The Chant of Savant

Saturday 15 August 2015

Walevi kumuaga Njaa Kaya kisanii


          Baada ya wasanii wenzake kuwezesha na chama chake kuandaa sherehe za kumuaga msanii mkuu, na walevi wamepanga kufanya hivyo japo jamaa hakuwa mlevi mwenzao na alipandisha bei ya kanywaji. Kwa vile walevi ni wachovu na hawana mfadhili, wamepanga kumualika jamaa Uwanja wa Fisi na kumpa ofa ya kanywaji na mapupu lau ajue maisha wanayoishi.
          Japo si kawaida ya walevi kujikomba, kwa spidi anayokwenda nayo jamaa ya kuanga ughaibuni na kwa ujumla, tusipochangamka kuna uwezekano jamaa akakitoa bila kupata serfie nasi. Lazima tumualike aje tumuonyesha tulivyopigika chini ya sera zake holela za uchukuaji aliouita uwekezaji.
          Hatujui kama wakulima watapata fursa ya kumuita na kumuandalia sherehe ya kumuaga wakati ndiye aliyepaswa kuwaaga. Ama kweli usanii unalipa. Maana ukiangalia huku kuagana hujui nani anamuaga nani na kwa lipi hasa ikizingatiwa kuwa walevi na wakulima wanaendelea kupigika.  Kwa vile sisi tumepigika, hatutampa zawadi yoyote zaidi ya kumbomu kitu kidogo lau tupate kanywaji.
          Litakuwa jambo la kushangaza kama wakulima maskini wa makondeni wataandaa sherehe za kumuaga ilhali wamepigika kulhali tena chini ya sera zake za uchuuzi, uombaomba na kopakopa.
           Kwanza, ndiyo wanaoumia na ndiyo wengi wanaoendesha kaya hii kwa kutoa msosi wakati wengi wa wasanii ni wachafuzi wa maadili ukiachia mbali wengine kuwa wakimbizi wa kiuchumi toka kaya nyingine.  Hakuna kitu kiliniacha hoi kama vihereni na minyoo ya ajabu ajabu! Ama kweli ushoga unaanza kuingia taratibu tusipoangalia. Hivi vihereni si bure hadi mjengoni!
          Huwa sijui ni kwanini hakuanza na wafanyakazi ambao wanawezesha hata hao wasanii kupata mshiko kwa kuwauzia usanii wao? Kwanini hakuwaaga walevi ambapo hawakumpa hardtime wakati akifanya usanii na utanuaji wake?
          Kimsingi, maswali bado ni mengi kuliko majibu.  Wasanii lazima waheshimike. Wanaagwa kwanza kuliko hata wasoja na mandata kwanza, kwa vile ndiyo waliompa kampani ya kufanya usanii wake kwa miaka kumi bila kufurushwa au ku-Gaddafiwa? Maana kwa alivyotunisha deni la kaya kwa kutanua na marafiki zake na shoga za bi mkubwa, bila shaka ataacha bonge ya pengo ambalo huenda litagharimu maisha ya walevi kama siyo vitegemezi vyao.
          Hivi kweli na waendesha mikokoteni na watembea kwa miguu ambao amekuwa akiwafungia barabara ili apite kuwahi uwanja wa ndege kwenda kutanua kama nao watapata ubavu na uchache wa kumuandalia sherehe za kumuaga wakati wengi aliwalostisha?
          Sijui kama wamachinga nao watakuwa na hamu ya kumuaga hasa ikizingatiwa kuwa jamaa aliruhusu machinga wa kichina, kigabacholi na sasa kituruki kufurika kaya huku wakizidi kuminya fursa kidogo iliyopo kwa ajili yao.
          Ina maana huyu njemba asipoandaliwa sherehe za kuagwa angeishia bila kuaga hasa ikizingatiwa alivyoungaza mabilioni kwenda ughaibuni kuaga huku akingoja aandaliwe sherehe za kumuaga. Huu ni uonevu na unyonyaji fulani. Mbona ughaibuni hakungoja wamuandalie sherehe na badala yake alijipeleka mwenye au ni kwa vile ni ughaibuni anakolipwa per diem kwa kwenda kutanua?
          Je kwanini ameanza na ughaibuni na kufuatia wasanii hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchakachuaji? Yupo mlevi mmoja fyatu aliyetuacha hoi kwa kusema kuwa jamaa ameanzia kuaga ughaibuni kwa vile atapamiss kutokana na kuwa bonge la Vasco da Gama. Pia anasema lazima wasanii wamuage mwenzao kwanza kabla ya wengine kwa vile yeye alikuwa msanii mkuu.
           Ukiachia mbali na hayo, lazima wasanii wawe na thamani kuliko hata wapika kura ya kula kwa vile ndiyo hao hao watakaotumika kupiga kampeni kwa kuwaweka sawa wapika kula hasa wa kule uswekeni ambao huwaona wasanii uchwara mali wanapokwenda kule kubangaiza wasijue nao ni wabangaizaji kama wao sema tofauti ni kwamba wale ni wasanii na wanabangaizia downtown wakati wakulima wanabangaizia mashambani.
          Wapo walevi wanaoona kama jamaa anaubariki ubangaizaji ambao mara nyingi husaidi lisirikali kupeta bila kutoa huduma kwa umma kwa vile kila ngurumbili anakuwa bize na ubangaizaji badala ya kulikaba lisirikali. Huoni mikashfa kama escrow ilivyonyongwa na hakuna anayehoji kwa vile kila mtu yuko bize kwenye ubangaizaji, ufisadi, ujambazi, uuza bwimbwi, usanii na upuuzi mwingine.
          Hakuna kilichowaacha hoi walevi kama kushuhudia hata wahamiaji haramu wanaosaka ulaji kupitia usanii uchwara kama kuchafua maadili nao eti kupata serfie na msanii mkuu.  Hamkuwaona wale wachafuzi wa maadili toka kwa akina Pedejee nao eti wakipiga picha naye. Wamepata uhalali lini au ni yale yale kuwa wanajua kuwa hii ni kaya na wasanii, wachumia tumbo na ngurumbili wasio makini? Kwa kaya makini kitendo hicho kwanza kisingetokea ukiachia mbali kuwa lupango sasa wakingoja kurejeshwa kwao wakachafue huko huko.
          Kwa vile huu ni msimu wa kuagana na kuombana kula, acha nikitoe nikapate kanywaji na tubangi tayari kujiandaa kumpokea msanii mkuu lau nipate serfie naye. Ama kweli urahis siku hizi umekwisha thamani! Zama za mzee Mchonga kila msanii amuage mkuu! Kakwambia nani? Acha kila fisadi autake urahis uliokuwa urais zama zile.
Chanzo: Nipashe Agosti 15, 2015.

No comments: