Monday, 22 December 2014

Anna Tibaijuka unangoja nini?

Anna Tibaijuka akisakata ngoma ya kihaya na James Rugemalira baada ya kumkatia shilingi bilioni moja na nuka sita (A day Tibaijuka danced with the devil)
Anna Tibaijuka akimsomesha Rugemalayer ili akate pochi
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, profesa Anna Tibaijuka yumo msambweni akikabiliana kashfa ya kumegewa mgao wa fedha zilizoibwa kwenye mfuko wa Escrow. Taarifa za vyombo vya habari ni kwamba Tibaijuka aligawiwa kiasi cha shilingi bilioni moja nukta sita. Hii si fedha ya ugoro wala vijisenti. Ni fedha nyingi hasa kwenye nchi maskini na ombaomba.
           Japo Tibaijuka haoni ubaya wa kumwagiwa utajiri wa ghafla bin vu, wengi wanaohoji amelipwa kwa kazi ipi kama mtumishi wa umma? Japo Tibaijuka haoni kosa kiasi cha kuitisha mkutano wa waandishi wa habari na kujitoa kimasomaso akisema kuwa hawezi kujiuzulu pamoja na Kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali (PAC) kupendekeza awajibike, wengi wanahoji anakopata hii jeuri ya kusema kuwa hatajiuzulu. Je Tibaijuka ameamua kwa makusudi mazima kuidharau Kamati ya Bunge huku akimtwisha rais Jakaya Kikwete mzigo wa kuamua hatima yake? Je hii ni heshima kwa Bunge na kwa rais na watanzania kwa ujumla.         
          Tibaijuka ni mmoja wa watumishi wa umma aliyekuwa ametukuka kabla ya kuingia kwenye tope hili la ufisadi na kusaka utajiri wa haraka. Ni mama aliyejizolea sifa kemkem kiasi cha kutajwa kwenye watanzania wachache wenye kuweza kuteuliwa kugombea urais. Sifa za Tibaijuka zinavuka mipaka ya Tanzania. Aliwahi kuwa mkurugenzi wa shirika la makazi la Umoja wa Mataifa kabla ya kurejea nyumbani na kugombea ubunge na kushinda. Kwa msomi wa kada hii, kufanya madudu aliyofanya ni jambo la kusikitisha na kukatisha tamaa kiasi cha wengi kuhoji ulipo usomi wa mama huyu.         
          Tibaijuka alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Huu uvumi unatakiwa kuachwa, sioni sababu yeyote ya mimi kujiuzuru kwa kuwa sijahusika kwa namna yeyote kwenye sakata hili la Escrow.” Kwanza ni ajabu kwa Tibaijuka kuita taarifa ya Kamati ya Bunge uvumi wakati kuna ushahidi tosha wa kumhusisha na kashfa husika. Anasema hakuhusika na wizi wa fedha ya escrow. Ni ajabu. Anataka uhusike mara ngapi wakati alinufaika na wizi husika au haujui maana ya neno kuhusika? Atake asitake, Tibaijuka anahusika kwenye wizi wa fedha za escrow vinginevyo aishitaki Kamati ya Bunge iliyopendekeza awajibike au kuwajibishwa. Je anachofanya Tibaijuka ni kutapatapa akijua wazi kuwa mwisho wa siku ataachia ngazi? Arejee tambo za wenzake kama alivyowahi kusema aliyekuwa Mwanasheria mkuu wa Serikali jaji Fredrick Werema aliyesema kuwa asingejiuzulu hatimaye akaramba matapishi yake.           
          Ni jambo la hovyo na hatari kwa mtumishi wa umma kung’ang’ania ofisi ya umma hata baada ya kupoteza udhu utadhani ofisi hii ni mali binafsi. Hii ni dharau kwa utumishi wa umma ukiachia mbali kuuibia umma anaopaswa kuutumikia badala yake akautumia kwa maslahi binafsi. Lazima Tibaijuka ajiondoe haraka ili asafishwe baadaye kama anaona hana hatia wala hakushiriki kwenye wizi wa fedha ya escrow. Ni rahisi hivyo. Achia ngazi ndipo uchunguzi mwingine uombe ufanyike ili ukweli ujulikane. Kusema kuwa taarifa ya Kamati ya Bunge ni uvumi ni matusi ya nguoni kwa wabunge, bunge hata watanzania waliokasimu madaraka yao kwa Kamati husika. Tunamshauri Tibaijuka aige mfano wa mwanamama mwingine nguli barani Afrika aliyekuwa makamu wa rais wa Zimbabwe Cde Joyce Mujuru aliyekubali uwajibishwa aliposingiziwa kuwa alikuwa akifanya mipango ya kumuua na kumwangusha rais king’ang’anizi wa Zimbabwe Robert Mugabe hivi karibuni. Haja ya mja hunena kwa muungwana ni vitendo. Ni ustaarabu na uwajibikaji uliotukuka kwa mtumishi wa umma kukubali kuwajibika badala ya kujiingiza kwenye malumbano na hatimaye akaramba matamshi yake kama Jaji Werema.
           Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Tibaijuka kukumbwa na shinikizo la kumtaka awajibike baada ya kutokidhi matarajio ya wengi akiwa waziri. Rejea kushindwa kubomoa jengo la Mtaa wa India lililoua watu tokana na kujengwa chini ya viwango. Ni Tibaijuka huyu huyu aliyejipiga kifua kuwa angeporomosha lile jengo uaji akaishia kuufyata. Wengi hawajui sababu za kushindwa kuangusha jengo husika. Kadhalika, Tibaijuka, pamoja na kujivuvumua akisema kuwa haoni sababu ya kuwajibika, ameshindwa kujua kuwa fedha aliyopewa ni ya wizi. Je hili nalo linahitaji shahada ya uzamivu? Je alipewa fedha hii chafu kwa kazi gani? Katika kujitetea alidai kuwa James Rugemalira mmojawapo wa watuhumiwa wa ukwapuaji wa mabilioni ya fedha ya umma ni kaka yake. Hili  halina ubishi.  Hata kama ni kaka yake, bado anatuhumiwa kuuibia umma.
          Kitu kingine kinachomfanya Tibaijuka astahili kuwajibika au kuwajibishwa haraka ni ile hali ya kumilki shule binafsi tena ikipokea fedha chafu kwa mabilioni. Je hapa hakuna mgongano wa kimaslahi baina ya kazi yake na biashara zake? Je alipewa kiasi hiki kikubwa cha fedha kutokana na ukaka au cheo chake? Mbona kwenye watuhumiwa wa kumegewa fedha chafu hatuoni dada au kaka wa mtuhumiwa kama hakuna namna? Je Tibaijuka ataendelea kujidanganya hadi lini? Je rais Kikwete atamkingia kifua ili naye aonekane kuwa kwenye dili hili la wizi wa umma au atamwajibisha mara moja kama Kamati ya Bunge ilivyopendekeza? Umma unangoja kuona mwisho wa sakata hili ambalo limelichafua taifa kitaifa na kimataifa. 
      Tumalizie kwa kumtaka na kumsihi Tibaijuka aachie ngazi mapema kabla ya kuchafuka na kufichuliwa zaidi. Maji yameishamwagika hayazoleki na huu ndiyo mwanzo wa mwisho wa zama za Tibaijuka kisiasa. Akubali ukweli na kujiulaumu badala ya kusukumizia Kamati ya Bunge lawama bila sababu. Aeleze amepewa hiyo fedha kwa kazi gani na kwaninini? Simpo. Je Anna Tibaijuka anangoja nini wakati kila kitu kiko wazi?
Chanzo:Dira ya Mtanzania leo

No comments: