The Chant of Savant

Tuesday 28 May 2013

Uombaomba wetu ni wa kujitakia


TAARIFA na ripoti za kufichuliwa wizi wa mabilioni ya shilingi unaotokea kila mwaka zinasikitisha sana.
Hivi karibuni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifichua kuwa makampuni ya uchimbaji madini kwa mwaka wa fedha uliopita yalikwepa kulipa kodi kiasi cha dola za Marekani bilioni moja.
Hii ni pesa nyingi hasa kwa taifa maskini na ombaomba kama Tanzania. Hizi dola bilioni moja ni makampuni ya madini tu. Je, hayo makampuni ya simu, wahamiaji haramu wanaofanya kila aina ya biashara halali na haramu, mabenki, waagizaji na wauzaji bidhaa nje, makampuni ya utalii, maduka ya kubadili fedha za kigeni, wafanya magendo na wengine wanatuibia mabilioni mangapi?
Inatia kinyaa kuona mamlaka zinazembea kukusanya kodi na badala yake zinaendekeza kukopakopa na kuombaomba bila sababu ya msingi.
Ukiangalia mianya ya misamaha ya kodi na ukwepaji kodi nchini, unagundua kuwa taifa letu ni tajiri sana. Laiti ungepatikana uongozi unaoweza kukusanya kodi hata kwa kiwango cha robo, taifa letu linaweza kujitosheleza kwa bajeti yake na kuwa na kiasi cha kuweka benki.
Ni aibu na ajabu kuona kuwa pesa tunayodhalilishwa kwayo kwa njia ya kuombaomba na kukopa ni tone katika bahari ikilinganishwa na ile tunayozembea kukusanya na kufuja.
Hakuna nchi iliyowahi kuendelea kwa njia ya kuzembea kukusanya kodi na badala yake ikawekeza kwenye kuombaomba na kukopa hovyo tena mikopo yenyewe yenye riba kubwa.
Kama kuna jinsi ya kuelezea hivi, ni kwamba tuna umaskini na uombaomba wa kujitakia. Ni kwanini hatuoni hata aibu kuona rais wetu anavyodhalilika kila uchao kwenda nje kuomba wakati pesa inapotea hivi hivi kutokana na watu wachache mafisadi na waroho kuruhusu wengine waibe pesa yetu na kusamehe kodi ukiachia mbali kuachia mianya ya kukwepa kodi? Tunamkomoa nani?
Je, kwanini wakubwa wetu wanafanya hivi? Jibu ni rahisi kuwa wameridhika na mabaki ya ‘ten percent’ wanayopewa kiasi cha kushindwa kuelewa kuwa wangeamua kukusanya kodi na kusimamia rasilimali zetu vizuri wana uwezo wa kujilipa hata mara tatu ya mabaki wanayohongwa.
Kama siyo hivi ni nini? Kwanini wanafanya hivyo wakati wana elimu ya kutosha? Lazima kuna sababu tena zaidi ya hiyo tajwa hapo juu. Hata hivyo, tunaweza kufupisha matatizo yote kwenye neno moja tu- UFISADI.
Hivi karibuni Mbunge Zitto Kabwe Kigoma Mashariki (CHADEMA) alikaririwa akishangaa kuhusu hujuma hii tunayotendewa kama taifa.
Alisema kuwa Rwanda ambayo wateja wake wa simu ni wa kampuni moja ya Vodacom, iliweza kukusanya kodi ya dola milioni 14 wakati Tanzania yenye makampuni mengi ya simu ilikusanya kiasi cha dola milioni 1.4. Kabwe alisema: “Sasa serikali ikusanye kodi iache bla bla, TCRA ipewe mamlaka kama TMAA, sasa imetosha.”
Kinachoshangaza ni kwamba Kabwe alipofichua hujuma hii kwa taifa, mamkala husika zilikuja na vitisho kuwa ni kinyume cha sheria kufuatilia shughuli zake.
Je hawa jamaa wa TCRA wanadhani hayo maofisi wanayotumia kuhujumia taifa ni mali ya mama zao?
Inahitajika roho ya mwendawazimu kukubali kuwa taifa lenye kila aina ya rasilimali hasa madini linaweza kuzidiwa na viinchi jirani kama Kenya na Rwanda ambavyo havina rasilimali hata nusu yetu.
