Friday, 5 December 2014

Wananchi wanyang'anyeni polisi kadi za CCM

Japo kinaweza kuchukuliwa kirahisirahisi na kitendo cha kawaida, kitendo walichotenda polisi kule Kyerwa mkoani Kagera ni cha aibu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) serikali na jeshi la polisi kwa ujumla. Mkuu wa polisi wa wilaya ya Kyerwa OCD Pius Paul anatajwa kuwa nyuma ya hujuma hii ya kizamani. Ushahidi wa mazingira utokanao na upendeleo na kitendo chake ni kwamba huyu atakuwa mwanachama wa CCM piga ua.
Vyombo vya habari viliripoti kitendo cha kishenzi cha polisi kuzuia na kuupiga mabomu mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) uliokuwa umepangwa kufanyika wilayani humo hapo Oktoba 30 na kuhutubiwa na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Halima Mdee. Kinachoshangaza ni ile hali ya polisi kupokea taarifa ya mkutano tajwa na kukaa kimya hadi kutoa zuio saa saba usiku. Huu ni ushenzi na uhuni hata kama unatendwa na polisi wanaolipwa mishahara toka kwenye kodi za hao hao wanaowahujumu, kuwadhalilisha na kuwatesa bila sababu
Kuna haja ya polisi wetu kutaja uanachama, ushabiki na ukada wao kwa CCM. OCD Paul anapaswa kuwajibishwa mara moja ili liwe somo kwa wengine wenye mawazo mgando na uhuni wa kisiasa. Kama Paul amenogewa na siasa basi avue magwanda ya jeshi na kuvaa ya CCM ili ajulikane kuliko kuchanga mambo na kusababisha mgongano wa kimaslahi katika utumishi wa umma licha ya kuvunja katiba. Huyu hawasaidii CCM bali kuwaumiza. Wanapaswa kumuogopa kama ukoma vinginevyo lao liwe moja. Je huyu mkuu wa polisi alihongwa cheo ili afue nepi za CCM? Inakuwaje mtu mzima na anayepaswa kuwa na akili timamu na kujua mipaka ya mamlaka yake afanye hivyo kama hakuna namna? Ajabu polisi hawa hawa ndiyo walinzi wazuri wa ufisadi nchini ambapo watuhumiwa wengi wanaendelea kutanua mitaani. Ni hawa hawa wanaolalamikia uchache wa polisi wa kulinda wananchi lakini wakapata polisi wa kupiga wananchi na kulipua mabomu. Watanzania wanataka huduma na si mabomu na vipigo.
Kisheria polisi hawapaswi kushiriki siasa wala kuwa wapenzi au wanachama wa chama chochote. Hii imewekwa ili kuwawezesha kufanya kazi zao kitaalamu na bila upendeleo. Sasa inapofikia mahali polisi wanaonyesha unazi wazi wazi, huku licha ya kuvunja sheria, ni utovu wa nidhamu usiopaswa kuvumiliwa.
Kama serikali inafurahia kwa vile inanufaika na jinai hii, basi wananchi wachukue hatua mujarabu kwa kuhakikisha wanawakataa polisi wanaowahujumu kutokana na itikadi zao za kisiasa jambo ambalo ni haki yao kikatiba. Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kyerwa, Deus Rutakyamilwa alikaririwa akisema, “Tulitangaza mikutano yetu mji mzima, tumepita mbele ya kituo cha polisi hawakutuzuia, lakini nashangaa ilipofika saa 7:00 usiku OCD alinipigia simu akiniomba niende kituoni nikamkatalia kwa sababu ulikuwa usiku.” Kwanza, kwenda nyumbani kwa mtu saa saba usiku ni kuvunja haki yake na kukiuka taratibu hasa ikizingatiwa kuwa Rutakyamilwa hakuwa mtuhumiwa wa kosa lolote ambalo lingewalazimu polisi kufanya kazi usiku wa manane kama wanga.
Rutakyamilwa aliongeza, “Katika hali ya kushangaza akaamua kuja mwenyewe nyumbani kwangu kuniletea zuio la mkutano.” Huu ni uhuni na ujinga wa hali ya juu kutendwa na ofisa wa polisi mwenye cheo kikubwa kama hiki. Kuna haja ya kumchunguza mhusika ili kufichua mengi hasa kuhusiana na sifa zake za kupewa cheo hicho, aliyempa cheo hicho na mengine ambayo hayajulikana aliyokwisha kutenda. Paul amehujumu jeshi la polisi wazi wazi. Itakuwa ajabu kama wakubwa wake wa kazi watamnyamazia ili kuonyesha kuwa lao ni moja na wanavyojikomba kwa serikali na chama tawala.
Na hii si mara ya kwanza kwa polisi kuonyesha upendeleo wa wazi wazi na kuvunja sheria. Nani mara hii kasahau mauaji ya kinyama ya Arusha ya Januari 5, 2011 ambapo polisi walituhumiwa kurusha mabomu yaliyoua watu watano? Nani mara hii amesahau au kusamehe amri ya waziri mkuu Mizengo Pinda kuwataka polisi wawapige wapinzani? Pinda alikaririwa akisema, “Mheshimiwa Mangungu hapa ameanza vizuri, lakini mwisho hapa naona anasema vyombo vya dola vinapiga watu, ukifanya fujo au umeambiwa usifanye hiki ukaamua kukaidi upigwe tu.” Pinda alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu bungeni. Na kweli baada ya Pinda kutoa amri hiyo, vyombo vya habari viliripoti visa vingi vya unyanyasaji vilivyotendwa na polisi nchini. Eti huyu naye anataka awa rais! Akiwa rais si wananchi watauawa kama wadudu na jeshi lake la polisi analopenda kulitumia kufanya kile waingereza huita dirty laundry?
Tumalizie kwa kuwahimiza wakuu wa serikali, CCM na serikali kukomesha uhuni huu ili wasilitumbukize taifa kwenye machafuko kutokana na kutotenda haki na kutekekeza sheria kwa upendeleo. OCD Paul anapaswa kuwa mfano kwa kushughulikiwa ili wenye ndoto na upogo kama wake watie adabu. Kuna haya ya wananchi kuhakikisha polisi makada na mashabiki wa CCM wananyang’anywa kadi za CCM na kufutwa kazi mara moja.
Chanzo: Dira ya Mtanzania.

No comments: