. Kikwete atakumbukwa kwa kuwaamuru polisi kuua raia na kuwanyanyasa wapinzani. Hili si jambo bora kwa nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia.
Hata hivyo, mara nyingi kila kitu kina sura mbali. Wapo watakaomkumbuka Kikwete kwa kujenga barabara nyingi hata kama viwango vyake ni suala jingine. Kadhalika watamkumbuka kwa ujenzi wa shule za sekondari za kata hata kama ni kata kweli kweli kuwa zinawakata watahiniwa kwa kupata elimu dhaifu.
Kitu kingine alichofanikiwa kufanya Kikwete ni kufanya urais uwe urahisi jambo ambalo rais ajaye anapaswa kulipiga vita kweli kweli kwa kurejesha uchapakazi na maadili ya utumishi wa umma badala ya madili.
Hata hivyo, ukilinganisha mema ya Kikwete na mabaya yake, unakuta kuwa hana lolote la maana analoacha nyuma kama mtaji kwake. Wahenga walinena kuwa baya moja hufuta mema yote.

Kwa ufupi ni kwamba Kikwete alikuwa rais dhaifu na asiye na msimao kuliko aliyewahi kutokea ukiachia mbali kutojali na kufanya mambo hovyo hovyo.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 2, 2015.

1 comment:

Anonymous said...

Rais aliyepata PHD
Hakuna Duniani