Wednesday, 26 September 2012

Nani kiwanda cha uongo kati ya wapinzani na Kikwete?

 
Hivi karibuni, akizindua mradi wa ujenziw a daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam, rais Jakaya Kikwete alikaririwa akisema kuwa wapinzani wana viwanda vya uongo. Aliwanasihi bila kujinajisi, waache kusema uongo; wamsifie hata kama hawaoni sababu ya kufanya hivyo. Kwa wengi, maneno ya Kikwete yalikuwa kama harakati za mfa maji baada ya kuona mambo hayaendi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa Kikwete hajakidhi matarajio ya watanzania.   Nikiri; ilikuwa ni mara ya kwanza kwangu kusikia kuwa kumbe kuna viwanda vya uongo.  Mwanzoni nilidhani nilikuwa nimesoma vibaya. Nilidhani alimaanisha viwanda vya gongo. Kumbe rais alimaanisha viwanda vya uongo!  Kwa hadhi na nafasi ya rais, kwanza, lugha aliyotumia ni ya matusi ukiachia mbali kusahau kuwa aliyeanzisha “viwanda” hiyo vya uongo hata kabla ya wapinzani ni yeye na chama chake.
 
Alikaririwa akisema, “Watu wana uongo mwingi eti nimeuza eneo kwa Bush, huo ni upotoshaji mwingi. Maana kuna watu kila kukicha wana viwanda vya kutengeneza uongo. Wako ambao hawapendi maendeleo,” 
Kuuza nchi si lazima auziwe George Bush. Je ni wawekezaji wangapi wanafanya mambo kama vile wamenunua Tanzania wakiwamo Dowans waliotokana na kampuni iliyoingizwa nchini kinyemela na Kikwete na Lowassa ya Richmond? Je ni matapeli wangapi wanaitwa wawekezaji wakati ni waganga njaa na makuadi wa wakubwa wenye madaraka wasio na uzalendo wala udhu wa kuwa hapo walipo? Hapa rais anataka kumdanganya na kumfanya nani mpumbavu asiyeona yanayoendelea?
 
Tofauti na wapinzani ni kwamba huyu mwanzilishi wa “viwanda” vya uongo ni mwepesi wa kusahau ukiachia mbali kupenda kujisahaulisha na kujifanya hajui kinachoendelea. Hivi kweli Tanzania kuna kiwanda cha uongo chenye ukubwa na hatari kuliko kile kiitwacho Jakaya Mrisho Kikwete aka Kipenzi cha watu? Kuna kiwanda cha uongo kama “Tumaini lililopotea?”
 
Hebu tumpe ushahidi ili angalau imsaidie mheshimiwa huu kuamua nani mwenye kiwanda au viwanda vya uongo. Mwaka 2005 akiwa mgombea wa CCM aliwaahidi watanzania maisha bora chini ya kauli mbiu ya Maisha bora kwa wote. Je Kama rais hakuongopa, anaweza kuonyesha nini zaidi ya kulalamika kuhusiana na maisha bora kwa watanzania? Tofauti na alivyoahidi, rais ameletea maisha balaa kwa watanzania kutokana na kudaiwa kuwa alipata ushindi na kuwa rais kupitia pesa chafu ya iliyotokana na ufisadi wa EPA ambayo hajawahi kukanusha wala kutolea maelezo.
 
Kikwete aliahidi kutaja mali zake na mkewe. Hili huwa hapendi kulisikia achia mbali kutoa maelezo au kuzitaja hizo mali. Je anaogopa nini? Je kwa kutotaja mali wakati alipaswa kufanya hivyo na akaahidi kufanya hivyo si uongo? Nilishaliandikia zaidi ya mara saba lakini rais hajawahi kutaka hata kuligusia. Hata watu wake wa usalama huwa wanahofia hata kupiga mkwara kwa gazeti kwa kuhofia mengi yataibuka kuhusiana na usafi wake binafsi.
 
Turejee kwenye “viwanda” vya uongo. Kikwete aliongeza na kusema, “Hili daraja na barabara ambazo nasimamia vitabeba watu wa vyama vyote CCM, CUF, CHADEMA, TLP na wasio na vyama na wasiposhukuru au wakishukuru shauri yao lakini maendeleo yanafanyika na watu wanaona hata kama wanajifanya hawaoni,.”
 
Hii ni kauli ya ajabu inayoonyesha uwezo ima uwezo mdogo wa msemaji kuelewa mambo au kuamua kuongopa kusudi. Kwani ni wapinzani gani waliwahi kudai kuwa daraja na barabara vitatumiwa na wana CCM tu? Je kusema kuwa wapinzani wanaangalia miradi ya kitaifa kama mali ya chama si kuzua hata kuongopa? Wapinzani hawana ugomvi na kuanzishwa kwa miradi ilmradi wapate maelezo ya kina jinsi pesa ya walipa kodi inavyotumika.  Na isitoshe, Kikwete na chama chake hawajengi hivyo vitu kama hisani au msaada kwa watanzania. Wala hawajengi kwa pesa yao. Ni kazi ya serikali kufanya vitu hivyo kutokana na ukweli kuwa wananchi wanalipa kodi. Kinachogomba kwanza ni umadhubuti au uwezo wa kufikia viwango vinavyokubalika na gharama za miradi hiyo. ni ajabu kwa Kikwete kudhani kuwa watanzania wengi walio makini wanajiuliza swali moja kuu: Kama daraja la Kigamboni litajengwa hovyo hovyo kama barabara zetu kutokana na tenda kupatikana kwa kutumia ten percent, siku moja litaua wangapi? Huu ndiyo wasi wasi wa watu wenye kufikiri sawa sawa wanaojua jinsi serikali ya Kikwete inavyoendeshwa.
 
Muulize Kikwete kama anakumbuka alivyowahi kutamba tena hadharani kuwa ana orodha za wezi bandarini, majambazi na wauza mihadarati. Kama anakumbuka muulize tena, aliwafanya nini kama kweli alikuwa ana orodha yao zaidi ya kunogesha stori. je kama kweli anazo orodha za wahusika na vyombo vya dola vya kuwashughulikia, ana maslahi gani au ameshindwa nini kuwashughulikia? Je kuendelea kutowashughulikia wakati aliahidi kuwashughulikia si uongo tosha?   Ukimuuliza hili naamini hatakuwa na la kukwambia zaidi ya kukuweka kwenye kundi la watu wasiopenda maendeleo yake. amini maneno yangu. Hata baada ya watu wake kusoma makala hii, hawatajibu kwa kujua fika watakuwa wanamvua nguo mtu wao anayewatuhumu wapinzani kufanya kile ambacho kimemweka madarakani.  Ni mtu wa namna hiyo na kwa kiasi fulani watanzania wameishamzoea wakiomba Mungu muda wake uishe ajiondokee.
 
Kikwete kama rais aliapa kulinda wananchi na raslimali zao. Muulize hili amelifanyaje iwapo wanyama wetu wanatoroshwa huku serikali yake ikiwa inasema eti haina habari. Wananchi wanauawa na polisi kwa maagizo ya Kikwete kupitia wateule wake na usalama nchini umekuwa tatizo. Je wapinzani wakisema kuwa Kikwete aliwaongopea watanzania kuwa atawalinda wakati hafanyi hivyo ni kuchukia maendeleo au kuunda viwanda vya uongo? kama hivi ndivyo viwanda anavyoongelea Kikwete, tofauti na chake, ni viwanda vizuri maana hii ndiyo kazi ya upinzani-kumkosoa na kumshauri wanapohisi anakwenda ndivyo sivyo.  Kikwete aliahidi angefuata sheria za nchi na kuzitekeleza bila ubaguzi. Katika hili amenoa karibu kila eneo. Kuna watu kama rafiki zake na washirika zake kama Edward Lowassa na Andrew Chenge wako juu ya sheria.  Pamoja na wengine kukiri na wengine kuletewa ushahidi wa kutosha wa kushiriki wizi na ufisadi, bado Kikwete anasema ni wachapa kazi bora hakuna mfano. Hivi kuna kiwanda cha uongo kama hiki. Leo nimeongelea uchache tu juu ya products za kiwanda cha uongo cha Jakaya Kikwete. Kwa ufupi ni kwamba kama wapinzani wana viwanda vya uongo basi ni jua kali. Kile kiwanda mama yao na kikubwa kuliko yote cha uongo nchini si kingine bali JMK.
Chanzo; Tanzania Daima Sept. 26, 2012.

1 comment:

Anonymous said...

kikwete,lowasa, Richmond,Epa,wanyama pori,Endrew chenga, Ufisadi,List of shame,Meremeta,kagado,Kuwadi,Zaidi ya hapo hakuna hoja ni yale na yele kila siku.