Sijui kwanini hatujisuti na kuona aibu tunavyoonekana mataahira waliokalia utajiri mkubwa huku tukiombaomba kuanzia misaada hadi rushwa?
Tumejigeuza majuha na hayawani kama samaki aliyekufa kwa kiu kutokana na kushindwa kutumia maji aishimo!
Tusiwe kama tembo ambaye huwa ana nguvu nyingi ya kuangusha miti lakini akaishi bila hata kibanda huku akishindwa na nyuni ajijengeaye kiota pamoja na udhalili na utepetevu wake.
Ajabu ya maajabu yetu ni pale tunaposhabikia kuwa na serikali kubwa bila sababu.
Kila awamu ukiachia mbili za mwanzo inasifika kwa kuanzisha wilaya na mikoa mipya ili kukidhi haja binafsi za baadhi ya wanasiasa wakubwa au marafiki zao. Pigo ni pale tunaposhabikia hata kununua migari ya bei mbaya karibu kwa kila mkubwa hata wa ngazi ya chini.
Kama wendawazimu unaoendelea hautakomeshwa, tutaendelea kuonekana kama jamii ya mazuzu na wehu.
Tutashindwaje kuonekana mataahira iwapo tunao ubingwa wa kurudia makosa na madudu mengi hivi?
Ni ajabu kuwa hata watawala wetu hawalioni hili. Kwanini, kwa mfano, kuendelea kushuhudia rais wetu akiombaomba kana kwamba nchi yetu haikujaliwa raslimali na akili?
Sijui kama rais anajisikia vizuri kwenda kuwapigia magoti marais wenzake kuomba hata pesa ya bajeti. Tumsaidie rais wetu aachane na udhalili huu.
Ni bahati mbaya kuwa mfumo wetu umekuwa wa kihasara hasara. Hebu angalia kwa mfano tulivyo na serikali kubwa bila hata sababu ya kufanya hivyo.
Ni bahati mbaya kuwa tangu kuondoka mzee Mwinyi karibu kila rais aliyeingia baadaye alianzisha au ameanzisha wilaya na mikoa bila sababu za msingi zaidi ya masilahi binafsi ya baadhi ya wanasiasa.
Mkapa alianzisha Mkoa wa Manyara nyumbani kwa waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye huku Kikwete akianzisha Katavi nyumbani kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Geita, Njombe na Simiu. Tunaongeza mikoa kwa utajiri gani?
Hebu kwa mfano angalia majirani zetu wa Kenya. Serikali mpya pamoja na kuruhusiwa kuunda baraza la mawaziri wasiozidi 22, kwa kuzingatia mzigo kwa uchumi, iliunda wizara 18. Sie tunao 50 na ushei! Hii ni akili au matope?
Kwa ufupi ni kwamba kinachoisumbua nchi yetu si ukosefu wa rasilimali kuanzia watu hadi madini na vitu vingine bali ombwe la utawala.
Utawala wa namna hii hauwezi kuivusha nchi yetu zaidi ya kuizamisha kama inavyoanza kujidhihirisha ambapo rasilimali zetu zimegeuka laana badala ya Baraka.
Kuna haja ya watawala wetu kujua kuwa kila jambo lina wakati wake. Wajifunze kutoka kwenye tawala zilizowahi kuamini kuwa haziwezi kuguswa na walalaho. Mfano wa karibu ni anguko la aibu na ajabu la Muamar Gaddafi kule Libya hivi karibuni.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 28, 2013.

2 comments:

Jaribu said...

Nafikiri na hawa wakuu wetu wana hisa na hizi kampuni za utapeli. Badala ya kuimarishi simu za nyumbani wao wameng'ang'ania tu simu za mkononi. Maendeleo ya mawasiliano hayapimwi na wingi wa simu za mkononi.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kumbuka Kikwete alisema kuwa hata msongamano wa magari na wapangaji majumbani ni ushahidi kuwa mambo mswano au vipi? Nasikia alisoma uchumi sijui uchumi gani? Ni bahati yake kuwa anatawala kondoo vinginevyo kauli kama hizi zingeishia kum-Gaddafi kama siyo ku-Mbarak