Wednesday, 24 December 2014

Kijiwe chamuaga Werema kwa mipasho!

          Mgosi Machungi anaingia huku akiimba kana kwamba ana mtu wake anayempa vipande vyake.
          Anaamkua bila kujali na kuendelea kuimba, “Nenda Fedick Weeema nenda. Nenda jaji junk. Nenda jaji janga. Nenda tu umenyea kambi. Ushakula vya kutosha nenda kabuikie mbali.”
          Mpemba akionyesha furaha na mstuko wa wazi anaamua kutia timu kana kwamba walikuwa wamepanga wimbo huu na Mgosi. Anakwanyua mic, “Nenda wala usiangalie nyuma. Nenda tu mwanakwenda. Msiba ulotuachia watosha. Nenda ukaajiriwe na PAPu na VIPi kama Pat Rutabanonihino. Nenda ukawatumikie mabwana zako. Nenda tu hakuna anayekuhitaji.”
          Ngoma inzidi kunoga kwani Mgosi anaendelea, “Nenda sasa unanuka.Unanuka ufisadi. Umeoza na kuozeana nenda tu mwanakwenda.     Nenda huna wa kukulilia isipokuwa Kikwekwe.Kikwekwe atakulilia. Atakumiss.Amekusifia kwa kazi "njema" kwake na IpTL.”
          Mbwamiwtu anadandia mic na kuweka kibwagizi akiwaigiza Mgosi na Mpemba, “Hata hivyo, umma hauoni kazi njema zaidi ya machukizo ujambazi na hujuma. Nenda mura ukale bukima na musuli. Nenda kwa haraka nenda Harbinger Sethi Sing atakumiss. Mafisi watakumiss.”
          Mijjinga anaamua kuingia kwa wimbo tena kwa lafudhi ya kisukuma. Anahanikiza, “Jimmy Rugemalayer atakuombolezea.Wadanganyika watakuzomea. Jagishi nkwinga. Jagi ng’wana jaga. Jaga kajagi lulu, pela ng’wana njinga.”
Akiwa anaendelea kurap Kapende analalamika kuhusu yeye kuimba kisukuma.
          Mijjinga anaamua kurejea kwenye mstari na kuhanikiza huku akimtazama Kapenda kuonyesha amemwelewa, “Nendaga mwana kwendaga.Tokomea huko utokomeako hata ukicheza litungu. Nenda usigeuke nyuma tukakuonea huruma. Nenda huko usirejee tena kwenye ofisi zetu. Nenda na balaa lako.”
           Leo ni kuimba kwa kwenda mbele. Naona na Mheshimiwa Bwege ameamua kutia timu huku akiwaonyesha dole akina Sofi Lion aka Kanungaembe na Kanji. “Nenda na kazi zako chafu. Nenda msomi aliyefanya ujinga kuliko hata mbumbumbu. Nenda msomi mbumbumbu. Nenda tu. Tangulia mwana kutangulia. Muongo anangoja kukufuata. Nenda tu usigeuke nyuma ukawa jiwe la chumvi japo u zigo la uoza. Nenda tu mwanakwenda mura. Nenda usinung'unike. Nenda usisingizie. Nenda usilaumu. Nenda huenda bosi wako atakuzawadia. Kwa kazi "njema" ulofanya ya kutetea uoza wake.”
          Tulidhani ulikuwa mwisho wa mashairi ngonjera na nyodo tusijue ndiyo vilikuwa kimeanza. Mara nona mzee Maneno anauganisha akaiimba kwa lafudhi ya kizaramizi, “Huenda atakupa ubalozi kama wengine. Siku akikuteua. Nitararua nguo zangu. Nitavaa magunia. Nitajipaka majivu.Nitaomboleza. Nenda mjalaana nenda. Nenda usigeuke nyuma. Nenda ushatuchafua. Nenda ushatuibia. Nenda wala hatukutaki.Nenda kwatumikie hao waliokuumba.”
          Mipawa naye hataki kuachwa nyuma. Anamua kukamua kwa lugha ya kisukuma kama mwenzake Mijjinga, “Nendaga tuache tusherehekeeage. Tusherehekee anguko lako takatifu.Umetoka kwenye utukufu na kuangukia kwenye ukufu. Nenda usivuruge sherehe zetu. Nenda tuache tujipongeze.”
          Wakati akijiandaa kuendelea kumwaga mipasho mzee Kidevu anaamua kunyang’anya mic na kumwaga mistari, “Kama kibwengo nenda. Nenda na mzigo wako wa moto kichwani.Kama mtalaka nenda. Ndoa imekushinda. Nenda kaolewe na akina Harbinder wako. Nenda na nyodo zako. Nenda usilete fyoko. Nenda mura nenda.”
          Baada ya Msomi Mkata tamaa kuridhika kuwa watu wamemwaga usongo na nyodo zao anaamua kuingilia kati. Anakohoa kidogo na kusema, “Jamani imetosha na naamini ataipata ajue tulivyompenda sana kiasi cha kumsindikiza kwa nyimbo na ngonjera. Hata hivyo, nimegundua kuwa mipasho yenu inafikisha ujumbe. Hakuna sehemu mmnigusa kama kusema huenda jamaa anaweza kuteuliwa ubalozi kama jamaa yangu Kamara aliyeghushi na Komba aliyesafirisha wanyama wote wakaishia kuteuliwa ulaji nje.”
          Sofia aliyekuwa amefura nusu kupasuka anaamua kula mic, “Nanyi sasa mmezidi unazi. Kwani mtukufu akimteua kuna kosa gani iwapo ana mamlaka kikatiba?”
          Kapende anakula mic, “Hivi mnazi ni nani kati ya tunaotetea haki na uwajibikaji nawe unayetetea ukale na ufisadi?”
          Mheshimiwa Bwege anadandia, “Kwanini da Sofi usiombe kazi kwenye ofisi ya uenezi ukatia timu na Nipe Mapepe ambaye huongea utadhani hakujaliwa ubongo bali utumbo? Kama unampenda mura si uende akuwowe? Maana jamaa walivyo kwa kuwowa hovyo hovyo sina mfano.”
          Kanji naye hajivungi, anakula mic, “Sasa dugu yangu Bwege sasa veve bwege kweli kweli. Kwanini taka mura oa Sofi kwenda gombana na bibi yake? Kama naona oa zuri sana basi toa bibi yako kwa mura.”
          Mheshimiwa Bwege kaguswa pabaya. Anajibu mapigo, “Nenda kakuoe wewe kama Harbinger. Unadhani hatujui kuwa huyu ponjoro mwenzako anatumiwa?”
          “Sasa dugu tusi mimi. Mimi hapana iko kama Harbinger. Ile kama tumiwa sauri yake. Mimi hapana tumika. Kama iko mtu nataka tumika basi mimi napenda tumia yeye.”
          Mbwamwitu, huku akimtazama Kanji anasema, “Basi dugu yangu nenda tumia Sofi yako.”
          Msomi anaamua kula mic, “Japo mnaweza kusema msemayo kama masihara, ukweli ni kwamba hawa matapeli tunaoshuhudiwa wanatumiwa mbele nyuma kulia kushoto. Rejea Rugemalayer alivyotembeza mshiko karibu kwa vigogo wote kuanzia wa siasa hadi wa majoho. Huu ni ushahidi kuwa hii biashara si ya mtu mmoja bali wengi hata usiowategemea. Nadhani ndiyo maana wanashikwa kigugumizi kuwajibishana.”
          “Hebu ngoja,”anasema Msomi huku akiangalia upande wa Kamata. Anaendelea, “Hivi lile siyo shangingi la Mura We-rema?”

          Anatugeukia na kusema, “Hebu twende tukamtia adabu nyani dume huyu.” Wote tunatimka kuelekea Nyerere Road kwenda kumfanyia kitu mbaya mura We-rema. Tulimfanya nini? Please don’t ask.
Chanzo: Tanzania Daima leo.

No comments: