
Bwana Joni Kanywaji Makufuri,
Kwa heshima na taadhima napenda nikusalimie na kukutakia afya njema wakati nikiandika yafuatayo kama nilivyoelezwa.
Kwa ufupi hii ni injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Mpayukaji Msemahovyo, mtume kwa walevi wote.
Hii mhishimiwa ni fursa ambayo hutaisahau maishani mwako kupata kuandikiwa waraka na mtume kama mimi.
Mimi ni tofauti na matapeli wanaojiita mitume na wachungaji wakati ni
matapeli wa kawaida wanaowachuna watu kwa kutumia majoho na jina la
Mungu.
Mimi ni tofauti na akina Ka-Tortoise, Rwakatarehe, Gamanyua,
Mwakasenge, Lushekelo au Muzee wa Upakazio na matepeli wengine wengi
waliojivika majoho wakati ni wezi wa kawaida.
Kijiwe kimeniagiza nikuandikie waraka huu kuelezea msimamo wao baada
ya kuona walevi na Wadanganyika wakikenua njino walipomuona mkuu
akizindua ujenzi wa daraja la kisasa na kisasi la Kigamboni. Wanakijiwe
hawakuwa na furaha. Mwanzoni niliwashangaa nisijue nao walikuwa
wakinishangaa!
Baada ya Dk. Msomi Mkatatamaa kunielimisha niligundua ni kwanini. Kuna
madai kuwa kuna wahuni wanataka kutoza nauli ya kuvuka daraja hilo kwa
vile wamelijenga. Kijiwe kinasema nasi tuwatoze kodi kwa kujenga kwenye
ardhi na bahari yetu.
Wanakijiwe wana wasiwasi kuwa kama daraja litajengwa na makampuni
yaliyopata tenda kupitia sayansi ya Ten percent basi litabomoka na
kuangamiza maisha ya walevi wengi. Mie na bi mkubwa tunaogopa sana
samaki. Kwani kwa mamia ya miaka, kama mkuu, tumekuwa na mapenzi makubwa
ya kuwala.
Hivyo, tunahofia kuwa ufisadi wa ten percent unaweza kuwapa fish
nafasi ya kutupenda kwa kutugeuza kitoweo kama ambayo maisha yetu yote
tumewageuza.
Baada ya kutumia madaraka yangu kijiweni kumwezesha bi mkubwa kufungua
NGO ambayo ilimuingiza pesa, tulifanikiwa kununua uwanja kule Kigamboni
hasa baada ya kusikia kuwa kuna mpango wa kujenga daraja.
Hatukuwa tumeona mbali kama walevi. Pia tuna bahati kuwa uwanja wetu
haukukumbwa na sekeseke la kupisha daraja na wajanja fulani kuutumia
kujilipa fidia badala ya sisi.
Mwanzoni wasiwasi huu ulipoonyeshwa kwangu niliwaona walevi kama
manazi wasiopenda hata kukubali kuwa haya ni maendeleo. Walinipa mifano
ya barabara nyingi zilizojengwa ndani ya wiki na kuharibika ndani ya
masaa kaya nzima.
Pia walikuwa na shaka na hili la kutozwa nauli. Walisema kuwa mbona
kwenye daraja la Jangwani na mengine mengi hawatozwi ushuru wala nauli.
Kwani daraja ni treni au basi au ndege? Je, daraja linatuma mafuta au
umeme? Je, ni lini walevi watalitumia free wakati kaya na ardhi vyao
vinatumika free?
Ingawa walevi ni walevi, wana hoja. Walisema kuwa wakikumbuka jinsi
EPA ilivyoleta uchakachuaji wanakosa imani na binadamu ngurumbili.
Pia walitoa mfano wa Richmond ambapo mkuu na Ewassa waliahidi kuwa
mgawo wa umeme ungekuwa historia na badala yake ikawa kinyume. Sana sana
faida ya mgawo ni kutengeneza na kutotoa vitegemezi vingi ambavyo
walevi hawawezi kuvimudu na mstakabali wao unazidi kubomolewa.
Mie nashukuru Mungu bi mkubwa alikubali ushauri wangu wa kuweka
kakomeo ili asivitotoe vikatunyotoa roho maana ukiona hizo shule za kata
na matuisheni ya wezi wanaoitwa walimu utaogopa. Jamani mtoto
asipokwenda tuisheni siku mbili maksi zinashuka kama ndege ilizomika!
Mwe! Tunakwenda wapi?
Sasa daraja likijengwa na watu wenye akili na roho za kituisheni si
litaua hata kabla ya mwaka? Lazima tuseme kuwa daraja lisijengwe kivoda
fasta ili kunusuru maisha ya walevi wetu wapenda amani na mshikamano
hata kama havipo kivitendo bali kinadharia.
Wana Kijiwe siku zote ni mabingwa wa hoja kutokana na wote kuwa
madaktari tena wa kusomea na si heshima kughushi wala kugawiwa
kishikaji.
Walitoa pia mfano wa maisha bora kwa walevi wote ambayo yameishia kuwa
maisha balaa kwao huku yakiwa bora kwa nyumba ntobhu. Hivyo siandiki
kwa hiari yangu wala ushabiki bali kuwasilisha kilio cha walevi ili
kikufikie nawe ukifikishe kunakohusika.
Kitu kingine walichoniambia walevi tena chenye kusikitisha ni wasiwasi
wao kuhusiana na Eniesiesiefu (ENSSF) inayojenga hilo daraja.
Tulikusikia ukisema kuwa mkurugenzi wake Juma Kidau apewe nishani badala
ya wanagesi. Hayo ni yenu mtajuana. Mnaweza kupeana nishani hata za
ufisadi na usanii. Walitaka kujua ni kwanini haina huruma na wachangiaji
na inawekeza njuluku yao kwenye biashara wakati watoa michango
wakiendelea kusota na hakuna anayejali?
Kusema ukweli nilishindwa kuwajibu kwa vile mie si mwajiriwa wa lisirikali na Eniesiesiefu wenye maulaji yao.
Kwanza, walevi walitaka wapewe hakikisho kuwa hakutakuwa na rushwa ya
kuweza kusababisha daraja lijengwe chini ya kiwango na kuua walevi wasio
na hatia kama ambavyo imewahi kutokea kwenye kashfa ya MV Bukoba na
lile jahazi lililoua watu hivi karibuni kule Zenji.
Tukizingatia matukio hayo hapo juu ambayo yaliacha misiba mikubwa kwa
walevi, kama thinkers of our own light and time, we need assurance from
you by getting it from the mounth of the horse. Mark my words; I am not
saying you are a horse neither are we. Again, we need convincing
explanations befitting thinkers not horses like your cheerleaders and
major domos.
Samahani mhishimiwa, huwa nina ka-ugonjwa ka kupandisha mwenembago
ambapo hujikuta nikibwabwaja kikameruni ambacho naamini unakijua
kutokana na kuwa daktari kama mimi. Najua udaktari wako siyo wa kupewa
wala kughushi. Hivyo nisamehe. Naamini umenielewa bwana Kanywaji.
Tena kabla ya kusahau, napenda nichukue fursa hii kukwambia kuwa
Kijiwe kimenituma nikwambie umwambie bosi wako aache matusi ya rejareja
kama alilotoa juzi kuwa wapingaji wana viwanda vya kuunda uongo wakati
mwanzilishi ni yeye.
Kusema ukweli mimi na wana Kijiwe hatukupenda haya matusi ya nguoni
ikizingatiwa kuwa nasi ni wapinzani wanaopinga ulegelege na uholela wa
lisirikali la jamaa yako.
Acha niwahi Brela kuona orodha ya makampuni yaliyopata tenda ya kujenga daraja na mbinu waliyotumia kupata ulaji huu.
Bwana Kanywaji, mfikishie salamu zake ndugu yetu, mpendwa wetu, kipenzi cha wengi na chaguo la God, Dk. Njaa Kaya.
Chanzo: Tanzania Daima Sept. 26,2012.