Si uchochezi kusema kuwa watawala wetu wameshindwa, tena vibaya sana. Ni aibu kwa taifa ambalo limesherehekea miaka 53 ya uhuru kushindwa kufanya maamuzi magumu hadi lishinikizwe na wafadhili. Tishio na amri ya hivi karibuni toka kwa serikali ya Marekani kwa Tanzania kuwa haitatoa fedha za Changamoto za Milenia (MCC) kama serikali haitawachukulia hatua watuhumiwa wa kashfa ya uchotaji wa mabilioni ya fedha za umma, escrow ni somo tosha.
Heri wafadhili wamenena. Hili ni pigo na aibu kwa rais Jakaya Kikwete, serikali na CCM ambao wamekuwa wakiwahadaa watanzania kuwa wako madarakani kwa maslahi yao wakati hali ni tofauti. Huu ni ushahidi kuwa CCM na serikali yake wamewekwa mfukoni na mafisadi. Hali ikiendelea hivi, watawala wetu wataipeleka nchi kubaya. Huu ni ushahidi tosha kuwa utawala wa sasa umechoka, upumzishwe ili wenye uwezo watawale na kusafisha uchafu uliopo. Inakuwaje wananchi wanashindwa kuona haya na kuiwajibisha vilivyo CCM kwa kuishikisha adabu?
Ni ajabu kwa nchi inayojidai kuwa na utawala wa sheria lakini ikawekwa mifukono mwa matapeli wachache, wasaka tonge na wahalifu wa kawaida. Ziko wapi tambo za kupambana na biashara ya madawa ya kulevya? Nani anawagusa? Je hawa hawana ubia kwenye serikali ya sasa? Je hawa hawajaiweka serikali mfukoni? Asitokee mtu akaniambia kuwa hawajulikani. Mbona rais alishakiri kupewa orodha ya wauza unga asiifanyie kazi kwa sababu ajuazo? Je inakuwaje tunashindwa kupambana na ufisadi ilhali tukijua kuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya taifa? Je ni kwa vile mafisadi ni washirika wa nyuma ya pazia ya watawala wetu?
Najua wengi wanaweza kusema tunaizushia serikali. Kama watachunguza sababu za serikali kuruhusu ufisadi kuwa sehemu ya maisha ya serikali yetu, wataelewa tunachosema. Hivi kweli nchi inayoamriwa na wafadhili la kufanya ni huru? Je kwa uzembe na upofu wetu tunapaswa kuwalaumu wafadhili kwa kuingilia mambo yetu? Watashindwaje kuingilia iwapo tunafanya mambo ya kitoto na ya hovyo? Imefikia mahali hata bunge linatoa maagizo halafu wakubwa wanayadharau na kuja na mambo yasiyo ingia kichwani kama ilivyotokea juzi wakati Ikulu iliposema kuwa haitawawajibisha watuhumiwa wa wizi wa escrow wala kuchukua hatua hadi ifanye uchunguzi wake. Tambo za ikulu zimeishia wapi baada ya kubanwa? Ndani ya wiki moja ikulu, ikiwa imechanganyikiwa na kujichanganya ilitoa tamko jingine la kijichanganya zaidi ikisema kuwa rais atawashughulikia watuhumiwa ndani ya wiki moja. Hii maana yake ni kwamba ikulu imeminywa na kufanya kile ambacho haikutaka kufanya. Maana ukiangalia timing ya tamko la Marekani na mkengeuko wa Ikulu unagundua kuwa hata kama rais atawawajibisha wahusika si kwa kutaka bali kulazimishwa na wafadhili. Je rais au chama kinachounda serikali vya namna hii bado vinawafaa watanzania? Je ni vibaya kusema kuwa rais amegeuka mhimili wa ufisadi anaopaswa kuuchikia na kupamba nao? Je ni kwanini inakuwa hivi kama rais hanufaiki na jinai hii au kuishiriki?
Ushahidi wa kimazingira unaonyesha wazi kuwa, kama si papara za bunge, au tuseme kuwekwa sawa na kuingia mkenge, lilipaswa kuiwajibisha serikali yote. Kwa vile inaonyesha escrow ni dili lao. Haiwezekani mawaziri tena waandamizi na maafisa wengi wa serikali waruhusu wizi wa mabilioni hivi kusiwe na mkono wa wakubwa zao. Nani anakanusha kutajwa kwa afisa wa ikulu Prosper Mbena anayedaiwa na kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa aliandika barua ya kushinikiza pesa zichotwe? Je hapa tunatafuta ushahidi upi wa kuihusisha ikulu? Ushahidi mwingine ni ukimya wa muda mrefu wa serikali. Hata kitendo cha rais kusuasua hadi alazimishwe na wafadhili kuchukua hatua ni ushahidi tosha ukiachia mbali rais kuhusishwa moja kwa moja na uletaji wa kampuni jizi ya IPTL hapo mwaka 2004.
Laiti wafadhili wangekwenda mbele zaidi na kuhakikisha hili jinni linalotunyonya damu IPTL linafurushwa na wahusika kufungwa, wangekuwa wametukomboa hata kama wakubwa watalalamika kuwa wanaingiliwa. Kwanini wasiingiliwe iwapo wamejirahisi kiasi cha kuacha mafisadi wajifanyie watakavyo? Kwanini wasiingiliwe iwapo wameonyesha wazi walivyo wa hovyo na fisadi? Nani angeweza kumwamrisha baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere katika lolote? Je ilikuwaje Nyerere akaogopewa na kutopewa amri? Jibu ni rahisi. Alikuwa msafi na mwenye visheni tofauti na hawa walioigeuza ikulu deni la wezi kama alivyowahi kuonya Nyerere huku akiwakataa wengi wa tunaowaona leo madarakani wakiyafuja ili kutimiza utabiri na madai ya nguli huyu (Mungu amlaze pahali pema peponi). Rais anayeamrishwa kufanya alichoapa kufanya amebaki na nini? Je nafsi zo zinawasuta? Je sisi tunawasuta na kuwawajibisha au kuendelea kuwagwaya?
Tumalizie kwa kuwataka watanzania kutorudia makosa. Kwenye uchaguzi ujao licha ya kuhoji ni kwanini ufisadi uliachiwa kuwa sehemu ya utawala wasiangalie sura wala ukongwe wa chama. Wahakikishe wanajipatia serikali safi, mpya, yenye mapya na si huu wendawazimu wa siku zetu. Maana waingereza husema “insanity is doing the same thing over and over again and expecting different results.” Tuachane na wendawazimu huku tukijitofautisha na mafisadi ili mataifa mengine yasiendelee kutucheka kwa kuruhusu taifa letu kuwa shamba la bibi tena bibi mwenyewe hamnazo. Imetosha, wananchi wanapaswa kuanza kwajibika kwa kuwawajibishwa watawala fisadi na wachovu na wabovu.
Chanzo: Tanzania Daima leo.
6 comments:
Kwanza Samahani Mhango, sisi tunamfumo wetu wa utawala unaitwa sirikali siyo hiyo unayofikiri wewe serikali. Wewe haufahamu hatua za maendeleo ya sirikali yetu
Pili kimsingi sisi hatulazimishwi na taasisi au serikali yoyote duniani kufanya maamuzi kwa maslahi yetu.
Tatu utafiti tunaofanya sasa tutatumia watalaamu wetu kutoka peponi na kalumanzira ili kuwaletea majibu shetani wetu atakapojalia.
Nne katika kundi ketu la sirikali mtu ambaye siyo Kundi letu tumekwisha muondoa kwa kumfukuza madarakni tena bila shukurani.
Tano Jamaa zetu wa kundi letu tumekubaliana umma nchi za magharibi waikutishika kooni basi tunawashauri kujiuuzulu au kuwasimamisha tunawapatia mafao yao yote na kuwateua vyeo vingine pia, tunatoa shukurani kwa utendaji wao mzuri uliyotukuka kudumisha sirikali yetu.
Nategemea Mhango utakuwa umetuleewa na pia hii ni zawadi yako krismasi na heri ya mwaka mpya. Shetani wetu akubariki kwa mwaka ujayo.
Maana tutawekeza juhudi zetu katika kupata viungo vingi kutoka Zaruzaru kama mahitaji yetu kutoka kamati zetu karumanzira inavyosema ili tushinde uchaguzi katika sirikali yetu.
Mimi sijui ni kitu gani Amerika kilichomfanya kimuume sana mpaka kumuwekea mikwara kibaraka wao kiketwe kwamba watamnyima misaada.Tanzazia imekuwa ni ajent wa Marekani tangu utawala wa Mwinyi hadi huyu brother man kikwete.Ni amri nyingi tu ambazo serikali ya Marekani inazitoa kwa serikali ya CCM nyuma ya pazia na nyingine hadharani na kutekelezwa dhidi ya nchi,masilahi na ya wananchi wa Tanzania na hii leo FBI,CIA na MOSSAD zinafanya shughuli zao Tanzania kwa wepesi mno kwa hoja ya kupambana na ugaidi wa kimataifa.
Mwalimu Mhango usijipe matumaini sana kwa serikali ya marekani kupigia makelele au kuingilia kati ufisadi wa nchi yetu uliojipalia mizizi na magugu yasiyolimika ni mchezo tu wa kisiasa na kutuziba macho sisi watanzania kuona kwamba marekani inajali wananchi wa Tanzania.Rekodi ya marekani ipo wazi wala haitaji mjadala kwa kuwaunga mkono madikiteta vibaraka popte pale walipo muda wa kudumu tu watayatetea masilahi ya Amerika.Unakumka Mwalimu Mhango msaada wa mabilioni ya madola ambayo Misri ilikuwa inapewa tangu utawala wa Sadat hadi wa Mubaraka?Je marikani ilikua inajali kutenguliwa haki za kibinadamu,mateso na mauaji yaliokuwa yanafanyika tangu Sadati hadi Mubaraka?Je hawajaitwa madikiteta Museveni na Kagame kwamba ni DARLING wa Mgharibi?
Kwa uvundo ulikuwepo wa ufisadi Tanzania je serikali ya marekani inaweza kuiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi yetu mapka watawala wa CCM waipende nchi yao na wananchi wake?unaweza kusema kwamba kuiwekea Tanzania vikwazo vya kiuchumi kutawathiri wananchi zaidi kuliko viongozi wa CCM,je Marekani inaweza kuwawekea vikwazo viongozi wa CCM na watoto wao na waramba viatu vyao wasikanyage Marekani au EU kama walivyomfanyia Mugabe?jawabu kwa maoni yangu hapna serikali ya Marekani haiwezi kufanya hivyo na haitofanya hivyo kwani wao kupitia makampuni yao ambayo mengine hata wananchi wa tanzania hatuyajui yanashiriki vyema kutuibia kwa hoja ya uwekezaji na kuukomaza utaratibu wa kiuchumi wa kirebelari.
Mwalimu Mhango,kama kweli tunataka mabadiliko ya nchi yetu na kuitoa CCM madarakani yaanze kwetu sisi wenyewe wadanganyika kama unavyotuita,ni miaka 53 ya uhuru wa nchi yetu na kwa maana mwananchi aliezaliwa wakati nchi yetu inapata uhuru ameshaingia katika umri wa uzeeni na tuulizane je wengi wa wananchi hawa wamefaidika nini ni awamu hizi tatu tukiondoa awamu ya Mwalimu Nyerere?Jawabu ni kapa,leo hii ni viongozi na watoto wao na waramba viatu vyao ndio wanaofaidika na nchi na kuifanya nchi ni shamba la bibi.Sisi wadanganyika hatuna ubavu wa kufanya mabadiliko kama yaliyotokea mashariki ya kati na hata ya karibuni huko Burkina Faso na sababu ya kimsingi kwamba Jeshi letu si kulinda mipaka yetu na wananchi kama lilivyotakiwa liwe bali ni jeshi la kuilinda serikali ya CCM na viongozi wake.Lakini mabadiliko yawe kwa kwa wadanganyika wenyewe kwa kusema kwamba TOSHA!Kudanganywa kwa muda mfupi unaweza kuzielewa sababu zake za kimsini na kujishitukia kwamba nimedanganywa,lakini kuendelea kudanganywa milele kosa sio la mdanganyaji bali kosa kubwa na lisolosameheka ni la mdanganywaji.
Mwalimu Mhango,umekuwa mwenye kukemea sana kuhusu biashara ya madawa ya kulevya nchini mwetu na kuuelezea utaraibu wa ambao kwa karibu au kwa mbali jinsi gani baadhi ya majina makubwa na madogo yanajulikana mbele ya Rais wetu na hadi hii leo hakuna hatua yoyote ile aliyochukua na atakayochukua.Ukweli uliopo wazi Mwalimu Mhango wafanya biashara wa madawa ya kulevya wakubwa wakubwa katika ulimwengu wa tati ikiwemo Tanzania ni lazima waitie serikali mfukoni mwao na hata kuna ushawishi ambao mwafanya biashara hawa wakubwa kuwashawishi baadhi ya vingozi kushirikiana nao katika biashara hiyo na hatimaye ndiyo hali ambayo tuliyokuwa nayo nchini mwetu majina yanajulikana lakini ni nani mwenye ushjaa wa kuyataja iwapo baadhi ya viongozi wenyewe wanashiriki.
Mwalimu Mhango,huo wote ulikua ni utangulizi tu ninalotaka kuliongea hapa ni kwamba kuna vijana wetu ambao sio watoto wa wakubwa(vigogo)ambao kwa kukosekana ajira nchini mwetu au kwa mvutio wa biashara hii ya madawa ya kulevya ya kupata utajiri kwa kufumba na kufumbua aidha wanakuwa wanatumiwa na wafanya biashara wakubwa au hata wadogo na lakini wengi wao huwa wanaishia majela katika nchi mbali mbali aidha kama ni masoko au mashamba.Vijana sehemu nyingi huwa wanatumikia muda wao wa kifungo na kuachwa huru,lakini Mwalimu Muhango,kuna hii kesi ya baadhi ya vijana ambao wamekuwepo katika baadhi ya majela nchini Irani,na imetokea kwamba muda wao wa kutumikia hukumu yao umekwisha na serikali ya Irani inaitaka serikali ya Tanzania kuwatambua raia zake hao na kuwatafutia ufumbuzi wa kuwarudisha Tanzania,lakini jibu la serikali ya Tanzania(wizara ya mambo ya nchi ya nje)kwamba haiwatambui wala kuwasaidia watanzanzia ambao wamekutwa na hatia ya madawa ya kulevya na hatimae vijana hao wamebaki katika baadhi ya jela hizo nchini Irani bila ya kujulikana hatima yao itakuwaje,na balozi wetu nchini Saudi Arabia ambae analinda masilahi ya Tanzania nchi Irani ameshawatembelea mara kadhaa amewaambia kwamba yeye hana uwezo wa kuiwekea presha serikali yake.
Swali langu Mwalimu Mhango ni hili Je hivi mtanzania ambaye amekamatwa nje ya nchi kwa kosa la dawa ya kulevya anakuwa anavuliwa uraia kiasi ambacho serikali yake haimtambui?Je mtanzania huyu kweli amekuwa ni mkosa mkubwa sana kuliko wale wafame wa biashara za kulevya ambao wnaozifanya ndani ya nchi yetu na wakawa wanapeta kama wendawazimu?Je vijana kama hawa kesho unaweza kuwalaumu wanpoichukia serikali ya nchi yao na hata kukosa uzalendo?Ni wazi kabisa na hili linajulikana kwa vile serikali yetu si tajiri kuweza kupeleka ndege ya kuwachukua vijana hao au hata kuwagharamikia tiketi zao lakini kutowatambua kama ni watanzania kwa vile kosa lao ni kushiriki katika biashara ya madawa ya kulevya,Mwalimu Mhango ili nimeshindwa kulielewa kabisa.Inawezekana ukawa na muona tofauti katika jambo hili lakini ninachopigia makelele mimi ni kwa mtanzania kutotambuliwa kama ni mtanzania na kukosa msaada wa aina yoyote ile mua wa kudumu amepatikana na hatia ya biashara ya madawa ya kulevya nje ya nchi.
