Hivi
karibuni, akizindua mradi wa ujenziw a daraja la Kigamboni jijini Dar
es Salaam, rais Jakaya Kikwete alikaririwa akisema kuwa wapinzani wana
viwanda vya uongo. Aliwanasihi bila kujinajisi, waache kusema uongo;
wamsifie hata kama hawaoni sababu ya kufanya hivyo. Kwa wengi, maneno ya
Kikwete yalikuwa kama harakati za mfa maji baada ya kuona mambo
hayaendi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa Kikwete hajakidhi matarajio ya
watanzania. Nikiri; ilikuwa ni mara ya kwanza kwangu kusikia kuwa kumbe kuna viwanda vya uongo. Mwanzoni nilidhani nilikuwa nimesoma vibaya. Nilidhani alimaanisha viwanda vya gongo. Kumbe rais alimaanisha viwanda vya uongo! Kwa hadhi na nafasi ya rais, kwanza, lugha aliyotumia ni ya
matusi ukiachia mbali kusahau kuwa aliyeanzisha “viwanda” hiyo vya uongo hata kabla ya wapinzani ni yeye na chama chake.
Alikaririwa
akisema, “Watu wana uongo mwingi eti nimeuza eneo kwa Bush, huo ni
upotoshaji mwingi. Maana kuna watu kila kukicha wana viwanda vya
kutengeneza uongo. Wako ambao hawapendi maendeleo,”
Kuuza
nchi si lazima auziwe George Bush. Je ni wawekezaji wangapi wanafanya
mambo kama vile wamenunua Tanzania wakiwamo Dowans waliotokana na
kampuni iliyoingizwa nchini kinyemela na Kikwete na Lowassa ya Richmond?
Je ni matapeli wangapi wanaitwa wawekezaji wakati ni waganga njaa na
makuadi wa wakubwa wenye madaraka wasio na uzalendo wala udhu wa kuwa
hapo walipo? Hapa rais anataka kumdanganya na kumfanya nani mpumbavu
asiyeona yanayoendelea?
Tofauti
na wapinzani ni kwamba huyu mwanzilishi wa “viwanda” vya uongo ni
mwepesi wa kusahau ukiachia mbali kupenda kujisahaulisha na kujifanya
hajui kinachoendelea. Hivi kweli Tanzania kuna kiwanda cha uongo chenye
ukubwa na hatari kuliko kile kiitwacho Jakaya Mrisho Kikwete aka Kipenzi
cha watu? Kuna kiwanda cha uongo kama “Tumaini lililopotea?”
Hebu
tumpe ushahidi ili angalau imsaidie mheshimiwa huu kuamua nani mwenye
kiwanda au viwanda vya uongo. Mwaka 2005 akiwa mgombea wa CCM aliwaahidi
watanzania maisha bora chini ya kauli mbiu ya Maisha bora kwa wote. Je
Kama rais hakuongopa, anaweza kuonyesha nini zaidi ya kulalamika
kuhusiana na maisha bora kwa watanzania? Tofauti na alivyoahidi, rais
ameletea maisha balaa kwa watanzania kutokana na kudaiwa kuwa alipata
ushindi na kuwa rais kupitia pesa chafu ya iliyotokana na ufisadi wa EPA
ambayo hajawahi kukanusha wala kutolea maelezo.
Kikwete
aliahidi kutaja mali zake na mkewe. Hili huwa hapendi kulisikia achia
mbali kutoa maelezo au kuzitaja hizo mali. Je anaogopa nini? Je kwa
kutotaja mali wakati alipaswa kufanya hivyo na akaahidi kufanya hivyo si
uongo? Nilishaliandikia zaidi ya mara saba lakini rais hajawahi kutaka
hata kuligusia. Hata watu wake wa usalama huwa wanahofia hata kupiga
mkwara kwa gazeti kwa kuhofia mengi yataibuka kuhusiana na usafi wake
binafsi.
Turejee kwenye “viwanda” vya uongo. Kikwete aliongeza na kusema, “Hili
daraja na barabara ambazo nasimamia vitabeba watu wa vyama vyote CCM,
CUF, CHADEMA, TLP na wasio na vyama na wasiposhukuru au wakishukuru
shauri yao lakini maendeleo yanafanyika na watu wanaona hata kama
wanajifanya hawaoni,.”
Hii
ni kauli ya ajabu inayoonyesha uwezo ima uwezo mdogo wa msemaji kuelewa
mambo au kuamua kuongopa kusudi. Kwani ni wapinzani gani waliwahi kudai
kuwa daraja na barabara vitatumiwa na wana CCM tu? Je kusema kuwa
wapinzani wanaangalia miradi ya kitaifa kama mali ya chama si kuzua hata
kuongopa? Wapinzani hawana ugomvi na kuanzishwa kwa miradi ilmradi
wapate maelezo ya kina jinsi pesa ya walipa kodi inavyotumika. Na
isitoshe, Kikwete na chama chake hawajengi hivyo vitu kama hisani au
msaada kwa watanzania. Wala hawajengi kwa pesa yao. Ni kazi ya serikali
kufanya vitu hivyo kutokana na ukweli kuwa wananchi wanalipa kodi.
Kinachogomba kwanza ni umadhubuti au uwezo wa kufikia viwango
vinavyokubalika na gharama za miradi hiyo. ni ajabu kwa Kikwete kudhani
kuwa watanzania wengi walio makini
wanajiuliza swali moja kuu: Kama daraja la Kigamboni litajengwa hovyo
hovyo kama barabara zetu kutokana na tenda kupatikana kwa kutumia ten
percent, siku moja litaua wangapi? Huu ndiyo wasi wasi wa watu wenye
kufikiri sawa sawa wanaojua jinsi serikali ya Kikwete inavyoendeshwa.
Muulize
Kikwete kama anakumbuka alivyowahi kutamba tena hadharani kuwa ana
orodha za wezi bandarini, majambazi na wauza mihadarati. Kama anakumbuka
muulize tena, aliwafanya nini kama kweli alikuwa ana orodha yao zaidi
ya kunogesha stori. je kama kweli anazo orodha za wahusika na vyombo vya
dola vya kuwashughulikia, ana maslahi gani au ameshindwa nini
kuwashughulikia? Je kuendelea kutowashughulikia wakati aliahidi
kuwashughulikia si uongo tosha? Ukimuuliza
hili naamini hatakuwa na la kukwambia zaidi ya kukuweka kwenye kundi la
watu wasiopenda maendeleo yake. amini maneno yangu. Hata baada ya watu
wake kusoma makala hii, hawatajibu kwa kujua fika watakuwa wanamvua nguo
mtu wao anayewatuhumu wapinzani kufanya kile ambacho kimemweka
madarakani. Ni mtu wa namna hiyo na kwa kiasi fulani watanzania wameishamzoea wakiomba Mungu muda wake uishe ajiondokee.
Kikwete
kama rais aliapa kulinda wananchi na raslimali zao. Muulize hili
amelifanyaje iwapo wanyama wetu wanatoroshwa huku serikali yake ikiwa
inasema eti haina habari. Wananchi wanauawa na polisi kwa maagizo ya
Kikwete kupitia wateule wake na usalama nchini umekuwa tatizo. Je
wapinzani wakisema kuwa Kikwete aliwaongopea watanzania kuwa atawalinda
wakati hafanyi hivyo ni kuchukia maendeleo au kuunda viwanda vya uongo?
kama hivi ndivyo viwanda anavyoongelea Kikwete, tofauti na chake, ni
viwanda vizuri maana hii ndiyo kazi ya upinzani-kumkosoa na kumshauri
wanapohisi anakwenda ndivyo sivyo. Kikwete
aliahidi angefuata sheria za nchi na kuzitekeleza bila ubaguzi. Katika
hili amenoa karibu kila eneo. Kuna watu kama rafiki zake na washirika
zake kama Edward Lowassa na Andrew Chenge wako juu ya
sheria. Pamoja na wengine kukiri na wengine
kuletewa ushahidi wa kutosha wa kushiriki wizi na ufisadi, bado Kikwete
anasema ni wachapa kazi bora hakuna mfano. Hivi kuna kiwanda cha uongo
kama hiki. Leo nimeongelea uchache tu juu ya products za kiwanda cha
uongo cha Jakaya Kikwete. Kwa ufupi ni kwamba kama wapinzani wana
viwanda vya uongo basi ni jua kali. Kile kiwanda mama yao na kikubwa
kuliko yote cha uongo nchini si kingine bali JMK.
Chanzo; Tanzania Daima Sept. 26, 2012.
1 comment:
kikwete,lowasa, Richmond,Epa,wanyama pori,Endrew chenga, Ufisadi,List of shame,Meremeta,kagado,Kuwadi,Zaidi ya hapo hakuna hoja ni yale na yele kila siku.
Post a Comment