Wednesday, 31 December 2014

Bado serikali ya Kikwete si ya Ubia?

Japo rais Jakaya Kikwete huwa haishiwi vituko au mazingaombwe au sanaa kama watani zake wapendavyo kusema, juzi aliwaacha wengi hoi. Alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Kimsingi fedha hizi ni za IPTL, katika swali pesa za nani, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipoulizwa na Kamati ya Bunge alisema humu yawezekana zipo za umma pia zipo za IPTL.” Kama fedha kweli ni za IPTL na si mizengwe na upotoshaji, ilikuwaje Kikwete huyu huyu akamfukuza kazi Anna Tibaijuka waziri wa zamani wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi? Je ilikuwaje Kikwete huyu huyu akakubali kujiuzulu kwa mwanasheria wa serikali wa zamani Jaji Fredrick Werema? Je Kamati ya Bunge iliyofichua kashfa nzima na kugundua kuwa fedha ya umma ni uongo au uvumi kama alivyowahi kusema Tibaijuka wakati akijitetea asijue ataenda na maji? Je inakuwaje Kikwete aone fedha za IPTL asione za umma alizosema CAG kuwa zilikuwa kwenye escrow? Je ameishakatiwa chake?
Je anachosema Kikwete ndiyo msimamo wake na serikali yake au atabadilisha lugha kama alivyokaririwa akisema wakati akimwajibisha Tibaijuka aliposema, “Tumezungumza na Profesa Tibaijuka na tumemuomba atupishe ili tuweze kuteua waziri mwingine kwani viashiri vyote vinaonyesha kuwa alikiuka kanuni na sheria ya maadili ya Umma.” Je haya maadili ya umma anayosema Kikwete ni yapi wakati mgao wa fedha aliyopewa Tibaijuka ni fedha ya IPTL?  Rais anatuma ujumbe gani kati ya anachosema kuhalalisha fedha ya umma kuwa ya IPTL anayodaiwa kuisaidia kuingia nchini akiwa waziri wa Nishati na Madini na kile kinachosemwa na Bunge kuwa fedha ni ya umma?
Kimsingi, kama Kikwete hatakanusha madai yake, ni dhahiri, kuna mgongano baina ya mihimili mitatu ya dola jambo ambalo ni hatari sana. Je Kikwete ameshindwa kutangaza mgogoro huu hadi akaamua kutumia lugha ya mafumbo? Je ni wangapi wanauona huu mgogoro ambao unaweza kulizamisha taifa kama siyo kuliingiza kwenye machafuko pale ukweli utakapojulikana? Je Kikwete amejipa usemaji wa IPTL au ni kutimia madai ya CHADEMA kuwa alikuwa akipokea amri toka kwa James Regamalira juu ya jinsi ya kushughulikia kashfa ya escrow bila kuumiza maslahi yao? Je Kikwete ni mwenye shea kwenye IPTL au IPTL ina shea kwenye serikali yake? Kuna mantiki katika kuhoji. Kwanini serikali ya Kikwete ilikaa kimya sana wakati umma ukihanikiza watuhumiwa wa escrow washughulikiwe? Kama hakuna ubia ilikuwaje Kikwete akadharau hata mapendekezo ya Bunge kwa kuwawaweka kiporo kingpin au wawezeshaji wakuu wa wizi mzima?
Wengi wanahoji mantiki ya rais kuhalalisha wizi wa fedha za umma. Kama fedha ni za IPTL, je ushahidi wote uliotolewa na kamati ya Bunge ni uongo mtupu?  Inahitaji nguvu ya ziada kuwashawishi watanzania kuwa fedha ni ya IPTL. Fedha ni ya Watanzania. Kikwete anasema hakuna hasara. Hasara ipo tena kubwa.
Kwa waliofuatia sakata zima la escrow watakubaliana nasi kuwa watu kama waziri mkuu Mizengo Pinda, Saada Mkuya, Profesa Benno Ndullu na wengine waliotajwa wana ubia kwenye serikali. Maana hawakuwa na sababu ya msingi kubaki maofisini wakifanya madudu yale yale. Hivi mantiki ya kuendelea kulumbana juu ya uhalali wa mmilki wa fedha ya escrow ni yapi wakati tumeishaanza kuwachukulia hatua baadhi ya wadau wa kashfa husika? Je nini mantiki ya kuwaacha watuhumiwa wakuu yaani James Rugemalira na Harbinder Sethi Singh kuendelea kuchezea mahakama zetu kama si kuwa na ubia kwenye serikali husika? Hivi hili nalo linahitaji PhD in Political Science?
 Marehemu baba wa taifa aliwahi kulalamikia CCM kutekwa na mafisadi asijue watateka kila kitu. Baada ya kuiteka CCM wameteka na serikali yake kiasi cha kuwa mtumishi wao aliyewasaliti wananchi. Haiwezekani kila mwaka utokee ufisadi wa kutisha serikali isiushughulikie iwe haijatekwa na kufungiwa kwenye mifuko ya mafisadi wanaowakatia viongozi wetu zawadi za kipuuzi kama vijisenti vya ugolo, suti, saa na upuuzi mwingine. Serikali ya Kikwete haiwezi kujidai kuwa si ya ubia. Uliza, wauza unga majambazi na wahalifu wengine wamefanywa nini na kwanini? Kuna watu wanajulikana. Utajiri wao ima umetokana na kuuza unga au ujambazi na jinai nyingine. Nani anawawagusa zaidi ya kuwa wafadhili wakubwa wa CCM? Mfadhili mmojawapo wa CCM anayetafutwa na vyombo vya kimataifa ni Alex Massawe ambaye kama si vyombo vya kimataifa kuingilia kati angekuwa huru akiendelea na ujambazi kama kawaida.
Kuonyesha IPTL ilivyo mbia wa serikali ya Kikwete, vyombo vya habari vimeripoti matukio ambapo mtuhumiwa anayejifanya kuimilki IPTL inayosemakana kupatikana kinyume cha sheria Harbinder anaonekana akimwaga fedha kwa jeshi la polisi linalopaswa kuchunguza uchafu wake. Je jeshi kama hili linalofadhiliwa na fisadi kama huyu linaweza kumchukulia hatua? Kibaya zaidi, unapoona wakubwa wa polisi wakipokea msaada wa fedha toka kwa fisadi kama huyu usidhani mambo yanaishia hapo. Nao lazima wakati chao binafsi.
Kwa tabia na mazingira tajwa hapo juu, ufisadi na utawala vinafunga ndoa na kutenda na kuishi pamoja kama ilivyo sasa ambapo rais anapata kigugumizi kuwatimua hata mawaziri wachache waliotolewa kafara kunusuru serikali yake. Hata ukiangalia sakata zima lilivyoshughulikiwa kwa papara na Bunge unagundua aina nyingine ya ubia kwenye vyombo vingine vya dola.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 31, 2014.

No comments: