Wednesday, 3 December 2014

Escrow imefichua utawala na mfumo vya kijambazi

          Mazingaombwe yanayoendelea ambapo watawala wanataka kujinasua kwenye kashfa itokanayo na ufisi na ufisadi yamefichua uoza wa mfumo, utawala na taasisi zetu. Bila shaka, yamefichua aibu ya taifa letu ambapo kundi la wezi wachache, chini ya kisingizio na ulinzi wa madaraka, linawahujumu raia maskini. Ni bahati mbaya kuwa hatutaondokana na balaa hili hasa ikizingatiwa kuwa tunawalilia wahalifu wale wale watutendee haki wakati hawawezi. Je yawezekana fisi kula mkia wake?
Kwa wanaokumbuka kilichotokea 2008 wakati wa kashfa nyingine ya kijambazi kama hii alipotolewa kafara waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa, watakubaliana nasi kuwa maandalizi ya ujambazi huu yalifanyika hata kabla ya Richmond. Baada ya Spika wa Bunge wa zamani Samuel Sitta kuruhusu kukaangwa kwa Lowassa ambaye, kimsingi, alitolewa kafara kuokoa utawala mzima, wezi wetu waligundua kosa la kutokuwa na mtu wao kwenye taasisi hii.  Hivyo, walichukua hatua za haraka haraka kwa kumwengua Sitta na kupachika kibaraka wao ambaye angewalinda wakati muafaka ukifika. Hapa ndipo yalipo mantiki ya spika wa sasa Anna Makinda aliyeshutumiwa kuwa chaguo la mafisadi kutaka kuua mjadala wa kashfa ya escrow. Amefanya kazi aliyosimikwa kuifanya. Nani anaongelea kutimua serikali nzima iliyothibitisha wazi kuwa nyuma ya ujambazi wa escrow?
Tunasema bila kumung’unya kuwa serikali nzima inahusika na ujambazi huu. Ushahidi rahisi ni ule ukweli kuwa haiwezekani kwa nchi yenye serikali yenye kila taasisi na nyenzo za usalama kuachia mabilioni ya shilingi yachotwe na kusombwa kwenye magunia kama dagaa. Je ina maana vyombo vyetu vya usalama havikujua wala havijui? Bila shaka wanajua kila kitu.  Na si ajabu hata vilishiriki katika kufanikisha jinai hii. Haiingii akilini eti serikali haikujua ujambazi huu. Kama haikujua basi hafai kuendelea kuwa madarakani. Kwa kazi ipi iwapo imegeuka mhuri na koleo kuibia fedha zetu? Haiingii akilini kusema kuwa rais na mawaziri na vyombo vya usalama havikujua kila kitu.
Bahati nzuri, tumekuwa tukishinikiza rais achunguzwe na kujua mchango wake katika kashfa hii ambayo ilianza chini ya uangalizi na maelekezo yake akiwa waziri wa Nishati na Madini na baadaye waziri wa fedha. Bahati nzuri zaidi wazito wameanza kuongea lugha ile ile kwa ufasaha zaidi hata baada ya wachambuzi na waandishi wa habari kulifichua lakini wakapuuzwa. Rejea maneno ya mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alaiyekaririwa akisema, “Mwaka 1994 wakati IPTL wanaandika MoU (makubaliano ya awali) na Serikali, Waziri wa Nishati na Madini alikuwa Kanali Jakaya Kikwete, mwaka 1995 wakati mkataba wa kununua umeme unasainiwa kati ya Serikali na wawekezaji hawa, Waziri wa Fedha alikuwa mtu aitwaye, Kanali Jakaya Mrisho Kikwete.” Nani anashinikiza rais Jakaya Kikwete achunguzwe ili kuchimbua mzizi wa tatizo zima? Je Makinda ataruhusu hili?  Nini kifanyike? Jibu si rahisi. Kama wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wangeacha kigeugeu na kulinda ufisadi walipaswa kuungana bila kujali itikadi na mafungamano wakamng’oa Makinda kwanza, halafu wakachagua mtu mwenye udhu asimamie Bunge kufumua na kuusuka upya mfumo mzima wa kijambazi.
Kinachogomba hapa ni utashi wa wanasiasa wetu. Ni bahati mbaya kuwa hata upinzani umeingia mkenge ule ule kwa kutaka mawaziri pekee ndiyo wawajibishwe wakati wenye mradi wanachekelea na kuendelea kuandaa mazingira ya ujambazi mwingine.
Bunge lisipoangalia litaishia kubweka na kugeuka mhuri wa kubariki jinai hii ambayo tuendako inaweza kuangamiza taifa. Kwa wanaojali sana ndiyo maana tukapendekeza wananchi kuingia mitaani na kuondoa utawala na mfumo mbovu unaokumbatia na kushiriki maovu.
Kwa vile Bunge limeonekana kuwekwa mfukoni, kuna njia mbili tu zilizobaki za kuondoa uoza, ima umma kuingia mitaani au kungoja kusikia wafadhili wataamua nini. Hata hivyo, tusitegemee sana wafadhili. Maslahi yao yakihakikishwa, wanabadili msimamo. Maana, huu siyo ujambazi na uhujumu wa kwanza. Hata hawa watuhumiwa wawili yaani James Rugemalira na Harbinder Sethi Singh tunaohangaishwa nao si chochote wala lolote bali makuwadi wa kawaida wanaolipwa bakshishi na kuwezesha wakubwa kuondoa na chumo lote. Wenye mradi wako nyuma ya pazia wakivuta kamba na kupanga ujambazi mwingine.  Anayebisha ajiulize ilikuwaje waziri Sospiter Muhugo na uprofesa wake kukubali kupewa dola milioni 95 zinazosemekana kusombwa kwa magunia. Ni wazi kuwa mtandao wa ujambazi hu ni mkubwa kuliko tunavyodhania na kuelewa. Bila kumchunguza rais na kuiwajibisha serikali yake, Bunge linapoteza muda na fedha yetu bure. Hili halitawezekana bila kumng’oa Makinda kwanza.
Ukiangalia hata lugha ya maazimio inayoongelewa si ya kutatua tatizo bali kuliahirisha. Wanaongelea kujizulu kwa mawaziri bila kutamka wazi kuwa wafilisiwe na kutupwa gerezani hadi ukweli utakapojulikana. Wanaogopana na kulindana huku umma ukiendelea kuwa maskini tokana na ulafi na ufisi wao.
Kwanini wabunge hawakujifunza tokana na Richmond? Lowassa aliachia ngazi na baadaye mawaziri wengine kwenye kashfa nyingine, mbona sasa mchezo ule ule umerudiwa? Dawa ya kuondokana na uoza nchini ni kumchungaza kutimua serikali yote ili liwe somo kwa watakaofuata. Mwandishi wa makala hii anatarajia kutoa kitabu cha NYUMA YA PAZIA kitakachochapishwa nchini Kameruni baada ya wachapishaji nchini kuogopa kukichapisha. Kinafichua uoza na mbinu ambazo wakubwa hutumia kuibia mataifa yao kwa njia ya kufungua makampuni na kuwapa makuwadi wao wanaopewa tenda kama IPTL na wakubwa zetu.
Chanzo: Tanzania Daima leo.

No comments: