How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 7 September 2012

Ni rahisi kusafirisha wanyama nje si kuingiza gari Tanzania


MZEE mwenzenu yamenikuta. Si juzi niliangiza mkangafu toka Japan ili unihudumie na si kuwakoga wanyonge na wabaya wangu kuwa nina usafiri kama wafanyavyo majuha na mafisi yenye usafiri.
Isitoshe nikiishaupata mchuma nitautumia kuhudumia walevi wenzangu na siyo kuutumia kama nyenzo ya kuopolea wake za watu na hata mabinti wa shule wanikome.
Mie siyo sawa na wale wauaji wasiojali hata kama wana miwaya lazima watumie michuma yao kuchuma wale aliopata kusema mkuu wa kijiwe kwamba wana kiherehere ndiyo maana wanapata mimba.
Mimi nataka gari kama zana ya kusafiria na si nyenzo ya kuwakoga na kuwadhalilisha wenzangu kama majuha na mafisi wengi wanavyofanya.
Kitu kimoja kimenikatisha tamaa ingawa kilinisaidia kugundua kuwa siku hizi kaya yetu ina mamlaka ya mapato yaitwayo Personal Revenue Authority (PRA) iliyochukua nafasi ya Tanzia Revenue Authority (TRA).
Kumbe sikujua kuwa maafisa (ambao kwangu nawaona mafisi) wa kodi wana mamlaka zao tofauti na ya kaya! Kila mtu anajitozolea ushuru wake na kuweka mfukoni mwake.
Anayedhani nawapakazia hawa jamaa, aangalie utajiri wao. The guys are filthy rich. Msione wezi fulani wakijidai mitaani kwa kuendesha midudu mizito aghali na kujenga mahekalu mkadhani ni wajanja. Ni wezi wa kawaida wanaowaibieni walevi kila uchao.
Hawa ni wajinga wa kawaida waliowekwa pale walipo na mfumo au jamaa zao ima kwa kuwahonga au kuwatumia kukusanya kodi na ushuru.
Msiwaone wanawakoga na vijimwana wazuri wazuri si chochote wala lolote bali wezi wa kawaida waliojificha nyuma ya utumishi. Ole wao siku zao zinahesabika.
Msione wanajenga maghorofa na kununua ardhi kila mahali mkadhani wamepata kijanja.
Hawa ni nepi za ufisadi wanaotumiwa kuhujumu na kuharibu kaya wanaopaswa kuchomwa moto kama siyo kutundikwa msalabani mchana kweupe ili liwe somo kwa wengine.
Hawa hawana tofauti na wahishimiwa waliohongwa au kuhonga kuupata uhishimiwa uwe wa kuchaguliwa au wa chupi ashakum si matusi.
Ni wezi wa kawaida wanaoitwa wahishimiwa sawa na hawa wezi wanavyoitwa wafanyakazi wakati ni majambazi wa kawaida.
Hawa ni vyangu wa kawaida wanaotumia matumbo yao kufikiri hata masaburi badala ya ubongo. Maana kwao kesho imo matumboni mwao.
Leo nina hasira ya kuweza kumtafuna mtu akiwa hai. Mie nina hasira kama yule jamaa wa Nepal aliyeng’atwa na nyoka aina ya Cobra naye akaamua kumkimbiza na kumkamata na kumng’ata hadi kufa. Nina hasira kiasi kwamba ukiniudhi naweza kujifunga mibomu na kumlipua hata kuku wako nikikukosa wewe. Nina hasara mimi kuliko magaidi wenyewe amini nawambieni.
Siku zote natamani apatikane mkuu mwenye akili na udhu afanye utaifishaji upya. Maana tuna matajiri wengi watokanao na ukupe uliolelewa na ukondoo wa walevi.
Natamani aje mtu mwenye visheni kama yangu awakamate hawa Majambazi na kuwapiga risasi hadharani bila kujali haki za binadamu.
Kwani hawa nao ni binadamu au mbwa watu? Natamani apatikane mkuu mwenye kujua anachofanya awafanyie shughuli ambayo vizazi vyote vijavyo vitasifu na kutosahau kwa ajili ya mstakabali wao.
Natamani mkuu asiyetumia masaburi kufikiri wala asiyependa sifa uchwara akifanya mambo ya kitoto wakati ni mtu mzima. Natamani mkuu mwenye kuona ufisadi akachukia hata kulia akaamua kuufutilia mbali tena kwa mkono mzito na sheria na adhabu kali hasa kifo.
Najua mkuu wa namna hii ni mmoja tu kayani yaani mzee Alhaj Profesa, Dokta, Kepteni, Field Marshal, Shehe, Mchungaji Mpayukaji Msemahovyo mjukuu wa mzee Wapashe.
Ni mimi pekee mwenye uchungu na visheni anayeweza kuwashughulikia hawa fisi watu na kuokoa kaya ambayo imewekwa reheni na mijitu vipofu ingawa ina macho.
Ni mimi pekee niwezaye kuleta maisha bora kwa watu badala ya hawa wanaoleta maisha bora kwa genge la watu tena mafisi na mafisadi na kuwaacha waliobaki waishi maisha balaa yatokanayo na maisha bora ya mafisadi.
Turejee kwa yaliyonikuta. Si niliagiza mkangafu toka Japan kwa kiasi kadhaa cha dola. Hii ni pesa yangu halali wala sikukwapua kwenye kijiwe kama jamaa wanavyokwapua kwenye kaya halafu wanakwenda kuombaomba.
Basi, baada ya mchuma kufika bandarini si wale wezi wakaanza kuchomoa spea huku wale wezi wanaojiita wafanyakazi wa mamlaka ya mapato wakitaka kunilangua eti nilipie gari langu ushuru aslimia mia.
Baada ya kuniambia upuuzi huu niliwauliza kama wale waliosafirisha wanyama hai mchana kweupe waliwatoza ushuru kiasi gani kama siyo uhuni wa kifisadi? Nilipowauliza swali hili la haja walichukia na kusema nitawatambua wao ni nani.
Bila kusita niliwapa wazi kuwa wao ni wezi na mafisadi wanaokunya kwenye ofisi zetu huku wakijiona wajanja. Niliwauliza kama na magari yao tena ya bei mbaya wanalipia ushuru. Hivi wale wachungaji wanaouuza unga na kusingizia dini nao huwa wanawatoza ushuru?
Niliwachafua nikaamua liwalo na liwe kama ikibidi mchuma wangu urejeshwe ujapani.
Nisiwachoshe na stori ya hawa nyang’au wanaopaswa kuchomwa moto siku moja. Ni kwamba niligundua kuwa kaya yetu inaliwa na wachache wasio na hata elimu ya kutosha ukiachia mbali common sense.
If I can put my two penn’orth in, how can they be truly educated and let such debauchery create debacle for just hoi polloi like you and me? Lol! Hasira nazo ni ugonjwa. Nshajisahau na kuanza kulonga Kikameruni!
Ni ajabu kuona mijitu hairidhiki na mipesa ya miunga inayohongwa kupitisha bwimbwi na magendo mengine inaanza kutuibia hata sisi wanyonge? Kama mnataka pesa kwanini hamkuwatoza pesa za kutosha waliovusha wanyama au kununua Loliondo na badala yake mnatusumbua sisi? Bahati yenu, mngemfanyia ujambazi huu wa mchana Mriiisho Gumbo asingeacha kuwaambia kuwa shahada zenu ni za chupi.
Mkiendelea na upuuzi huu nitafanya mipango na Dokta Kingwalangwala, Basha na Rege waje wawafyatue na mibastola yao. Mkizidi nitawalisiliana na Johb Ndungui na mzee wa matusi Livingjiwe Lusindwe waje wawatukane hadi mjinyotoe roho.
Mngejua washenzi hawa wakishavuta misigara yao mikubwa na kunusa mibwimbwi huwa hamnazo.
Naona Jumaa Pondaponda anapita ngoja nimuulize wanaomdhamini kupinga sensa. Kweli kaya yetu imegeuka kichwa cha Mwendawazimu.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 5, 2012.

No comments: