The Chant of Savant

Saturday 18 May 2013

Nini tafsiri ya ndoto hii?



Mwalimu Nkwazi Mhango
Naota nipo mitaa ya Mwitongo kule Butiama alipozaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Najihisi nikipiga ‘ulabu’ na jamaa zangu wa huko kabla ya kuondoka pale na kwenda zetu nyumbani kukamata ‘bukima’ na ‘msuli’ wa nyama au ‘inswi’ (ninaamisha ugali na mchuzi wa nyama au samaki).
Nikiwa narejea zangu home kutoka ulabuni, ghafla ‘ulabu’ wote unanitoka. Badala ya kuendelea kujiimbia wangu wa ‘ekerombeta n’ekerongo’ pombe zote zinaniishia.
Ninahisi mwili kunisisimka kana kwamba nitaona maajabu kama siyo balaa! Kujipa moyo na ithibati naamua kubadili wimbo. Najiimbia wimbo wa nyansuguta. Hili nalo halinisaidii.
Kwani mwili unazidi kunisisimka ikiwa ni dalili kuwa kuna jambo litatokea. Miili ya walevi kwa machale usipime. Na huu ni ukweli ambao naweza kuapia.
Maana bila ya kuwa na miili yenye ‘machele’ walevi wengi wangeishia ‘lupango’ kama siyo kufilisiwa na ‘ndata’ wakiwatoza uchache kwa kunywa pombe haramu.
Huwa nashangaa kuona ‘ndata’ haramu wakiwakamata walevi kwa kujinywea pombe wakidai ni haramu. Mbona hawakamati ‘lisirikali’ haramu linalokula rushwa na kuumiza walevi? Haya tuyaache.
Sitaki kuamsha hasira kiasi cha kwenda vituoni na kutembeza ‘makarate’ na ‘making-fu’ na ‘jet kune doo’ bure.
Ghafla, naona kaburi la tembo likinajisiwa na panya na vicheche aliowakaripia wakati wa uhai wake. Wana maya naye. Kwani aliwazuia kuirarua na kuinajisi ngozi.
Kila kinyama cha mwitu kiko pale kikifanya makufuru kwa kisingizio eti cha kumlilia tembo wakati ukweli ni kwamba vinamsimanga! Huu, kwa hivi vinyama, si msiba bali sherehe.
Vinasherehekea utadhani havitakufa! Hata kama vinaishi ni kimwili, kiroho vilijifia zamani gani! Ni bahati mbaya sana kwangu muota ndoto.
Nahisi hasira ikinipanda kiasi cha kukaribia kupasuka.  Najiuliza ndotoni kwa mshangao na uchungu: Amekosekana mwanaume wa kweli kwenda kuviangamiza vinyama hivi vichafu!
Tembo analia kwa majonzi hajililii, bali anawalilia swala na mbarapi aliowanya wasijirahisi na kuwaruhusu panya na vijinyama vya kiza wawatawale.
Fisi, mbwamwitu, nguchiro na vicheche wameshika kani. Maskini hayawani hawakumsikiliza wala kuelewa ujumbe wa maonyo yake!
Nani atawaokoa wakati huu walipozungukwa na vinyama vya kiza vyenye kila aina ya uroho na ulafi?
Anasikitika na kulia kwa vile hawakumuelewa. Waliingia `mkenge’ mchana kweupe hadi ikala kwao. Namuona mjane mtaua akilia. hajililii wala kumlilia mumewe wala watoto wake bali taifa la mahayawani wasiosikia wala kuhisi.
Hasemi. Ukikutana naye anatabasamu tabasamu la huzuni. Wajinga na wapumbavu huliona kama tabasamu la kweli wasijue ni kilio na unguliko! Tabasamu la mama huyu si la kweli hata kidogo.
Ana kinyongo, usongo, majonzi na ngoa. Atafurahia nini iwapo alimpoteza mume na kile walichotesekea?
Afurahie misiba ya kujitakia wa hayawani wanaoteseka wakimkumbuka mumewe na kumlilia aje kuwaokoa wakati kitabu chake kilishafungwa wasielewe?
Hili nalo linahitaji manabii kuja kuelezea? Mtakwisha msipoamka na kujipigania.
Naona nguruwe akijidai amejipaka uturi wakati anuka kinyesi kitupu. Harufu yake ni machukizo makuu sawa na matendo na tabia yake. Hana aibu wala akili. Kweli nguruwe ni nguruwe.
Ni hayawani mchafu na wa hovyo sina mfano. Anakwenda kwenye kaburi la tembo na kujifanya anamhani na kutoa heshima.
Tembo anakaribia kupasuka kwa hasira. Kwa vile hakuna mawasiliano baina ya wawili hawa, nguruwe anajiridhisha kuwa amempumbaza tembo na kumfurahisha ukiachia mbali kuwadanganya hayawani wenzake waliomzunguka wakimsifia upumbavu.
Nguruwe bila kujua anavyosanifika na wenye akili anahanikiza kujifisifu kuwa ametenda la maana. Ameridhika moyoni kuwa ameua ndege wawili, kumpumbaza tembo hata umma wa hayawani waliomwamini.
Naona machukizo ya kutisha. Ni bahati mbaya wengine wanayaona na kuogopa kusema wala kusimulia ndoto na uoni wao kama mimi. Sitanyamaza.
Nitasema hadi nipasuke kama siyo kutumiwa watu kunimaliza. Waovu na vinyama vya kiza hawapendi kusikia ndoto na mawazo yangu.
Kwani yanawaumbua na kuwaacha uchi. Wanaelewa vizuri ninachosema. Nyoyo zao zinawasonga. Wanatamani wanirarue kama siyo kuniteketeza wasiweze. Hata wakifanikiwa kunimaliza hawatamaliza mawazo na ndoto zangu.
Mie ni muota ndoto na kuota ndoto si kosa kama kunajisi vitakatifu.
Nikiwa natokwa na jasho najifunua na kuzidi kuota. Naona nguruwe mweupe akinajisi kila kitu. Amewaarika nguruwe wenzake kunajisi kila kitu. Anajishaua asijue tupo tunaotamani tumle lau aishie matumboni mwetu kwa hasira na chuki!
Naona nguruwe akitabasamu. Hii ni kawaida yake. Nguruwe ni mnyama asiye na aibu wala adabu. Hana akili wala busara zaidi ya hasara.

Tabasamu na tambo yake hata makufuru vinanifanya nihisi kibuhuti na hasira kiasi cha kutaka kumuua haramu huyu. Nawa moyoni na kujisemea:
Laiti hawa wanaogombea kuchinja wangemchinja huyu hayawani amani ikarejea duniani. Natamani niokote mawe na kumkong’ota huyu hayawani na kuvunja bufulu lake nisiweze.

Wenzake wamemzunguka hasa fisi wenye uchu wa nyama. Nitaanzia wapi wakati najiotea tu? Natamani ndoto hii ingekuwa ukweli lau niwateketeze vinyama hawa.
Naona kundi la bundi na kunguru wakiungana na hayawani wanajisi. Wanalizunguka kaburi la tembo wakiimba nyimbo za sifa ili kuwapumbaza swala wadhani lao moja wasijue ndiyo mwisho wa majaliwa yao. 
Kunguru wanaruka huku na huku wakiokota kila taka na manyoya ya tembo. Wanakenua utadhani watendacho ni sawa!
Nyoka wanafiki nao hawajivungi. Wanakuja na filimbi zao wakiimba nyimbo za sifa kwa nguruwe mpenda sifa.
Ametuna akitabasamu na kufaidi muziki wa kinafiki na kipumbavu. Laiti nguruwe huyu na wenzake wangejua kuwa kuna siku watalipa tena kwa bei mbaya huu uovu na makufuru wanayotenda, wala asingekenua na kufurahia kiama chake.
Nani amstue astuke hayawani huyu aso aibu na kidhabu?
Nikiwa naendelea kujiotea si wale nyoka waliacha kupiga filimbi wakajongelea kwangu! Ghafla niliamka na huku nikitweta kwa jasho ngoa na hasira!
Tuache utani. Tusipoamka kupambana, tutaishia kunajisiwa hai mithili ya tembo yule wa ndotoni.
Ni ndoto tu!

Chanzo: Nipashe Jumamomsi Mei 18, 2013.

3 comments:

Anonymous said...

Ustaadh umeua. Yaani unamlinganisha jamaa na nguruwe au nimekupata vibaya. Je huyo tembo ni nani kama siyo Mwalimu? Una mambo wewe. Kazi yako ya fasihi ni pevu kweli kweli. Sijui kama walengwa wanaipata. Wakiipata jiandae kung'olewa meno na kunyofolewa kucha mwanangu. Good job.

Jaribu said...

Sijui kama wanaipata. Madakta njaa hawa wanahitaji hadithi zilizojaa picha na michoro isiyoumiza akili, lakini tusikate tamaa.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anonymous hapo juu sijaua bali huo ndiyo ukweli niijuao ingawa ukweli una sura nyingi. Hata hivyo ukweli una sura moja yaani UKWELI NI UKWELI. Na kipimo chake ni rahisi kukipata. Ama Jaribu nimefurahi kuona kuwa uko as optimistic as I always am. Hawasemi lakini joto ya jiwe wanaipata. Ni kweli kuwa hakuna haja ya kukata tamaa maana hiyo si suluhisho la matatizo yetu. Nawatakieni kila la heri ndugu zanguni. Karibu tena na tena hata pale nitakapochelewa kuchungulia na kujibu.