Anon wa pili hapo, kuna zawadi x-mas na mwaka mpya amepatiwa Mhango kutoka kwa anon wa kwanza hapo. Reje kipengele cha pili kwamba sirikali inatekeleza ajenda kwa ajili yao binafsi siyo raia wake.
Hivyo kuzungumzia kushughulikia watu ambao hawapo katika vipaumbele vyao ni kukiuka sirikali manefesto kwa kutetea watu walionje ya malengo ya sirikali iliyopo madarakani.
Nategemea utakuwa umelewa sababu za msingi kwenye suala, kumbuka hata wakati kuwasilisha sababu za raia wa nchi hiyo kuwa na uraia zaidi ya mmoja sirikali ilishasema kuwa, hao raia wa namna hiyo ni hatari kwa usalama wa sirikali.
Zawadi ya xmas aliotumiwa mwalimu Mhango nimeilewa vyema kama mwandishi alivyotaka kuifikisha lakini hii haina maana kwamba maandishi hayo ni ukweli mtupu au ukweli wote katika yaliyoandikwa,na kwamba sisi wadanganyika ndivyo tunatakiwa kuamini hivyo.Endapo mwandishi wa zawadi ya x-mas anakusudia kwamba serikali ya Tanzania inaongozwa na aina ya Jamii ya Siri(secret society) na ndio maana akaiita sirikali ingekuwa vyema zaidi atuelimishe Manifesto yao ili sisi wananchi wadanganyika tuelewe kwa undani kabisa kwamba serikali yetu inaongozwa na kikundi cha watu ambao hawana mapenzi ya nchi na wananchi wao isipokua ni kutetea masilahi yao binafsi na kutekeleza ajenda zao za siri.
Nilivyomuelewa mwandishi wa zawadi hiyo ya x-mas ni kutufikishia sisi wadanganyika kwa muono wa kuikebehi serikali yetu na kutoa machungu yake kwa upande mwingine kutokana na ufisadi,wizi,ujambazi na urithishaji wa madaraka kwa vizazi vyao tangu kuanzia awamu ya pili hadi hii tuliyokuwa nayo.
wache nikubaliane nawe kwa hoja ya mjadala kuhusu kukubalina kwako na zawadi hiyo ya x-mas kwamba kuna ukweli kama ulivyouona wewe,je ni hatua gani sisi wadanganyika tuichukue au tuendelee tu kubaki wadanganyika?Na kuwaachia hao wenye sirikali waendelee kututesa na kutunyanyasa?
Anon wote hapo juu mmetoa shule kubwa. Imenichukua muda mrefu kutafakari maoni yenu. ni kweli kuwa Marekani inatia mkwara. Mie nililenga kuwahamasisha watanzania kutumia fursa hii kama walivyofanya wamisri baada ya mabwana zake yaani Marekani kumchoka na kumtosa. Hivyo, silengi kuonyesha upendo wa Marekani kwa wadanganyika zaidi ya kuwasihi watumie fursa kama hii kama walivyofanya wenzao wa Burkina Faso baada ya Ufaransa kumchoka na kumtupa Compaore.
Kuhusiana vijana kushiriki biashara haramu ya mihadarati kwa kisingizio cha kutokuwa na ajira nadhani si jibu. Je kwa kuishia hata kufia magerezani ndiyo wamepata ajira? Badala ya kuhatarisha maisha yao kwenye kusafirisha uchafu kwanini wasihamasishane wakaingia mitaani kuikomboa nchi yao?
Ama kuhusiana na zawadi ya Xmas sijasema kuwa kila kitu ni sahihi zaidi ya kutaka kuonyesha hata wenzetu ambao si watanzania wanavyomuelezea rais wetu ambaye ametokea kuwa bomu kuliko watangulizi wake. Hivyo, nilichotaka kufanya, kama ilivyokuwa kwenye sakata la Marekani kumkoromea Kikwete ni kujenga mazingira ya kutafakari kutumia fursa kama hizi kujikomboa badala ya kulalamika lalamika. Naona nijibu kwa ufupi wakati nikiwahi kuandika mengine. Nawashukuru wachangaiaji wote kwa muda na mawazo yenu. Karibu tena.
Post a Comment