The Chant of Savant

Wednesday 19 September 2012

Niliyosikia, kuyaona Nairoberry yanatisha

JUZI nilikuwa na ziara ya kikazi kwa kaya ya nyayo ya akina Nyang’au wa zamani ambao wametokea kuwa wazalendo kuliko sisi ambao kijiwe chetu kimegeuka cha mafisadi.
Nilikwenda kule kushangaa shangaa barabara ya Thika ambayo kusema ukweli haina tofauti na zile nilizoona Ulaya na Amerika nilipokuwa kule kimasomo.
Wenzetu wamesonga mbele wakati sisi tunasonga nyuma kwa kasi ya ajabu. Ingawa si mshabiki wa Mzee Emilio Mwai Githinji Kibaki au Jamba ya Othaya, kwa hili nimemvulia kofia. Kumbe Kenya si mchezo! Jamaa wana barabara utadhani kwa Kameruni!
Nilitua kwenye uwanja wao wa ndege wa kimataifa wa Kamau wa Ngengi Jomo Kenyatta International Airport. Huwezi kulinganisha na wetu wa mzee Mchonga bin Mussa bin Burito International Airport.
Hata chuo chao huwezi kulinganisha na chuo chetu cha Manzese. Kama kawaida, sitataja nilioandamana nao ili nisijechafua hewa. Shosti wangu alikuwapo kushangaashangaa super highways za Nairoberry. Kama walevi wangejua shepu nilizoandamana nazo wangejinyotoa roho. Anyway mmojawapo alikuwa muuza miraa (mihadarati) aitwaye Dav Moshie.
Mwenzenu nilishangaa kuona ka nchi kasiko na rasilimali kama kaya yetu wala ardhi yenye rutuba kama yetu kufanya vitu vya nguvu kama hivi. Nikiwa kule si akina Kamau na Mureithi walicheka sana.
Nakumbuka stori ilikuwa hivi: “Mutongolya, ebu peana stori. Nasikianga kwenyu mafisi na mafisadi wana doo (pesa) kuliko gavu (Serikali). Pia nasikianga kuwa kwenye Folithi (polisi) wanaweza kushoot na kukill bila kushitakiwa wala wananchi kuandamana. Je, hii ni kweli ndugu?”
Kabla ya kujibu naye Wagacoi aliuliza swali jingine. Alisema: “Muthamaki, nasikianga eti prezzo wenu ni Vasco da Gama. Nilimuonanga juzi akiwa hapa na kibeti (mke) chake. Wamenona (kunenepa). Je, hiyo chapaa ya kutour (kufanya utalii) ni yake au ya gavu? “Pia nilisikianga kuwa wa TZ husema prezzo wetu ni guka (babu) na Lucy ni cucu (bibi), mbona na wenye nimeona kama guka sema hair yake ni black, je anaweka canta?”
Kwa ufupi ni kwamba maswali ya hawa athuri (wanaume), yaliniudhi ingawa yalibeba ukweli. Huku nikitabasamu kuficha hasira zangu nilianza kujibu moja baada ya jingine. Nilikohoa kidogo na kula miraa (mirungi) yangu na kuendelea: “Ni kweli makarau (polisi) wametokea kuwa wauaji wazuri kutokana na kutumiwa na genge fulani la majambazi wenye pawa. Lakini tuko kwenye jitihada za kukomesha mchezo huu mchafu.”
Kabla ya kuendelea, Wanyoike aliingilia: “Daddy usidanganye sisi. Kweli nyinyi mwaweza kufanya kitu zaidi ya kusemanga tafadhali karau acheni kutuua!” Alishangaa huku akicheka.
Nami kwa hasira kidogo nilimjibu: “Wanyoike mbona hunitendei haki? Kwani Kawangware, Kayole, Mukuru, Kanunga na Wanginge polisi hawaui watakavyo na hamfanyi kitu?”
Huku akionyesha kuchukia alijibu: “Kumbe wewe hujuangi sisi! Mbona tumeishadedisha karao kibao na siku hizi wameacha!”
Kabla ya kuendelea naye Mureithi aliingilia kati: “Kweli mwambie Nyoike. Huwa unasomanga Daily Neishon wewe? Somanga uone karao wanavyokukwa (kufa).”
Wakati nikitafakari hili na lile, Mwalimu Ndungu anapigilia msumari wa mwisho kwenye kujiamini kwangu, anauliza: “Nasikia kwenyu workers hawawezigoma. Sisi hapa maticha (walimu) na madokii (Madaktari) wamegoma hadi kimeumana na gavu. Nasikia kwenyu madokii walijaribu mdingi wao akakamatwa na kupigwa na kutoroka mgomo si ule anaitwa Walimboka?”
Kwa ukali nilisema: “Jamani imetosha. Yaani nyie mwatuona sisi twacheza mihigulo (kukata mauno) kwa kila kitu badala ya kujipigania?”
Kabla ya kuendelea, Muiruri alijibu: “Nyie mkicheza mwihigulo au mwomboka si mubaya. Yote ni muziki ya Kenya. Also sisi sasa ni citizens wa East African Community. Lazima muziki ya Kenya iwike. Maana ile ya TZ naonanga kwenye TV imejaa noises na vijana waliobomoa ears zao na kuvaa sag. Hapa Kenya sag haiko ruhusa au kutangaza condom kwa TV na barabarani.
“Looo! Nilipokwenda TZ kule Dasalaamu niliona adverts mingi ya sex nikaogopa. Je, hii haiharibu watoto yenyu? Pia nilisikia waTZ wakilalamika eti wadosi wengi kwenye gavu wameficha doo nyingi nje kama kwetu, lakini they are sleeping without any worries.
“Wajamaa, kwanini mnakuwa so mean? Yote mmesema kwanini hamchaganyi na nyigine zuri kama vile Tanzanite ambayo inaleta chapaa mingi kwa Kenya? Kwanini hamuogelei mchele tunayokula na fruits toka TZ?”
Baada ya kuona hawa jamaa wamezidi kiherehere kama vitoto vya shule za msingi alizosema rais kuwa vinapata mimba kutokana na kiherehere niliamua kuwatolea uvivu. Nilianza kumwaga mawe: “Atongolya, hebu tujaribu kuangalia mambo kwa macho bila makengeza ya kujipendelea hadi kutetea upuuzi.
“Mbona nyinyi hamna ardhi kiasi cha kukosa hata vyoo sisemi? Au hizi flying toilets (kinyesi kinachotupwa kwenye mifuko ya rambo) mnadhani sizioni kila sehemu kwenye slums?”
Najaribu kuwakazia macho na kugundua kuwa kila mtu alikuwa amepigwa na taharuki ya kufa mtu. Kuona hivyo niliendelea: “Mbona mimi sijagusia maisha yenu ya kuishi kwenye majumba ya mabati kama magari na ng’ombe? Au mnadhani kuwa sijui kuwa viongozi wenu waliiba ardhi wakati kwetu waliiba fedha? Mbona akina U-independence Muigai Kenyat na akina Daniel arap Mwai wana mamilioni ya heka wakati nyinyi hamna hata pa kukanyaga? Hamuoni watasha walivyo na mamilioni ya heka wakati nyinyi mnaishi kama ndege kwenye mti kwenye nchi yenu?”
Nilitema mabaki ya miraa na kuendelea: “Hebu tujaribu kuheshimiana badala ya kuchongoana.”
Inaonekana ukali wangu ulifanya kazi maana Kinyua hatimaye aliniunga mkono na kusema: “Kweli jamba unayosema imenigusa sana. Kwa watu maskini twapaswa kushikana na ku-fight impunity kwenye nchini zetu. Hapa Kenya iko wakora sawa na TZ.
“Hapa tuna Goldenberg na Anglo-Leasing na TZ wana EPA na Richmod.” Alinigeukia kuuliza kama amepatia, alisema: “Hii Richmod nasikia imeleta shida mingi hasa power rationing na pia EPA nasikia ilifanywa na watu iliyokuwa iki-vie kwenda state house.”
Wakati nikijiandaa kuchangia zaidi niligundua kuwa kumbe nilikuwa nakaribia kuchelewa pipa!
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 19, 2012.

No comments: