Zoezi la sensa
linaloendelea limetupa mafunzo, na kufichua mambo mengi mojawapo ikiwa ni
serikali yetu kutumia vibaya madaraka yake. Kwa mfano, kuna kikundi cha kidini
eti kinachosema bila kuweka kipengele cha dini kwenye dodoso za sensa
hakitashiriki zoezi hili kana kwamba sensa ni kwa ajili ya kujua idadi ya
waumini. Sensa dhumuni lake ni kujua idadi ya watanzania ili kuweza kupanga
mipango ya maendeleo kulingana na idadi ya watanzania. Heri wanaopinga kushiriki
sensa wangetoa sababu kuwa serikali haiwahudumii ipasavyo kwa vile imegubikwa na
ufisadi, wangeeleweka na hata kupata uungwaji mkono. Kwa mfano, wakazi wengi wa
vijijini hawana huduma yoyote toka serikalini zaidi ya kuwatoza kodi.
Wangedai kujua pesa sensa imetoka wapi na inatumika vipi kutokana na
serikali yetu kuwa mahiri katika ufisadi. Rejea ripoti ya CAG kila mwaka
kufichua madudu ya kutisha na wahusika wasichukuliwe hatua za kisheria.
Turejee kwenye
kikundi kinachopinga sensa. Kikundi hiki chenye kila dalili za kuwa haramu
kinakwenda mbali zaidi hata kuwagomesha wananchi eti wasihesabiwe na serikali
inaangalia tu! Inashangaza kuona serikali ikipata mshipa wa kuwapiga wapinzani
kila waendapo lakini inaogopa kuwaadhibu watu wachache wanaotumiwa na mabwana
zao kuichafua nchi. Je serikali inafaidika nini na hali hii? Je kuna wakubwa
serikalini walioasisi mpango huu lakini wanajifanya hawajui? Hebu tuangalie kwa
mfano maneno ya rais Kikwete.
Akizungumzia
umuhimu wa kushiriki sensa na madai ya kuingiza kipengelea cha dini, rais
Kikwete alisema yafuatayo, “Katika mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa
Waislamu niliwaambia kuwa naelewa sababu na hoja za wao kukasirishwa na
kutokuzikubali takwimu hizo. Vile vile, niliwaeleza kuwa takwimu hizo si za
Serikali bali ni za mashirika hayo.”
Je hizo sababu
ambazo rais alizifanya siri ni zipi na waliongelea wapi lina na akina nani?
Kumbe rais na hawa jamaa wanaelewana na ndiyo maana hawashughulikii? Je huku si
kulea udini na upendeleo wa kidini? Rejea alivyoongelea suala hili kwa upole
tofauti na alivyowahi kuongelea maandamano na migomo tena baada ya kutoa polisi
wakaua na kutesa kama ilivyotokea Arusha mwaka jana na kwenye mgomo wa
madaktari. Kwa vile hawa ni wenzake, hatukuona akiwaita “wazee” wa
Dar Es Salaam kulaani wapuuzi hawa wanaotaka kujenga chuki za kidini kwa sababu
wanazojua wenyewe.
Ingawa rais
amewaomba watanzania kushiriki sensa, bado ameonyesha upole sijui au uungwana
sijui uvumilivu, anajua yeye mwenyewe na sababu ya kufanya hivyo unaweza kuiona
kwenye nukuu hiyo hapo juu. Lakini hii pia inatia shaka. Kwanini afanye uungwana
kwa kikundi chenye kutumia lugha za kigaidi lakini ashindwe kufanya hivyo kwa
wapinzani wanaofanya shughuli halali kisheria? Je kwa vile Kikwete ni muislamu
haiwezi kujenga dhana kuwa anawapendelea waislamu wenzake? Je hawa watu wanapata
wapi kiburi cha kushindana na serikali tena katika jambo halali na muhimu kama
hili kama hakuna namna na Kikwete kuifahamu? Kwanini wakristo hawang’ang’anii
kipengee cha dini au yao si dini? Je inawezekana kuweka kipengele cha dini kwa
kusikiliza dini moja? Na hao wasio na dini hizi za mapokeo tunawaweka kundi
gani? Nchi yetu ni ya watanzania kwanza waislamu wakristo na wengine baadaye.
Wakati tukipigania uhuru, tulifanya hivyo kama watanzania na si kama waislam
wala wakristo. Dini zinasajiliwa lakini utaifa hausajiliwi.
Inashangaza kuona
watu wakijivika majoho ya dini na kufanya mambo ya kisiasa badala ya kufanya
shughuli za kidini. Kwanini wasianzishe chama wakafanya siasa badala ya
kujificha nyuma ya majoho na dini?
Imefikia mahali
hata baadhi ya watu kuwaumiza wengine kama shinikizo la kupinga sensa. Habari
zilizoripotiwa tarehe 29 Agosti toka Shinyana kwa mfano, ni kwamba mtu mmoja
aitwaye Esther Zablon allipigwa na kuumizwa vibaya na mumewe aliyetajwa kuwa
Ismail Yahya kisa eti alitoa ushirikiano kwa maafisa wa sensa. Kwa serikali
inayowajibika huyu alipaswa kuwa somo kwa wengine. Je huyu aliyempiga mkewe kwa
sababu ya sensa angefanya hivyo kwa vile mkewe ametoa ushirikiano kwa CCM dhidi
ya wapinzani angefanywa nini? Kwa kusindwa kushughulikia watu wanaoleta
chokochoko kwa taifa, inajenga dhana kuwa wahusika ima ni wenzake rais au
wanamdharau kiasi cha kumfanya aonekane kama mtu wa kuogopa hata vikundi visivyo
na kichwa wala miguu. Ni ajabu kuwa anakuwa mwepesi wakushguhulika na hata
kuongelea mambo yasiyo muhimu kwa taifa. Rejea alivyoshindwa kutoa tamko kuhusu
mgomo wa madaktari akakimbilia kwenye mazishi ya Kanumba. Si ajabu kusikia
Kikwete akiongelea mipira ya Barcelona lakini huwezi kumsikia akiongelea migomo
iliyotomalaki na kuuliwa na mahakama kwa shinikizo la serikali.
Kwa namna rais
alivyoshughulikia suala la kipengee cha dini katika sensa ameonekana kuwa
legelege kama alivoonyesha kuanzia kupambana na ufisadi, udini, uvivu, matumizi
mabaya ya raslimali na fedha za umma. Je kazi ya rais ni ipi iwapo mambo
yanaharibika wakati yeye akiangalia? Anatufaa nini rais Kama huyu ambaye anaishi
kwenye dunia yake huku umma ukizidi kuteketea kutokana na kila mtu kujifanya
atakavyo? Leo kikundi cha dini kinapinga wazi wazi shughuli za umma. Kesho
kitataka hata tubadilishe bendera ya taifa au wimbo wa taifa vinginevyo
kitaingia msituni. je namna hii hatukaribishi nyenzo za kulibomoa taifa letu? je
rais anapolea udini anauangalia mstakabali wa taifa letu au wa dini yake?
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 12, 2012.
1 comment:
Jamaa IQ yake ni ndogo, anafikiria vitu basic tu. Kula, mpira, safari nje, labda na nyumba ndogo. Anatumia dini kujustify his existence.
Post a Comment