Tuesday, 11 August 2015

Kijiwe chamkaribisha Prof Pumba

Baada ya kushuhudia Tsunami kwenye kambi ya upingaji magwiji kupukutishwa kama wadudu, Kijiwe kimeamua kuwapa tafu lau wakapoze machovu na kutumiwa kwa muda mrefu wasijue.
          Mpemba anaingia na gazeti la Danganyika Ever. Anaonekana mwenye furaha. Lazima ana jambo. Anaamukua, “Assalaam alaykum jamia.”
          Kwa pamoja tunajibu, “Wallaikum Salaam”.
          Anazoza, “Jamani mmeona kuwa maneno yetu yatimia hata kabla ya mwezi kupita?” Anampa gazeti Mgosi Machungi huku Mchunguliaji akionekana kukereka kwa kutopewa yeye.
          Wote tunamtazama Mgosi tukingoja atutongolee kilichojiri hadi Mpemba anaingia na bashasha.
          Punde tu baada ya ku-peruse, Mgosi anasema, “Tiisema kuwa ndoa za kisiasa zitavunjika. Sasa tazama na Poofwesa wa Uchumi ameamua kujitoa kwenye Kafu.”
          Mipawa anadakia, “Walitupuuzia tulipoonya. Na bado tu. Wengi watajiondoa kwenye uchafu huu wa kujitakia tokana na uroho wa njuluku na maulaji.”
          Msomi Mkatatamaa anaamua kutia buti. Anakohoa kidogo na kuzoza, “Hili liko wazi kama tulivyotabiri. Hata hivyo, msishangae. Ni jambo la kawaida hasa kwenye siasa nyemelezi na za uchumia tumbo. Kama alivyosema Mipawa, wengi watatimka kusaka kitumbua baada ya kuona walipo kimetiwa mchanga.”
          Mijjinga anakula mic, “Mimi namngoja mbunge wangu ambaye alitutelekeza kwa miaka mitano halafu sasa anajifanya kutukumbuka, kutupenda na ni mwenzetu wakati ni msaka tonge wa kawaida. Sijui atatwambia au kutuonyesha nini wakati hakufanya lolote la maana kwa miaka mitano.”
          Kanji anakwanyua mic, “Hii Pumba iko ondoka kati baya sana kwa KAWA. Tuliambia yeye hapana pwakia Luwasa lakini hapana sikia. Sasa ona vatu yote ya maana nagatuka KAFU. Hasara kuba sana dugu yangu.”
          Sofia Lion aka Kanungaembe ambaye siku hizi anatofautiana kidogo na mshikaji wake Kanji anakwanyua mic na kuzoza, “Sioni cha kutuhangaisha hapa. Kwani ukuti mmoja ukiondoka kwenye nyumba inadondoka? Acha ajiotoe japo viherehere wameishaanza kusema amenunuliwa. Alipoondoka Luwasa toka CcM hakununuliwa. Akitoka kwao kwenda kwingine amenunuliwa. Siasa hizi ni za kichovu na za kizamani.”
          Kapende anaamua kumchomekea Sofi. Anakula mic, “Japo sikubaliani na namna wapingaji walivyompwakia Luwasa, ningetamani huu uoza uliopo uondoke. Ni bahati mbaya kuwa hautaondoka kutokana na tamaa, upogo na kujikanganya kwa wapingaji huku wakiendekeza maslahi binafsi. Nadhani kuna mkono wa mtu kwenye haya yanayotokea hasa ikizingatiwa penye udhia penyeza rupia.”
          Msomi anarejea na kuuliza, “Kapende umeniacha hoi kwa uchambuzi wako wa kitaalamu. Je hapa nani amemhonga nani na nani amehongwa na nani? Unataka kusema kuwa sasa siasa ni biashara?”
          Kapende anajibu, “Sure, unadhani kupokelewa kwa kishindo kwa Luwasa ni bure hasa ikizingatiwa kuwa anajua kutembeza nshiko? Kama kuna waliokatiwa wakaminya kuwakatia wenzao, nini tatizo nao wakigoma au kukatiwa wakati kila mtu anaangalia kitumbua chake?”
          Msomi anajibu, “Umejibu kifalsafa. Message sent. Lolote linawezekana.”
          Mpemba anakatua mic, “Hata mie nshangaa sana wallahi. Maana ukiangalia profesa alivokuwa akisifia huu mpango wao uchwara usingedhani angetema ulaji kirahisi hivi wallahi. Mie naona nchukue hii fursa kunkaribisha kijiweni aje tujadili masaala ya maana kwa vile kule anshindwa.”
          Mzee Maneno anakatua mic, “Hapa lazima tumpe jukumu Msomi mwenzake amfuate huko aliko amkaribishe kuja kujiunga nasi wasomi wenzie ili tutoe upinzani wa kutosha kwa CcM na CcM B inayowakilishwa na UKAUA ambao wameamua kujiua kwa upogo na upofu wao.”
          Mijjinga anarejea, “Jana nilikuwa na mtu wa karibu wa Dk Kanywaji Makufuli. Anasema CcM wameshangilia na kufurahia kujiengua kwa Pumba kwa vile watazidi kupata nguvu wakati Luwasa na UKAUA wakizidi kujiua bila kujua.”
          Mgosi anapoka mic, “Hata mimi jana niiongea na mtu wa keibu na Dk Silaha na ameniambia kuwa hivi keibuni naye atajiondoka CHAKUDEMA na kujiunga na CcM. Kwei hai hii inatichanganya sana japo sisi tikiitumia vizui tinaweza kuchukua kaya au vipi?”
          Mheshimiwa Bwege anakwanyua mic, “Hebu tuwe wakweli. Hivi siku zote mmekuwa mkiamini kuna upingaji au kusaka tonge? Nijuavyo mimi sioni tofauti ya wanaopinga na wanaopingwa hasa ikizingatiwa kuwa wanagombea kutunyonya sisi na si vinginevyo. Hivyo, vita ya kunguru neema ya panzi. Acha wavuane nguo ili nasi tupate jinsi ya kuwashughulikia. Natamani kwenye uchakachuaji ujao asipatikane mshindi ili wafunge ndoa ya mkeka na kutoana macho nasi tufaidike au vipi?”
          “Kwa jinsi walivyoburuzana hata ningekuwa mimi ningejiondoa. KAFU walikosea kitu kimoja. Baada ya kulazimisha ndoa ya mkeka kule Zenj walizoea. Najua hata kwenye UKAUA hawapapendi sema wanataka kuongeza nguvu ili pale watakapoanza kutoana ngeu hapo Oktoba iwe ni pande zote za muunganiko. Maana nikiona Luwasa na Madevu walivyopania urahis, sijui kama watakubali matokeo bila kuanzisha fujo. Hivyo, asiyetaka fujo lazima ajiondoe mapema. Nitafanya mpango wa kumfuata Prof aje ajiunge nasi tutoe upinzani wa kweli,” Msomi anazoza.
          Sofia anabeza, “Nenda ukamkaribishe na Luwasa aje awabomoe kama alivyowafanyia UKAUA. Halo halo! Sisi na Makufuli yetu tunatesa.”
          “Unalinga na makufuli wakati tumeona mafunguo na hayakufanya kitu? Kwa taarifa yako sisi ndiyo wenye funguo za hayo makufuli yako,” anazoza Mzee Kidevu huu akimwangalia Sofi kwa jicho baya.
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapaki shangingi la Prof Pumba na kujiunga nasi tayari kwa kupata kahawa!
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 12, 2015.

No comments: