Wednesday, 10 December 2014

Escrow: Tumeahirisha tatizo “kumalizana”


Ukichunguza kwa makini jinsi sakata la kashfa ya escrow “lilivyomalizwa’ kimizengwe, haraka na kulindana, utagundua mapungufu mengi. Bunge, pamoja na kujivuvumua kuwa limefanya kazi pevu ya “kuwawajibisha” watuhumiwa wa skandali hii, limewanusuru wengi hasa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaojifanya kutojua ama kushiriki wakati ushahidi unaonyesha kuwa ndiyo wenye mradi mzima. Hawa akina James Rugemalira na Herbinder Sethi Sing ni makuwadi tu.
Ukichunguza maneno ya walioamua kwa mizengwe na ukosefu makini wa kashfa ya escrow, unagundua kuwa waliahirisha tatizo baada ya kutumia siasa za kumalizana na kuwekana sawa.
Nukuu za wahusika zinaonyesha kuwa uamuzi huu hatari kwa taifa haukugusa wahusika halisi zaidi ya vijidagaa vilivyotolewa kafara. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alikaririwa akisema, “Niombe tu Waziri Mkuu awe mkali ili tusifike kwenye mshike mshike kama huu tuliofikia kwa sasa.”  Huku ni kubembelezana. Hakuna haja ya kumuomba mtu kuwajibika wakati amethibitika wazi kazini. Mbowe alipaswa kumwambia Waziri Mkuu aondoke wenye uwezo waje na kulitumikia taifa kwa uadilifu na maarifa. Mbowe aliongeza, “Waziri Mkuu uwe mkali kwa kweli.” Rais hapa yuko wapi wakati Tundu Lissu anasema wazi kuwa ndiye chanzo cha haya yote? Rejea kuingizwa kwa mama wa ufisadi huu kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ambayo imekuwa ikiliibia taia kwa miongo zaidi ya miwili kiasi cha kusababisha kufilisika kwa Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) ukiachia mbali kuchangia ulanguaji na migao ya umeme vinavyodumaza uchumi wa taifa na kufanya maisha ya watanzania kuwa magumu.
Makamu mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe Ludewa (CCM), alisema, “Kumekuwa na makosa yamefanyika kwenye baadhi ya maeneo, hivyo hatua zimechukuliwa.”  Je hatua zilizochukuliwa ni mujarabu na zinaondoa tatizo au kuliahirisha?
Mwingine aliyechangia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira aliyesema, “Kazi haikuwa rahisi, lakini tumeelewana na aliyosema Zitto ndiyo tuliyokubaliana kwa kuwa CCM haina sera ya kukubali jambo lolote ambalo linaminya maendeleo ya wananchi.” Kumbe wameelewana! Anasema eti CCM haina sera hujuma kwa wananchi wakati imekuwa kinara wa kufanya hivyo. Go tell it the birds Wassira.

Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiel Wenje alikaririwa akifichua wazi mbinu iliyotumika kufikia uamuzi wa aibu. Alisema, “Kwa hiyo Spika mimi nakubali turudi saa kumi ili hiyo timu ikakae na sisi kwenye vikao vyetu tupewe taarifa tukifika hapa baadaye tumalizane tu.”
Mwingine aliyechangia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Christoms aliyesema “Waziri Mkuu angeondolewa angebaki kuwa waziri mkuu mstaafu. Serikali ingelazimika kumlipa asilimia 80 ya mshahara wa Waziri Mkuu aliyeko madarakani. Sasa kwa nini tufike huko wakati tunaweza kuwawajibisha waliohusika moja kwa moja.” Hoja dhaifu sana. Inajenga shaka juu ya uwezo wa mhusika. Sijui huyu anafundisha nini kama hawezi kufikiri kwa kina (critical thinking)? Huwezi kulea ufisadi wenye kula pesa nyingi kuliko hii unayosema ingetumika kumlipa waziri mkuu kama angewajibishwa.
 Hoja nyingi hapa ni dhaifu kwa vile zimeshindwa kuangalia tatizo zima kuwa ni serikali nzima. Kama wangeondoka wote ili kutoa onyo na nafasi kwa kuandika katiba mpya itakayopambana na ufisadi, tungeokoa fedha nyingi kuliko hizi wanazoongelea za kumlipa waziri mkuu mstaafu, Kama Lowassa hakustaafu, aliondoka kwa kashfa na rafiki yake anaendelea kumlipa na hakuna anayehoji, unategemea nini? Pesa anayopokea kama si wizi na kulipwa kwa wizi na ufisadi aliolipwa analipwa za nini? Dawa ilikuwa kuondoa serikali nzima pia kuwafungulia mashtaka wote waliounda serikali ili kuitakasa nchi tokana na ufisadi.
Katika waliotoa hoja zenye mashiko ni jaji Joseph Warioba aliyekaririwa akisema, ‘Naona kama kulikuwa na namna fulani hivi ya kulindana. Uamuzi wa Bunge ulifikiwa kutokana na msukumo wa wananchi wa kutaka kujua hatima ya suala la escrow na IPTL, wahisani kusitisha msaada kwa sababu ya uchotwaji huo wa fedha pamoja na siasa, hasa zinazolenga urais mwaka 2015." Huu ndiyo ukweli kuwa kilichofanyika ni kulindana au kuwekana sawa kama tulivyoonyesha hapo juu. Naye Katibu mkuu wa CHADEMA dk Wilbrod Slaa aliendelea kumuandama rais Jakaye Kikwete akisema, “Suala la Escrow ni bichi kuliko mnavyofikiria, lugha ya Mwalimu Nyerere aliposema watu wanaokimbilia Ikulu tuwaogope kama ukoma, Ikulu ni mahali patakatifu mahali pa heshima kumbe wakubwa walijua kuna nini? Atoke Kikwete hadharani kama nasema uongo.”
Wapo waliopongezea uamuzi hafifu wa Bunge wa kuikoa serikali kwa mara nyingine wakati ilipopaswa kufurushwa. Ni baada ya Bunge kuja na viini macho kuhusiana na kashfa ya escrow ambayo wengine huiita screw. Pamoja na uamuzi wa aibu na haraka, wahusika wanahanikiza watuhumiwa wawajibishwe na siyo kufilisiwa wala kufikishwa mahakamani.Hawaelezi fedha yetu itarejeshwa vipi.
Hawakufumua hata mama wa tatizo yaani kampuni ya IPTL ambayo tunaambiwa huyu mhindi anayejifanya ni yake wala si yake wala hajainunua kwa kufuata utaratibu.Ujiulize cha mno walichofanya zaidi ya kuhamisha tatizo huoni kitu. Kuna hoja ya watu makini hapa au wababaishaji tu wanaoonekana kutojua wanachofanya? Sana sana kilichofanywa na Bunge ni kuhalalisha mfumo wa kifisadi tokana na upogo, papara na upofu wa kuridhika na vitu vidogo na ukosefu wa malengo makubwa. Rais anaendelea kutesa huku akiendelea kuwachezea mahepe.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano.

4 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Muda mrefu sijapita hapa "kunoa ubongo"
Sijilaumu kurejea.
ASANTE

NN Mhango said...

Mzee wa Changamoto karibu tena. Huwa napita kwako na kunoa ubongo. Habari za Mitaa ya kati? Siye huku ni winter ya kuua mtu.

Anonymous said...

Nani ana mchunguza nani!? Nani anamuhukumu nani. Kama vile kwenye kitabu fulani cha Dini Neno akasema nchi kavu na maji yatengane. Halafu Neno akaendelea hivyo Neno ana mchunguza Neno au vipi Mwalimu?

NN Mhango said...

Anon, kama unaongelea viongozi wa dini la msanii wenu mkuu ni kwamba wote wnachuuzana na kutumiana huku kila mmoja akimuona mwenzake juha. Hata hivyo hakuna mshindi ikizingatiwa kuwa wote huvuna wasipopanda na hupanda wasipovuna. Kwangu wote ni wasanii wanaowachuuza wananchi wenye kudanganywa na majoho na maneno yao wakati matendo yao machafu. Vitabu vikaongelee huo upuuzi wake huko vilikotoka. Kwani nani hajui kuwa bahari na ardhi vimeshikana japo wao wanasema vimetengana?