Wednesday, 3 December 2014

Kijiwe chataka wachovu waingie mitaani


Baada ya kushuhudia mazingaombwe, ngonjera na mizengwe kuhusiana na kashfa ya escrew ambapo wachovu have been screwed, Kijiwe kimeamua kuhamasisha wachovu kuingia mitaani ili kujikomboa vilivyo once and for all kama anavyolonga Msomi.
Msomi Mkatatamaa anaingia akiwa anaonyesha kuchukia wazi. Bila kungoja, baada ya kutuamkua anasema, “Waheshimiwa, mmesikia huu upuuzi uaoitwa kushughulikia majambazi ya escrow jinsi ambavyo mama microphone Anna mcheza Makidamakida anavyotaka kuwalinda wahalifu mchana kweupe?”
Mijjinga hangoji, anakatua mic, “Unashangaa la huyu mteule wa mafisi na mafisadi kuwalinda mabwana zake? Hakuna waliponiacha hoi kama kushupalia vidagaa wakati papa likiendelea kuputa maji.”
“Unamaanisha niniii yakhe mbona sikuelewi. Hili papa ni nani yakhe?” Anauliza Mpemba huku akijiweka vizuri kwenye benchi.
Msomi anajibu, “Ami hukusikia maneno makali ya Tunduni Jissu aliyesema kuwa Njaa Kaya ndiye kila kitu katika ujambazi huu? Mbona alitaja jina moja kwa moja tena bila kumung’unya kuwa Njaa Kaya ndiye aliyeasisi, kubariki na sasa kutekeleza na kunufaika na jinai hii?”
Kapende anakwanyua mic, “Heri wakubwa watoboe. Maana nilishawahi kutomboa na hakuna aliyejali. Bila kumshughulikia huyu na genge lake ni kama wanatwanga maji kwenye kinu.”
Mipawa hangoji, anatafuna mic, “Mie hakuna waliponiacha hoi kama kugundua kuwa profesa Muongo alitumia magunia na maboksi kusomba dolari milioni 95. Kama msomi kama huyu anafanya upumbavu na utoto kama huu, wasiokwenda shule wafanyeje?”
Mzee Maneno anasema, “Acha nikuchomekee mkuu.” Kabla ya kuendelea Mipawa anadakia, “Mzee Maneno tuheshimiane. Chunga lugha hiyo. Wewe ni wa kunichomekea mimi?”
Mipawa anaomba msamaha na kuendelea, “Loh! Sikujua kuwa utajenga dhana tofauti na niliyomaanisha. Nisemacho ni kwamba kwenda shule au kuwa na PhD hakuondoi upumbavu wa mhusika hasa kama mhusika mwenyewe alikariri vitabu akashindwa kuchanganya na zake kama alivyochanganya mbayuwayu mwenyewe Njaa Kaya kwa kuendelea kuwachezea hawa waishiwa wanaohangaika na vidagaa huku mwenyewe akiendelea kula kuku kwa mrija na wezi wake.”
Mgosi Machungi anaamua kutia timu, “Mimi sichomekei mtu. Tikubaiane kuwa huu wizi ulianza wakati wa awamu ya pii ambapo watu wachafu walipewa dola. Mliposikia ruksa kumbe hamikujua kuwa ilikuwa ni kuwaibia hadi mkome!”
Sofia Lion aka Kunungaembe leo anaamua kutia guu mapema, anakatua mic, “Mimi siamini kama yanayosemwa kuhusiana na mtukufu ni kweli. Nadhani ni wivu tu wa kike tu.”
Mijjinga kaguswa pabaya, anapoka mic, “Sofi acha nikuchomekee sasa liwalo na liwe. Hivi umeingiliwa na nini dada'angu. Yaani pamoja na kila kitu kuwekwa wazi bado unaendelea kujigonga na mapenzi yako ya kibubusa. Huyu jamaa alikufanya nini hadi unamzimikia hivyo? Najua jamaa ni mwingi kweli kweli.”
Msomi anaamua kurejea haraka kuokoa jahazi. Anakwea mic, “Jamani huu mjadala si wa utani. Hebu tuwe serious kidogo achana mambo ya kuchomekeana wakati mlishachomekewa na hawa mafisi. Mnadhani wanaoathirika na huu ujambazi kama si akina Sofi na wengine ni nani? Hakuna ninapojisikia kutaka kupasuka kama kuwasikia wezi wenyewe wakiwahadaa walevi kuwa watashughulikia ujambazi huu wakati wao ndiyo wachezaji wakuu.”
Anapiga chafya na kuendelea, “Mlimsikia waziri mdogo wa ujambazi wa BoT Mwehujuu Michemba akijidai anajali wachovu kwa kusema eti atawabana wezi walipe kodi. Walipe kodi gani wakati fedha yenyewe tushaambiwa ni ya wizi? Rejesheni fedha yetu na kufunga hawa vyangudoa wa kimaadili na madili. Au wanataka kujenga mazingira kama ya Richmonduli ambapo mwizi mkuu aliwaamuru wadogo zake warejeshe njuluku utadhani walikuwa wamekopa. This is unacceptable. How long are we going to shy away from this rip off whereby our people are screwed up under escrow and other scams?”
“Msomi lugha hiyo. Unaongea kikameruni badala ya kwenda kuwakameruni hawa mabwabwa na majizi! Natamani atokee mrume wa kweli awasweke lupango ili wakafanyiwe kitu mbaya huko kama wanavyobaka njuluku na taasisi zetu.”
Kanji naye anaamua kula mic, “Mimi ogopa sana pango. Kama napelekwa basi Swahili yote takagombea gongo ya hindi. Iko tisha kweli kweli. Kama napelekea kuba takula dogo huko.”
“Naomba nivae Ninja na nyekundu niongee mambo mazito na makubwa.  Kama hatotafanya walichofanya wenzetu wa Burkina Faso tutaendelea kuliwa twajiona. Dawa ya mibaka na mijambazi mikubwa kama Muongo, Rugemalayer, Singasinga, Saada Mkuyati , Njaa Kaya ni kuchomwa moto. Mbona tunachoma vibaka huku tukigwaya na kuabudia mibaka? Nina usongo na Endelea Chenge, Anae Kajuamlo Tiba-ijuka na Sossie Muongo. Natamani atokee popobawa awaondolee jeuri wallahi.” Mheshimiwa Bwege anasema huku akijiandaa kuvaa ninja na vazi lake jekundu.
“Dua la kuku halimpati mwewe. Kwanini kutamani yawakute wakati umma unayo nguvu ya kuweza kuwadondosha kama alivyofanyiwa Compaore?” Mbwa Mwitu anachomekea.
“Mie naona yote ni kucheza makidamakida kama Makindamakida mwenyewe. Dawa hapa ni kutowaangalia nyani usoni. Furusha Chama Cha Mafisadi na Mafisi (CCMM) vinginevyo tukubali kuendelea kuliwa tu hata kama neno hili halipendezi.” Anachangia Kapende kwa hasira.
“Mie wote sawa lakini hili la wachunaji wa kondoo wanaojiita watu wa Sir God kama Kilainika na Nzingirwa kupokea njuluku limeniacha hoi.Sijui Baba Mtakatifu kama atamwacha hawa fisi waliojificha kwenye ngozi ya kondoo.” Anachomekea mzee Kidevu.
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la Rugemalayer na Singasinga. Tulilikimbiza na wahusika wakakimbia tukaishia kulichoma moto. Hamkusoma magazetini juu ya tukio hili! Ngojeni zali la kuingia mitaani kama Burkina Faso.
Chanzo: Tanzania Daima leo.

No comments: