The Chant of Savant

Tuesday 11 August 2015

Ndoa ya Lowassa na UKAWA, urais, taifa na maslahi binafsi

 
Baada ya waziri mkuu aliyeachia ngazi tokana na kashfa ya Richmond, Edward Lowassa kuhamia rasmi kwenye upinzani, bado amezidi kuongeza utata juu ya utata. Wapo wanaoona kama Lowassa amefanya maamuzi magumu na kuchukua hatua mujarabu. Pia wapo wanaopinga hatua hii na kuona ni kama matokeo ya tamaa urais kwa upande wa Lowassa na uchumia tumbo kwa upande wa upinzani.
Wale wasiokubaliana na uamuzi wa Lowassa wanaona kama amejimaliza na kuuchafua upinzani kiasi cha kukosa kuaminiwa na umma tena hasa kutokana na jinsi ulivyokuwa ukimsakama na kumuonyesha kama mtu asiyefaa kushika madaraka makubwa kama haya hasa kutokana na kuhusishwa na ufisadi wa kutisha.

Sasa si uvumi tena. Lowassa ametua CHADEMA. Wengi wanangojea kuona hatua nyingine atakayopiga Lowassa kwenye nyumba yake mpya.  Hata hivyo, maswali ni mengi kuliko majibu. Wapo wanaohoji: Je asingeahidiwa kuwa mgombewa kwa tiketi  ya upinzani angehama? Je hapa nani anamtumia nani na matokeo yake ni nini kwa watanzania? Je ikitokea wakamkatalia kugombea atarudi CCM na je CCM watampokea au ndiyo utakuwa mwisho wa Lowassa kisiasa?

Kimsingi, wengi wanashuku ndoa hii ya mkeka kati ya Lowassa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Kwani inakuwa vigumu kuwaelewa upinzani hasa namna watakavyoweza kuweleza wananchi haya mapenzi ya haraka na imani vimetoka wapi na sababu yake ni nini. Kitendo cha upinzani kumpwakia na kumpokea Lowassa kiasi cha kukiuka yale waliyohubiri kwa muda mrefu kimefanya kuwepo hata hisia zaidi ya siasa.  Maana wapo wenye hisia kuwa huenda kuna biashara nyuma ya pazia ambapo mhusika amenunua tiketi toka kwenye upinzani ambao umethibitisha kuwa kumbe ulikuwa ukipiga kelele tu. Haukuwa na mkakati wa kuweza kukishinda Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiasi cha kulazimia kuramba matapishi yake tena ya jana. Je ujio wa Lowassa kwenye upinzani ni Baraka au laana ambayo matokeo yake yatazidi kuudhofisha na kuunyima heshima mbele ya watanzania?

Ukiangalia sababu za Lowassa kujiengua CCM na kuelekea upinzani unagundua kuwa hata kama akibahatika kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya upizani na akashinda uchaguzi, anaweza kuwa tatizo zaidi ya suluhu. Je Lowassa amehama kulipiza kisasi, kutimiza ndoto ya urais au kujikoa kisiasa baada ya CCM kuonyesha wazi kumchoka na kumtosa kwa mara nyingine?

Je nini sababu ya UKAWA kumpokea na kumkweza Lowassa kiasi cha kuwaacha walio wengi midomo wazi? Je ni ile hali ya kujua kuwa hawakuwa na ubavu wa kuishinda CCM? Je ni mbinu ya kuishi kisiasa? Je hatua hii itazaa matunda au kuumaliza upya upinzani?

Kwa namna upinzani ulivyokuwa umembomoa Lowassa, utakuwa na kibarua kigumu kuwashawishi wapiga kura na watanzania ili auzike. Wengi wanadhani Lowassa asipewe tiketi na badala yake atulie kwenye upinzani akiusaidia kuiangusha CCM huku akibakia kuwa mtu muhimu katika upinzani na kwa taifa. Kama wote wataendekeza maslahi binafsi, uwezekano wa Lowassa kugeuka laana kwa upinzani ni mkubwa kuliko kugeuka baraka. Itakuwa jambo la ajabu kama wote wawili hawataiona hatari hii wakashikilia siasa za majaribio (Experimental politics). Maana inashangaza kuona magwiji wa upinzani tena madaktari wa falsafa kushindwa kutambua jambo rahisi kama hili. Kwanini Lowassa apate anachokitaka wakati upinzani ukose ulichopigania na kujiandalia kwa muda mrefu?  Nadhani, kama Lowassa atapitishwa kuwa mgombea wa upinzani atakuwa –licha ya kupata nguvu ya ajabu na haraka –na kila sababu ya kuuburuza kama alivyowahi kufanya Augustine Mrema ambaye kuhamia kwake NCCR-Mageuzi kulikiua chama na akageuka kuwa laana badala ya baraka. Je ni upofu kiasi gani kwa magwiji kama wa upinzani kushindwa kuisoma historian a mafunzo yake? Ama kweli tamaa mbele mauti nyuma walisema wahenga.

Kwa wenye kujua malengo binafsi ya Lowassa na malengo ya kitaifa ya upinzani, inakuwa vigumu kuona namna ya kusuluhisha tofauti hizi kimilengo na kimkakati. 

Ukisoma maoni mengi ya watanzania karibu kila sehemu, wenye shaka na ndoa ya Lowassa na UKAWA ni wengi kuliko wanaoiunga mkono. Kinachofanya ndoa hii kuwa ngumu ni ile hali ya wachumba kuwahi kutuhumiana mambo mengi machafu ambayo si rahisi kuyasafisha ndani ya muda mfupi. Na kama sikosei, CCM wataitumia hali hii vizuri kuzidi kumuumbua Lowassa kiasi cha upinzani kuishia kujilaumu baadaye baada ya uchaguzi ujao. Kumpokea si jambo baya. Maana, ni haki ya kila anayetaka kujiunga au kujitoa kwenye chama. Jambo linaloonekana kuwa baya ni kile kinachoonekana kama upinzani kuvunja kanuni zake na ahadi zake kiasi cha kumpa nafasi na hadhi ambayo Lowassa kimsingi hastahili. Je wamempima na wana uhakika gani kuwa kama atashindwa kupata anachokitafuta hatawafanyia kama alivyowafanyia CCM? Ama kweli mwenye mapenzi haoni hata kama macho anayo. Lowassa ni mtu anayejiona kuwa na nguvu kuliko chama. Hivyo, upinzani hauna namna ya kuipunguza au kui-control nguvu hii tokana na kumkubalia kila kitu haraka. Hata hivyo, tungoje tusikie vigezo vitakavyotolewa na UKAWA juu ya kumpokea na hata kumpitisha awe mgombea wake.

Tumalizie kwa kuwashauri Lowassa na UKAWA kuepuka maslahi binafsi na badala yake waangalie alama za nyakati na ukweli wa mambo kwa kuidurusu hali hali ya siasa za Tanzania. Nakumbuka, hata Raila Odinga, waziri mkuu wa zamani wa Kenya alipohamia upinzani toka KANU hakugombea urais zaidi ya kutumia umaarufu na nguvu yake kuunga mkono mgombea wa upinzani Mwai Kibaki na kushinda baada ya kutamka kauli yake maarufu KIBAKI TOSHA. Tunadhani hata Lowassa alipaswa kusema, MGOMBEA WA UPINZANI TOSHA badala ya kuhangaika na kugombea urais mwenyewe. Hii inaweza kufanya safari yake ya matumaini kuishi kuwa safari isiyo na matumaini chochote bali anguko jingine la kisiasa.
Chanzo: Dira

No comments: