Wednesday, 26 September 2012

Daraja la Kigamboni: Barua kwa Joni Bia Makufuri

 
Bwana Joni Kanywaji Makufuri,
Kwa heshima na taadhima napenda nikusalimie na kukutakia afya njema wakati nikiandika yafuatayo kama nilivyoelezwa.
Kwa ufupi hii ni injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Mpayukaji Msemahovyo, mtume kwa walevi wote.
Hii mhishimiwa ni fursa ambayo hutaisahau maishani mwako kupata kuandikiwa waraka na mtume kama mimi.
Mimi ni tofauti na matapeli wanaojiita mitume na wachungaji wakati ni matapeli wa kawaida wanaowachuna watu kwa kutumia majoho na jina la Mungu.
Mimi ni tofauti na akina Ka-Tortoise, Rwakatarehe, Gamanyua, Mwakasenge, Lushekelo au Muzee wa Upakazio na matepeli wengine wengi waliojivika majoho wakati ni wezi wa kawaida.
Kijiwe kimeniagiza nikuandikie waraka huu kuelezea msimamo wao baada ya kuona walevi na Wadanganyika wakikenua njino walipomuona mkuu akizindua ujenzi wa daraja la kisasa na kisasi la Kigamboni. Wanakijiwe hawakuwa na furaha. Mwanzoni niliwashangaa nisijue nao walikuwa wakinishangaa!
Baada ya Dk. Msomi Mkatatamaa kunielimisha niligundua ni kwanini. Kuna madai kuwa kuna wahuni wanataka kutoza nauli ya kuvuka daraja hilo kwa vile wamelijenga. Kijiwe kinasema nasi tuwatoze kodi kwa kujenga kwenye ardhi na bahari yetu.
Wanakijiwe wana wasiwasi kuwa kama daraja litajengwa na makampuni yaliyopata tenda kupitia sayansi ya Ten percent basi litabomoka na kuangamiza maisha ya walevi wengi. Mie na bi mkubwa tunaogopa sana samaki. Kwani kwa mamia ya miaka, kama mkuu, tumekuwa na mapenzi makubwa ya kuwala.
Hivyo, tunahofia kuwa ufisadi wa ten percent unaweza kuwapa fish nafasi ya kutupenda kwa kutugeuza kitoweo kama ambayo maisha yetu yote tumewageuza.
Baada ya kutumia madaraka yangu kijiweni kumwezesha bi mkubwa kufungua NGO ambayo ilimuingiza pesa, tulifanikiwa kununua uwanja kule Kigamboni hasa baada ya kusikia kuwa kuna mpango wa kujenga daraja.
Hatukuwa tumeona mbali kama walevi. Pia tuna bahati kuwa uwanja wetu haukukumbwa na sekeseke la kupisha daraja na wajanja fulani kuutumia kujilipa fidia badala ya sisi.
Mwanzoni wasiwasi huu ulipoonyeshwa kwangu niliwaona walevi kama manazi wasiopenda hata kukubali kuwa haya ni maendeleo. Walinipa mifano ya barabara nyingi zilizojengwa ndani ya wiki na kuharibika ndani ya masaa kaya nzima.
Pia walikuwa na shaka na hili la kutozwa nauli. Walisema kuwa mbona kwenye daraja la Jangwani na mengine mengi hawatozwi ushuru wala nauli. Kwani daraja ni treni au basi au ndege? Je, daraja linatuma mafuta au umeme? Je, ni lini walevi watalitumia free wakati kaya na ardhi vyao vinatumika free?
Ingawa walevi ni walevi, wana hoja. Walisema kuwa wakikumbuka jinsi EPA ilivyoleta uchakachuaji wanakosa imani na binadamu ngurumbili.
Pia walitoa mfano wa Richmond ambapo mkuu na Ewassa waliahidi kuwa mgawo wa umeme ungekuwa historia na badala yake ikawa kinyume. Sana sana faida ya mgawo ni kutengeneza na kutotoa vitegemezi vingi ambavyo walevi hawawezi kuvimudu na mstakabali wao unazidi kubomolewa.
