Friday, 28 August 2015

Leo mlevi anachonga na CcM


          Wiki jana tulichonga na muishiwa, sorry, mhishimwa Eddie Luwasa baada ya kutupiga changa la macho kuwa angewajaza mafweza wachovu hadi wajihisi wako Uswizi. Punde si punde, si Chama cha Maulaji (CcM) kikarudia ujinga, sorry, mchezo ule ule! Hii–kwa kitasha–huitwa counterstrategical approach. Sijui ni kwa sababu Luwasa na CcM wote ni dugu moja. Mie sijui.
          Baada ya kumsikia Luwasa akitishia kuifanya Bongolalaland Uswizi, CcM wamejivuvumua kuja na hoja kubwa nne ambazo ni kupambana na uchovu, kutengeneza ajira, ulinzi na usalama na kupambana na rushwa.
          Niliposikia ahadi hizi ilibidi kwanza nipate kanywaji na bangi kidogo ili kutuliza mshangao niliopata.  Sasa–kama bado kuna umaskini tena wa kunuka–ina maana ile sera yenu ya Best Life for All (BLA) ilibuma nini?  Je hamuoni kuwa mnakiri kuwa kwa muda mliokuwa maulajini mkitanua na kutanuka mlieneza umaskini?  Mlitegemea nini mlipoachia majambazi kama wale wa Escrow wakahomola kana kwamba kaya hii ni shamba la bibi? Nadhani kama ni kufuta umaskini basi mngewapitisha Jimmy Rugemalayer na Singasinga waliomtajirisha Anna Kajuamlo Tiba-Ijuka akachanganyikiwa; akasahau dhamana yake.
          Yote tisa. Kumi, mliniacha hoi pale mliposema eti mna mpango wa kupambana na ufisadi wakati kwa kipindi chote kilichopita mlihulalalisha karibu katika kila kona. Yupo mlevi mmoja–jina kapuni–aliyesema kuwa kweli nyinyi na chata la sanaa, mizengwe na ahadi hewa. Maana haiingii akilini kusema eti mnapambana na umaskini wakati mliueneza kwa kuushiriki na kuupamba ufisadi hadi wachovu wakaendelea kupigika wakati nyinyi mkipiga mabilioni.
          Hili la ulinzi na usalama limeniacha hoi hadi kuongeza dozi ya kanywaji na bangi ili kuepa kunyotoka roho (kufa) kwa mashambulio ya ugonjwa wa moyo. Je waandishi wa umbea nao wamo? Je akina Ulimboka na Kibanda nao wamo kwenye mpango wenu huu wa ulinzi na usalama wakati ndiyo sheria za kuwabana na kuwang’oa meno na kucha zinazidi kupeta huku tukiona watuhumiwa wakipelekwa majuu kuula kama mabalozi? Hivi Rama Ighon-du aliyemsulubu Ulimboka yuko wapi siku hizi?
          Je katika ulinzi na usalama wenu utahusisha wachovu wote? Nashangaa sana. Hasa nikizingatia kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe wanaendelea kunyotolewa roho ili viungo vyao kutumika kutengeneza utajiri baada ya ufisadi na ujambazi kubarikiwa. Mbona hamkuongelea kukuza elimu ambayo akina Dk Shukrani Kawa-dog walinyotoa huku wakipelekea vitegemezi vyao kupata elimu ya haja ughaibuni ukiachia mbali kughushi tena kukifanywa na wazito kukihalalishwa? Hivi mnaweza kunipa sababu japo moja ya wale wazito waliotuhumiwa kughushi kuendelea kushika nyadhifa kwenye ofisi za umma?
          Mliposema mtatengeneza ajira mmeniacha hoi. Je hizi ajira hewa mnazopanga kutengeneza ni kwa ajili ya wachovu au washikaji na vitegemezi vyenu? Ajira gani wakati mmeruhusu wachukuaji mnaowaita wawekezaji kuendesha biashara bila kulipa kodi ukiachia mbali kutujazia wamachinga toka India, China, Uturuki na kwingineko? Mnadhani tumelewa sana kiasi cha kutowaona machinga wa kigeni wakijaa mitaani na kuwatupa nje machinga wazawa? Je mna mpango wa kutumia Ben-Tunituni Makapi strategy ya kuwapa laivu wachovu kuwa nguvu ya maskini ni mtaji wake? Je mtaji wa wajinga ni nini hasa wale watakaoingia mkenge na kuona kuwa sasa mambo mswano wakati ndiyo mabalaa yanaongezeka kutokana na kubadili walaji?
          Kwa vile simo kwenye kuingizwa mkenge huu, siamini mnayosema ndiyo mtakayotenda. Najua wazi.  Mtasema msiyotenda na kutenda msiyosema kama mlivyozoea.
          Message sent. Insh’Allah tukutane wiki ijayo. 
Chanzo: Nipashe Agosti 29, 2015.

No comments: