The Chant of Savant

Wednesday 15 January 2014

Utabiri wa mwaka 2014


 
 
Ufuatao ni utabiri wa Shehe, Maalim, Nguli, Ustaadh, Alhaj, Dk, Profesa Mpayukaji Msemahovyo njukuu wa Msemakweli wa Waambie Waelewe katika kile ambacho wataalam wa nyota huita al khabar mutawatir.
Kwa taaluma yangu ya ilm al mubashir al nujm al maarif na shams ul maarif al kubra na ilm huroof. Mimi ni nguli katika sayansi iitwayo An-Najm uth-Thaqib na madude mengine mengi yenye majina magumu.
Kwanza, naomba msamaha kwa kuchelewesha utabiri huu tofauti na mazoea. Kwani huu utabiri ulipaswa kutoka tarehe moja Januari ila kutokana na udhuru haikuwa hivyo. Unaposoma utabiri huu ujue unasoma kitu ambacho kiliandikwa mwaka jana kwa ajili ya mwaka huu.
Natabiri kuwa kutakuwapo ongezeko la wizi wa mali ya umma a mbao utafutatiwa na ngurumo toka Karatu na kwingineko. Zile ngurumo zilizokuwa zikisikika toka Kigoma, Arusha na Iramba zilikuwa ni danganya toto. Ili kuepukana na mvua ya ufisadi na wizi wa mali na fedha ya umma lazima ngurumo zisikike toka nchi nzima.
Natabiri pia kuwa kutakuwa na ongezeko la ujangili na utoroshaji wa nyara na fedha za umma ughaibuni. Nyota zinaonyesha kuwa mali hizi zitapelekwa India, China na Mashariki ya Kati. Natabiri kuwa majangili wengi watakaoshiriki kuua na kusafirisha nyara hizi watakuwa wageni wakishirikiana na wenyeji wakiwamo hata ndata na baadhi ya maafisa wa serikali.
Kutakuwa na mafuriko kuanzia ya mvua hadi bidhaa na dawa feki. Mafuriko haya licha ya kuathiri wengi yataua wengi kama hatua za kuyadhibiti zisipochukuliwa haraka.
Natabiri kuwa atakufa kiongozi king’ang’anizi wa muda mrefu upande wa kusini.
Natabiri kuwa kuna ndoa moja ya mkeka ya kisiasa upande wa pili na ule mwingine iliyodumu kwa muda sasa itavunjika kutokana nammoja wa wanandoa kuona muda umemuacha na nyota yake inazidi kuchafuka kiasi cha kuhitaji kusafishwa.
Natabiri kuwa wanasiasa wataendelea kuumbuka huku wale waliojiona wanaweza kutumia ujana wakiangushwa na wazee. Wale wenye majina yanayoanza na Z, K, P na M wakae mkao wa kuadhirika. Hata chama dume kitakuwa na wakati mugumu wa kumeguka na kuchakaa kiasi cha kunyang’anywa tonge kama uchaguzi ufuatao hautahusisha uchakachuaji. Vyama vyenye majina yanayoishia na M, F, I viko hatarini. Vyama vyenye majina yanayoishia na A vina nafasi kubwa ya kufanya maajabu.
Natabiri kuwa kutakuwa na mgawanyiko mkubwa kwenye vyama vyenye kuishia na F na M kutokana na ima kuchokwa kwa viongozi wake au kuparaganyika kwao.
Pia natabiri kuwa kutakuwa na kashfa nyingi zinazowahusu wake na watoto wa watawala zitafumka kiasi cha kutishia mstakabali wa tawala za wazazi au waume zao.
Natabiri kuwa mwanasiasa mmoja mkubwa mwenye cheo kikuu ataanguka na afya yake itazidi kuwa mbaya kiasi ambacho si rahisi kujua nini kitakachofuatia kati ya kifo na uzima.
Natabiri kuwa waziri wa masuala ya njululu atakufa baada ya kuugua muda mfupi tena akiwa ugenini akitibiwa.
Natabiri kuwa kutakuwapo ongezeko la madudu kiutawala likiandamana na kutupwa watoto wengi mitaani.
Natabiri kuwa watazuka wagombea wengi wa urais ima wenye utata na kashfa au wenye kutumia majina ya baba zao. Wengi watakuwa na majina yanayoanza na herufi J, E, H na A. Hata hivyo, umma utawakataa na kuwazodoa kwa vile hawana sifa yoyote zaidi ya majina ya wazazi wao na tamaa ya kutaka kuufanya utawala kuwa wa kifalme wa kurithishana.
Natabiri kuwa gharama za maisha zitapanda kiasi cha watawaliwa kuwachukia watawala huku vitendo vya kujichukulia sheria mkononi vikiongezeka. Mawaziri wengi watazomewa kila watakapoenda kufanya ubabaishaji kuanzia Mbeya kwa warusha mawe. Natabiri kuwa kukutakuwa na ulannguzi mkubwa wa nishati kutokana na kuwapo kwa mikataba ya kijambazi.
Natabiri kuwa wenye nyumba wengi waliojaa mijini kwenye vibanda vyao watakimbilia mashambani na kuwaachia wapangaji au kuuza kabisa. Kwa jiji la Dar es Salaam natabiri wenye vibanda wataviuza na kwenda kujibanza Uzaramoni mashambani kutokana na ukali wa maisha.
Natabiri kuwa kutakuwa na ongezeko la wasanii hasa wale wa kisiasa ambao mustakabali wao utakuwa mahakamani lakini si kwenye vyama vyao.
Natabiri kuwa kutakuwa na ongezeko la ndata kujihusisha na uvunjaji sheria kama vile utekaji magari, ujambazi hata ujangili ukiachia mbali Jeiwii kuwaonea wachovu kwa kuwapiga wakigombea mambo ya kipuuzi kama mabibi na kadhalika.
 
Nataibiri kuwa kutakuwa na mapigano kwenye nchi moja changa ambayo yatasababisha vifo vingi na ukatili mkubwa upande wa kaskazini.
Natabiri kuwa vyama tawala vingi vitapoteza madaraka au kuwa na serikali zinazohusisha wapinzani.
Natabiri kuwa kiongozi mmoja wa juu atatumia pesa nyingi kwenye safari zisizo na umuhimu kwa walipa kodi. Nyota yake inaonyesha kuanza kufifia kiasi cha kuhisi kuwa anapaswa kuanza kutafuta mahali pa kuwekeza iwapo lolote litatokea.
Natabiri kuwa mwaka huu utashuhudia kuzidi kuzama kwa ilm kwenye ngazi zote kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu. Rushwa ya ngono na shahada za kughushi vitaongezeka huku ajira za kujuana zikizidi kuongezeka pia.
Natabiri kuwa wasani hasa wanamuziki na wachungaji wengi wanaotumia joho la sanaa na neno la Mungu watajikuta kwenye kashfa za kusafirisha mihadarati.
Natabiri mgosi Machungi atahamia Ushoto huku Mpemba akizamia Dar es salaam ili aongeze vitegemezi. Natabiri kuwa Kanji atakwenda India na kukuta surprise ya mwaka ambapo bi mkubwa wake atakuwa amemuongezea vitegemezi vitatu toka mtaani huku bi Sofi ataongeze mkorogo mpaka aungue na kuumbuka. Natabiri Msomi Mkatatamaa atatangaza nia ya kugombea urais mwaka 2015 kwa chama chake kiitwacho People’s Help and Development (PhD).
Natabiri kuwa wale wanaojigamba kuiweka polisi mifukoni mwao, mifuko yao itapasuliwa na nguvu ya umma. Mipawa na Kapende watatabiriwa baadaye.
Mnakaribishwa ofisini kwangu na utabiri ni bure isipokuwa ukitabiriwa kifo unaacha hati ya nyumba, gari hata talaka ya bi mkubwa.
Ofisi ziko Manzese mitaa ya kati nyumba namba 666.
Chanzo: Tanzania Daima Jan., 15, 2013.

4 comments:

Jaribu said...

Umenivunja mbavu na huo utabiri wa Sofi na mkorogo. Nilikuwa nafikiri huyo Sofi ni hadithi lakini sasa nimeipata.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Jaribu,
Sofi yupo kwa sana na ni mama mwenye maulaji yake yatokanayo na kujua kuwahudumia wakware nao wakampa ulaji. Her real name is Sofia Lion kama ukiitafsiri kwa kimakonde.

Jaribu said...

Wakwere na Wazaramo ndugu moja, na siku hizi wameanzisha ujinga wa ukanda. Imekuwa nongwa siku hizi, "Sisi watu wa pwani hivi, sisi wa watu wa pwani vile!"

Tukirudi kwenye mkorogo, nisingekuwa na mambo mazito zaidi ya taifa, ningeaanzisha kampeni ya kupiga vitu mikorogo. Huku utajua mama wa Kiafrika kutokana na uso wake uliochubuliwa.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ukitaka kuchukiwa piga kampeni dhidi ya nkorogo sorry mkorogo. Utaanzia wapi? Kama utawalenga akina mama wanaopaka utanoa. Ukiwalenga wanaume wanaowamotisha akina mama kupata mkorogo utanoa maana hawaupaki.
Kaka usiniponze. Nimesema anawahudumia wakware si wakwere hata kama nao anawahudumia. Hii falsafa ya upwani ni ujinga wa kawaida maana ukiangalia wanaojiita wapwani wanaishi bara na si pwani. Wengi hata kuogelea hawajui lakini wanajiita watu wa pwani. Hivi kweli Chalinze ni pwani? Na Lushoto je? Sitashangaa siku moja kusikia watu wa Morogoro wakasema nao ni watu wa pwani kwa vile ni kabila moja na wakwere.