Mie nashukuru Mungu bi mkubwa alikubali ushauri wangu wa kuweka kakomeo ili asivitotoe vikatunyotoa roho maana ukiona hizo shule za kata na matuisheni ya wezi wanaoitwa walimu utaogopa. Jamani mtoto asipokwenda tuisheni siku mbili maksi zinashuka kama ndege ilizomika! Mwe! Tunakwenda wapi?
Sasa daraja likijengwa na watu wenye akili na roho za kituisheni si litaua hata kabla ya mwaka? Lazima tuseme kuwa daraja lisijengwe kivoda fasta ili kunusuru maisha ya walevi wetu wapenda amani na mshikamano hata kama havipo kivitendo bali kinadharia.
Wana Kijiwe siku zote ni mabingwa wa hoja kutokana na wote kuwa madaktari tena wa kusomea na si heshima kughushi wala kugawiwa kishikaji.
Walitoa pia mfano wa maisha bora kwa walevi wote ambayo yameishia kuwa maisha balaa kwao huku yakiwa bora kwa nyumba ntobhu. Hivyo siandiki kwa hiari yangu wala ushabiki bali kuwasilisha kilio cha walevi ili kikufikie nawe ukifikishe kunakohusika.
Kitu kingine walichoniambia walevi tena chenye kusikitisha ni wasiwasi wao kuhusiana na Eniesiesiefu (ENSSF) inayojenga hilo daraja. Tulikusikia ukisema kuwa mkurugenzi wake Juma Kidau apewe nishani badala ya wanagesi. Hayo ni yenu mtajuana. Mnaweza kupeana nishani hata za ufisadi na usanii. Walitaka kujua ni kwanini haina huruma na wachangiaji na inawekeza njuluku yao kwenye biashara wakati watoa michango wakiendelea kusota na hakuna anayejali?
Kusema ukweli nilishindwa kuwajibu kwa vile mie si mwajiriwa wa lisirikali na Eniesiesiefu wenye maulaji yao.
Kwanza, walevi walitaka wapewe hakikisho kuwa hakutakuwa na rushwa ya kuweza kusababisha daraja lijengwe chini ya kiwango na kuua walevi wasio na hatia kama ambavyo imewahi kutokea kwenye kashfa ya MV Bukoba na lile jahazi lililoua watu hivi karibuni kule Zenji.
Tukizingatia matukio hayo hapo juu ambayo yaliacha misiba mikubwa kwa walevi, kama thinkers of our own light and time, we need assurance from you by getting it from the mounth of the horse. Mark my words; I am not saying you are a horse neither are we. Again, we need convincing explanations befitting thinkers not horses like your cheerleaders and major domos.
Samahani mhishimiwa, huwa nina ka-ugonjwa ka kupandisha mwenembago ambapo hujikuta nikibwabwaja kikameruni ambacho naamini unakijua kutokana na kuwa daktari kama mimi. Najua udaktari wako siyo wa kupewa wala kughushi. Hivyo nisamehe. Naamini umenielewa bwana Kanywaji.
Tena kabla ya kusahau, napenda nichukue fursa hii kukwambia kuwa Kijiwe kimenituma nikwambie umwambie bosi wako aache matusi ya rejareja kama alilotoa juzi kuwa wapingaji wana viwanda vya kuunda uongo wakati mwanzilishi ni yeye.
Kusema ukweli mimi na wana Kijiwe hatukupenda haya matusi ya nguoni ikizingatiwa kuwa nasi ni wapinzani wanaopinga ulegelege na uholela wa lisirikali la jamaa yako.
Acha niwahi Brela kuona orodha ya makampuni yaliyopata tenda ya kujenga daraja na mbinu waliyotumia kupata ulaji huu.
Bwana Kanywaji, mfikishie salamu zake ndugu yetu, mpendwa wetu, kipenzi cha wengi na chaguo la God, Dk. Njaa Kaya.
Chanzo: Tanzania Daima Sept. 26,2012.

No comments: