How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 7 September 2012

Polisi wajue kuna maisha baada ya kustaafu


HAKUNA ubishi kuwa jeshi la polisi la Tanzania sasa lina sifa mbaya kuliko wakati wowote katika hisotria ya nchi hata ilipokuwa chini ya mkoloni na KAR yake. Pamoja na kusifika kwa kuwa vinara wa rushwa nchini, jeshi la polisi sasa limeongeza sifa nyingine chafu, kuua raia wasio na hatia hasa wale wanaoshabikia upinzani.
Imefikia mahali jeshi letu linaua sana raia wasio na hatia kuliko hata majambazi au wale wanaouawa na majambazi kutokana na polisi kushikilia kuua badala ya kulinda umma ukiachia mbali baadhi yao kushirikiana na majambazi hao hao.
Jeshi la polisi sasa linaonekana kama genge la mauaji ambalo linaweza kufyatua risasi ( trigger happy) au kulipua mabomu bila kujali ubinadamu. Kinachogomba sana ni kwamba pamoja na jeshi hili kujirahisi kuruhusu litumike vibaya na wanasiasa wachovu, bado halijawa na fikra kuwa kuna kesho bila ya hao wanaolitumia vibaya.
Hakuna ubishi. Jeshi la polisi limewekwa kwenye mfuko wa CCM. Wengi wangedhani lingepambana na mafisadi na majambazi ambao wengine ni wadhaminini wa CCM badala ya wananchi wanaotimiza haki yao kidemokrasia yaani kuandamana na kuhudhuria mikutano ya kisiasa. Huku ni kuvunja katiba kosa ambalo hubeba adhabu kubwa sana kama sheria zitafuatwa vilivyo bila ya kubagua kama ilivyo sasa.
Je ni kwanini polisi wetu wamejidhalilisha kwa kujiruhusu kutumika kisiasa tena kinyume cha sheria? Jibu laweza kuwa zaidi ya moja mojawapo likiwa ni ukweli kuwa wengi wa wakubwa wa polisi wanateuliwa kutokana na mafungamano yao kisiasa, kujuana hata kuoleana.
Rejea IGP wa zamani Omar Mahita alivyowahi kusema kuwa kama CUF ni ngangari kisiasa basi yeye ni ngunguri iliyotafsiriwa kuwa CCM. Hutashangaa kusikia kuwa IGP ana uhusiano na rais kupitia ndoa. Hutashangaa kusikia Kamanda fulani ameteuliwa rasmi kwa ajili ya kuwashughulikia CHADEMA. Je watu wa namna hii wapo kwa ajili ya watanzania au jamaa zao na washitiri wao waliowateua na vyama vyao?
Je, wanapoua kuna mtu mwenye kuweza kuwashughulikia wakati wanaopaswa kufanya hivyo ni jamaa zao? Kinachogomba zaidi ni ule upuuzi wa eti polisi kuunda tume ya kuchunguza mauaji yaliyofanywa na polisi. Yaani polisi wanaua, wanajichunguza na kutoa matokea ambayo kila mtu anajua yanakuwa si matokeo kitu bali upuuzi. Wako wapi walioua Arusha? Wamefanywa nini walioua Mbarali? Wako wapi walioua Morogoro? Wako wapi walioua Tarime tena jana tu kabla ya mauaji ya Iringa? Nani amshitaki nani wakati wote mikono yao imejaa damu na haramu?
Polisi hawawezi kukana kutumika kisiasa. Walianza kutumika pale Chama Cha Wananchi (CUF) kilipoanza kuwa tishio. Baada ya CUF kuwa shirika moja na CCM na kuona kuwa CHADEMA ndiyo tishio, polisi walihamishia nguvu zao kwa CHADEMA. Polisi wanapaswa kufahamu kuwa watanzania ni watanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa na kidini.
Kwanini polisi wetu wameshindwa kuambua kitu kidogo? Hivi hawajui kuwa hawa watanzania wanaowaua kwa risasi kama swala kila siku ndiyo wanaolipa kodi zinazoendesha maisha yao ya kila siku? Isitoshe polisi hawa hawa nao wanaonekana kuwa vipofu kuhusiana na hali zao za kimaisha. Wanaishi kwenye maisha magumu ziangalie nyumba zao, mishahara yao hata sori za viatu vyao wengi vinavyokwenda upande hata magwanda yao. Kama siyo rushwa polisi wengi ima wangeumbuka kwa kukopa au hata kushindwa kujikimu. Waulize mshahara wao bila rushwa kama unatosha. Huo ndiyo ukweli.
Badala ya kujikomboa wanakubali kutumika kama nepi kwenye uhujumu wa kisiasa hata uchumi. Kama siyo rushwa na mapato haramu kazi ya polisi isingepata mtu wa kuifanya. Kuliwahi kutokea shutuma kuwa wanashirikiana na wahalifu hasa majambazi ukiachia mbali madereva wabovu na kuwabambikizia watu kesi.
Wanahitaji ukombozi kama nilivyowahi kuandika kwenye kitabu changu cha Saa Ya Ukombozi ambapo wanakijiji wenye hasira walitaka kuwaua polisi waliokuwa wakimlinda mkuu wa mkoa aliyetaka kuuza kijiji kwa mwekezaji uchwara. Lakini kiongozi wao wa mageuzi aliwazuia kufanya hivyo kwa vile wote walikuwa wakihitaji ukombozi.
Sasa wafanye nini? Badala ya kujirahisi na kukubali kutumiwa kisiasa na chama na serikali vilivyoko madarakani, waangalie mustakabali wao na wa taifa. Leo wanatumiwa na CCM kufanya uchafu wake. Kesho CCM inaweza kutimuliwa madarakani wakajikuta chini ya serikali mpya ya chama kingine kama ilivyowahi kutokea nchini Kenya, Malawi, Zambia na Burundi kwa nchi za jirani.
Polisi kama watumishi wengine wa umma wameapa kuwatumikia wananchi wote bila kujali dini wala itikadi na si kutumikia chama fulani. Hivyo, kuendelea kutumiwa kisiasa licha ya kujidhalilisha, polisi wanajenga uhasama na raia.
Tumeshuhudia uhasama wa namna hii ukisababisha maafa kwenye nchi nyingi mojawapo ni Kenya ambapo raia wamekuwa wakiuawa na polisi nao wakilipiza visasi kwa kuwaua polisi mmoja mmoja. Tumeshuhudia nchini Libya wakati wa kumwangusha imla wa nchi ile Muamar Gaddafi.
Polisi waliokuwa wakitumiwa naye sasa wamo mafichoni kuogopa umma kuwalipizia kisasi. Ajabu Gaddafi alipoambiwa angekumbwa na yaliyomkumba mwenzake wa Misri alijibu kwa kejeli kuwa ile ilikuwa Libya asijue ulikuwa mwanzo wa mwisho wake wa aibu. Hata jeshi la polisi laweza kusoma maandiko haya na kusema hii ni Tanzania wasijue mwisho wao unakaribia.
Wajue kuna maisha baada ya kustaaafu. Wajue nchi si CCM wala serikali yake bali wananchi. Wajue mishahara yao hata kama ni kidogo inatokana na kodi za hao wanaowaua. Lakini polisi hao hao wameishaua huko Arusha, Mara, Morogoro, Iringa, Mbeya na kwingineko.
Tumechoshwa na mauaji ya polisi. Hivyo, umefika wakati wa watanzania kukataa kutenswa kama wakimbizi kwenye nchi yao tena na kundi dogo la watu linaloishi migongoni mwao.
Tanzania ni nchi ya watanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa na za kidini lakini si nchi ya rais, CCM wala polisi wao wanaowatumia vibaya kukandamiza haki za binadamu kubwa ikiwa ni kuondoa uhai wa binadamu tena bila hatia. Kuna haja ya kuanza kutafakari jinsi ya kuanza mchakato wa kuwafikisha watawala wetu vichwa ngumu na wauaji The Hague.
Hili ni rahisi hasa kukusanya taarifa za watu waliouawa na polisi na kuangalia kama zinafika kiwango kinachokubalika mbele ya mahakama hii ya kimataifa.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 5, 2012. 

No comments: