Saturday, 29 August 2015

Je ahadi za CCM zinauzika?

Uchaguzi mkuu uko mlangoni kwa sasa. Wanasiasa na vyama vya siasa nchini wamo tena uwanjani wakijinadi kwa mbinu hizi na zile. Wapo wanaotumia–au tuseme–wanaokuja na mapya wakati wengine wakija na wimbo ule ule wa jogoo. Mojawapo ya vyama vilivyokwisha kutoa ahadi zake katika uchaguzi ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimetoa ahadi kuu nne kinachodhamiria kutekeleza kama kitapewa ridhaa ya kuongoza tena.
Ahadi ambazo CCM inalenga kuzinadi –na hatimaye –“kuzitekeleza” ni pamoja na kupambana na umaskini, ajira, ulinzi na usalama na kupambana na rushwa.
Ahadi hizi ni nzuri na zinaingia akilini hasa kipindi hiki ambapo nchi yetu inakabiliwa na umaskini wa kutisha kwa walio wengi. Pia nchi yetu inakumbwa na uhaba mkubwa wa ajira kutokana na serikali inayomaliza muda wake kuahidi kutengeneza ajira isifanye hivyo wala kutoa sababu za msingi za kushindwa kufanya hivyo. Kadhalika, wananchi wetu wengi ni maskini hasa kutokana na serikali inayomaliza muda wake kufumbia macho ufisadi ambao umeligharimu mabilioni ya shilingi huku wahalifu waliotenda jinai hii wakiachiwa waendelee kutanua na kutumia chumo lao la wizi. Pia hali ya usalama nchini ni tete hasa kuzidi kuwa tishio la ujambazi na jinai nyingine kama hizi ukiachia mbali migogoro kwenye nchi jirani na kitisho cha ugaidi. Kadhalika, kuzidi kuzoeleka na kufumbiwa macho kwa vitendo vya rushwa.
Kwa vile CCM ndiyo imekuwa madarakani tangu kupata uhuru, wengi wanajiuliza: Kwanini sasa? Hii maana yake ni kwamba CCM inakiri kuwa kwa kipindi chote ambacho imekuwa madarakani imeshindwa vibaya hasa pale ilipoamua kufumbia macho rushwa au kuiacha itanue kwa kipindi chote ilichokuwa madarakani. Je wapiga kura watafanya kosa jingine kuiamini serikali hiyo hiyo iliyokiri kushidwa? Je CCM ina mipango madhubuti inayotekelezeka na kuingia akilini ya kupambana na majanga haya kweli au ni ahadi za uchaguzi? Yako wapi maisha bora kwa watanzania iliyoahidi miaka kumi iliyopita?
Kuko wapi kufumua na kusukua mikataba ya uwekezaji upya ambayo, kimsingi, iliingiwa kutokana na kuwapo mianya ya rushwa tena kubwa tu.
          Kwa vile ushahidi unaonyesha kuwa CCM ilizembea kwa muda wote iliokuwa madrakani, wapo wanaohoji: Nani anamdanganya nani hapa? Je wapiga kura na wananchi nao wataingia mkenge na kusikiliza porojo hizi zinazolenga kuwatoa kura na baadaye watelekezwe kama ambayo CCM imefanya tangu mwaka 1985? Je watapambana na majanga haya vipi? Hawaelezi zaidi ya kutoa ahadi tamu tamu!
Huwezi kuondoa majanga husika ambayo ahadi za CCM ni kukiri wazi kuwa yapo kwa maneno. Ni vizuri wananchi wakaiuliza CCM ilikuwa wapi muda wote huo na imeona mwanga lini na kwanini kama siyo kusaka kura?
          Laiti kungekuwa na upinzani makini, nadhani hapa ndipo ungeanzia kuisambaratisha na kuimomonyoa CCM vilivyo once and for all kama wasemavyo waingereza. Maana imeshindwa vibaya sana. Ukitaka maelezo na sababu za msingi kwa majanga tajwa kuendelea kuwepo wakati CCM iliahidi kuyaondoa hupati jibu. Hii maana yake ni kwamba CCM wanatoa ahadi juu ya ahadi ili kupata kura wakijua wazi hawatazitimiza. CCM wangekuwa na dhamira ya kutekeleza wanayoahidi, angalau wangekuja na mikakati na sera ya kutekeleza ahadi ambazo waliahidi kwenye chaguzi zilizopita wasizitekeleze. Wengi –kabla ya kuchangamkia ahadi hizi mpya –walipaswa kuhoji ni kwanini ahadi za awali hazikutekelezwa.
          Tumalizie kwa kuwashauri wapiga kura na wananchi kuhoji ukweli, udhati, usayansi na utekelezekaji wa ahadi mpya zinazotolewa na CCM.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 30, 2015.

No comments: