Tuesday, 25 August 2015

Kijiwe chastukia janja ya CcM


          Baada ya msimu mwingine wa kusia uongo na kuingizana mkenge kuanza, tunaanza kusikia mambo ya ajabu ajabu. Ajabu ya maajabu ni kwamba wanaoyasema haya wanawageuza wachovu hamnazo au wasio na kumbukumbu.
          Mgosi Machungi baada ya kurejea kutoka Ushoto kupiga kura ya maoni analianzisha. Akionyesha gazeti la Danganyika Daima anasema, “Jamani mimeona ahadi mpya za CcM na jinsi waivyoenga kutiingiza mkenge mwingine?”
          Kapende anadakia, “Hawana jipya hawa wala hawana dola zaidi ya rongorongo za kusakia kura ya kulia bure tu. Hata hivyo, naona Eddie Luwasa amewashika vibaya kipindi hiki.”
          Mbwamwitu anachomekea, “Hebu fafanua tu-understand. Wameshikwa pabaya wapi na vipi?”
          Mpemba anakatua mic, “Yakhe tuache utani wallahi. Hawa jamaa wa CcM walozoea vya kunyonga vya kujichinja wasiweze kweli wamenasa muhula huu. Hivi mmeona wanivyohaha kuwahadaa wachovu kwa kuja na ahadi tamu mpya wakati zile za awali hawakutekeleza hata moja?”
          Mijjinga anakwanyua mic, “Hawa tulishawazoea. Ukifika wakati wa uchaguzi wanajifanya kujali maslahi ya umma wakati wao ndiyo kikwazo kikubwa cha mstakabali na maendeleo ya umma  husika. Nashauri kupindi hiki tuwapige chini kwa kuwajaribu wapingaji au vipi?”
          Sofia Lion aka Kanungaembe anakamua mic, “Wapingaji wapi wakati wote ni wana CcM? Mnadanganywa na Luwasa kuingia upinzani wakati hana sera zaidi ya za CcM? Ama kweli wajinga ndio waliwao! Nyie hamjui mchezo unavyokwenda siyo!”
          Kapende anakatua mic, “Japo siwapendi wapingaji, angalau wamethubutu kwa kuonyesha ujasiri wa kumchukua Luwasa na kumpitisha agombee urahis. Dawa ya moto ni moto. Kwa vile huyu alikuwa nao kitanda kimoja kwa muda mrefu basi tumtumie huyu huyu kuwamaliza mahabithi hawa.”
          Mheshimiwa Bwege anakatua mic, “Mheshimiwa Kapende nakuunga mkono. Wahenga walisema mchawi mpe mwana alee. Isitoshe, kama upingaji ungemkataa Luwasa ungepata hasara kuliko hatari ya kumtumia kupambana na joka kuu. Nakubaliana na wanaosema adui wa adui yako ni rafiki yako.”
          Kanji naye hajivungi. Anakatua mic, “Lakini pinjani siku mingi iko sema Luwasha iko fisadi papa. Sasa naingia pinjani nageuka malaika?”
          Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu, “Mheshimiwa Kanji usemacho ni kweli. Ila unapokuwa vitani akatokea mwanajeshi au wanajeshi pinzani wakaasi huwezi kuacha kuwachukua lau wakusaidie kupigana kwa kukupa siri za walikotoka ili ushinde kirahisi vita hii. Nadhani haya ndiyo mantiki waliyotumia wapingaji kumpokea na kumpa tiketi Luwasa. Najua wengi hawakubaliani na hili na wanalaumu sana upingaji. Tunapaswa kujua kuwa wakati wa vita haukupi fursa kubwa ya kuchagua zaidi ya kuchukua maamuzi magumu kama walivyofanya upingaji. Wale wanaopinga Luwasa kupokelewa na kuteuliwa walitaka aende wapi kama siyo upingaji?”
          Mzee Maneno anapoka mic, “Msomi hapa nikukubali. Luwasa ni bonge ya silaha dhidi ya CcM. Tunajua ana mapungufu yake.  Lakini ukiangalia hali halisi, mapungufu yake ni rahisi kuyashughulikia kuliko kukosa dola na kuendelea kuliacha kwenye mikono ya manyang’au.”
          Mgosi anarejea, “Hebu tiangaie ahadi za CcM za muongo huu. Wanasema eti watatengeneza ajia. Je ajia hizi ni kwa ajii ya wachovu au vigogo, vigemezi vyao na maafiki zao? Wanaendeea kusema eti watapambana na ufisadi, mbona hawajakama wezi wa Escoo?”
          Kabla ya kuendelea Mijjinga anakatua mic tena, “Hakuna waliponiacha hoi kama kusema eti watapambana na umaskini wakati ndiyo mtaji wao wa kuwatumia wajinga kuwapigia kura ya kula. Ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi. Sijui wachovu wafanywe nini au watukanwe tusi gani ndiyo wachukie na kufanya kweli mwaka huu?”
          Mgosi anachomekea, “Iko wapi ahadi ya kuandika katiba mpya ya wananchi? Upuuzi na uongo mtupu.”
          Msomi anaendelea, “Wasingeweza kuongelea katiba mpya. Kwani wanajua fika wakiigusia, wataumbuka. Wakisema iandikwe ile ya jaji Waryuba ndiyo watakuwa wamekufa kwa vile baada ya kuongopa itawawajibisha. Hivyo, kinachoendelea ni usanii ule ule. Hakuna la maana wala jipya. Heri tuwape wapingaji lau nao tuone vitu vyao chini ya Luwasa au vipi?”
          Sofi haridhiki. Anarejea upya, “Hivi mnaposema Luwasa ndiye apewe kaya mnajua mipango yake ya sirini?”
          Mbwamwitu anakatua mic, “Acha da Sofi nikuchomekee. Unakumbuka wewe ndiye ulikuwa mtetezi wake kabla ya kuwapiga teke? Basi tupe hiyo mipango yake ya siri ambayo umeijua wakati huu au ule lakini ukaificha. Nadhani huu ni unafiki kumuona Luwasa mbaya baada ya kuondoka kwenu wakati wewe mwenyewe ulikosana na watu wengi ukimtetea lakini leo unapiga madongo. Hivi umeingiliwa na nini dada yangu mbona huko nyuma hukuwa hivyo?”
          Mpemba anakatua mic tena, “Nyie hamuwajui hawa sisiemu. Wao mabingwa wa fitina ati. Na ni fitina na ghilba hizi hizi wanizotumia kuendelea kufanya mauza uza yao miaka nenda rudi wasiochelee lolote. Naunga nkono mwaka huu tuwape wapingaji potelea kote.”
          Mipawa anakatua mic, “Nami nakuunga mkono ami. Hizi ajira wanazoahidi kama si hewa basi zitakwenda kwa washikaji na vitegemezi vyao. Kuhusu usalama hiyo sahau. Usalama ni wao kuendelea kuula wakati sisi tukiliwa. Hili la kupambana na ufisadi nadhani wanamaanisha kuupamba zaidi nasi kupoteza njuluku zaidi. Ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi!”
          Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si lakipita shangingi la Nipe Mapepe. Acha tulitoa mkuku!
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 26, 2015.

No comments: