Friday, 12 December 2014

Mlevi asherehekea maadhimisho ya miaka 53 ya uhuru kwa vilio na kumbukizi

Najua wengi walisherehekea zaidi ya nusu karne ya udhuru, sorry, uhuru. Kwa mlevi haikuwa sherehe kitu bali kumwaga michozi na kuungulia utadhani mamisap wake amerejesha namba. Baada ya kupiga mibangi na ulabu nikidhani angalau ningepoteza mawazo, nilijikuta michozi ikinimwaika kama mtoto mchanga tena yatima. Je mimi si yatima usawa huu ambapo uhuru kwangu umegeuka udhuru? 
Katika kutokuwa mchoyo na mbinafsi, niliamua kuwakumbuka mashujaa na wahanga wa huu unaiotiwa uhuru. Je mimi ni huru, wewe ni huru, na wao ni huru?   Waliogeuza uhuru kuwa udhuru, kwa kuhalalisha ufisadi, ujambazi na udokozi nao ni huru? Thubutu! Walioua Ujamaa na Kujitegemea na kuanzisha Uhujumaa na Kujimegea wanahitaji kukombolewa lau nao wawe huru kama wale walio huru.  
Tunazidiwa na hata kunguru toka India wanafaidi katika kaya isiyo huru! Hivi kweli unaweza kuwa huru na ukaishi kwa kubomu, kukopa kopa na kufisidi? Jibu unalo wewe unayesoma unabii huu wa Mlevi asiyekubali kunyamazishwa iwe ni kwa mtutu au mamlaka. 
Nina maswali mengi ambayo hayana majibu.Sijui kama walevi na wavuta bangi wanaosulubiwa na umaskini, ufisadi, ujambazi, ukosefu wa usalama, huduma za afya na makandokando mengine ni huru. Hivi wale wanaodhulumiwa karibu kila kitu au kutozwa rushwa ili wapate huduma ni huru? Je wale wanaorundika kwenye vyumba vya kuongeza ujinga viitwavyo madarasa wakikaa chini kama kuku nao ni huru? 
Katika kujitahidi kuwa on the same page na wadanganyika na wengine katika kaya ya Tanzia, nilijikuta nikiwakumbuka hata wanyama. Niliwakumbuka wale twiga, digidigi, nguchiro na ndege waliovushwa kwenda Qatar hapo Novemba 20, 2010. Kwa namna ya pekee nilikuwakumbuka wahanga wa mauaji ya ndata hasa yale ya Arusha ya tarehe 5 Januari 2011. 
Sikuachia hapo. Kwa uchungu, niliikumbuka Loliondo iliyouzwa wakati wa utawala wa ruksa ya kufanya kila jinai.  Kwa namna ya pekee, nilimkumbuka mpiganaji mwenzetu, Stan Katabaro, aliyetolewa kafara kuficha uchafu huu. Nani anamkumbuka leo? Nani anampa nishani ya ushujaa wakati nishani zenyewe hazipo na kama zipo wanapewa wasaliti? Niliwalilia wakulima wanaolanguliwa mazao yao huku wakikamuliwa kodi za kuendesha maisha aghali ya watesi wao. 
Niliwakumbuka wahanga wa madawa ya kulevya wanaoendelea kuzalishwa, kuhujumiwa na kudhalilishwa na mfumo mbovu mitaani huku wakiendelea kuteketea.  Nani anapambana na wazungu wa unga zaidi ya kutoa ahadi hewa na majigambo kuwa wanajulikana lakini wasikamatwe lau kama danganya toto? 
Kwangu maadhimisho ya uhuru ilikuwa ni siku ya tafakuri nzito sana. Niliwakumbuka wote wanaosulubiwa na   umaskini huku wakishuhudia ujambazi kama EPA, Richmonduli, escrow, meremeta, kagoda na mwingine mwingi vikihalalishwa. Niliwakumbuka walevi wangu wanaolipa kodi wakaambulia kusomea taarifa za ukwapuzi wa mabilioni.  
Hakika, niliwakumbuka wote wanaohangaishwa na kuisaka elimu wasiipate huku wenye mamlaka wakibariki kila jina ya kughushi vyeti vya kitaaluma. Niliwakumbuka wagonjwa, hasa akina mama, wanaorundikwa kitanda kimoja kama migebuka ya kule Kigoma.  
Mama anakwenda kujifungua mjenzi wa kesho wa kaya anaishia kuaibishwa, kuteswa hata kuombwa chochote kitu! Kwani haya hayafanyiki hadi baadhi ya dada na mama zetu kujifungulia nje ya hospitali? Wakati haya makufuru yakiendelea wanakuja matapeli na kukuahidi maisha bora tena kwa wote usijue ni maisha bora kwao na watu wao hata waramba makalio yao. Nani anahoji kwa uchungu na uwazi kama mimi?  
Hakika naona uhuru katika kuvuta bangi na kulewa. Kwani huniwezesha kuzoza na kupayuka bila kuchelea lolote. Nitahofia nini wakati nilishajifia? Pia niliwakumbuka ndugu na jamaa zangu wanaoendelea kusota pale Ocean Road kwenye hospitali ya saratani huku wenzao wenye nazo na maulaji wakienda kuchunguza afya zao na kutibiwa ughaibuni kwa fedha ya hao hao wahanga. 
Hakika, kwa mlevi, siku hii ilikuwa shule tosha. Nilidurusu historia ya uhuru. Nilimkumbuka mzee Mchonga na wale wote walioteseke, kupigania hadi kufia uhuru uliogeuka udhuru. 
Niliikumbuka Benki ya NBC iliyouzwa kwa makaburu bila kuisahau mahututi Tanesco na machimbo ya makaa ya mawe ya Kiwira yaliyotwaliwa na kuendelea kuangamiza fedha za walevi. 
Siku ya kulia sana. Nilivaa magunia na kujipaka majivu nikiazimisha anguko hili. Nilipowaona ndata wakipiga kwata kuadhimisha siku hii, moyo ulinyatuka nikajikuta nawaombea na kuwakumbuka wahanga wote waliouawa na mibunduki ya ndata. Nilikuwakumbuka hata vibaka wanaochomwa moto huku mibaka ikiendelea kuabudiwa na kukingiwa kifua na wenye vifua. 
Kwangu siku hii ilikuwa na ya sononeko, ngoa na uchungu kiasi cha kulia hadi bi mkubwa akatishia kunivisha gagulo au kunibonda kwa mwiko akidhani namchulia. Uzuri ni kwamba nilipompa sababu za kilio changu alinielewa na kuungana nami katika kumwaga michozi. 
Si utani, hadi leo naendelea kulia. Nimefunga wiki nzima lau kuwapa heshima wahanga wa udhuru.  Nafunga kuomba aje mkombozi awakomboe walevi wangu. Aje asafishe hii ardhi iliyolaaniwa ambapo matabaka ya wenye nazo, tena wanaozipora kwa walevi na wasio nacho wanaoibiwa hata jasho na damu yao, yamejengeka na hakuna anayejali. 
Ninalia sana hasa nikikumbuka katiba mpya ambayo ingewakomboa walevi ilivyonyongwa huku shujaa Jose Waliobora akidhalilishwa na wahuni wa kulipwa huku tunaodhani ni wakubwa na wenzetu wakimkejeli kwa kuomba yasiwakute waliyomtendea wasijue ya kesho hayajulikani. 
Usidhani naongea kwa nguvu ya bangi. Hapana, nami nina ubongo tena unaochemka kuliko wale wenye mtindio wa ubongo wanaogeuza kaya hii shamba la bibi kwa akina Harbinder na Rugemalayer kuiba na kuwahonga njuluku ile ile waliyoruhusu iibwe kwa upogo na upofu wao. 
Uchungu umezidi. Siwezi kuendelea zaidi ya kujaza ndoo ya michozi. Uwiiiiii, mai wee, wooooi. Udhuru unaniliza kiasi cha kutamani uhuru!
CHANZO: NIPASHE 

No comments: