The Chant of Savant

Saturday 20 May 2017

Fisi anapochunga kondoo wa Bwana

 
            Japo vitabu vya dini vinatuzuia tusihukumu ili tusije kuhukumiwa, kuna wakati mwingine hakuna namna bali kuhukumu. Mlevi siogopi kuhukumiwa hasa ninapowahukumu wanaopaswa si kuhukumiwa tu bali kuchomwa moto. Wasichojua wengi ni kwamba dhana nzima ya usihukumu ili usihukumiwe ilipenyezwa kwenye vitabu husika na wakoloni wa kiutamaduni ili tusiwahukumu wao hata walipoturarua kama fisi wafanyavyo kwa kondoo hivi sasa chini ya kivuli cha uchungaji, uaskofu, unabii na madude mengine.
            Tukio la kutia kinyaa na kuamsha hasira lililotokea kwenye wilaya yeye jina kama Korogwe ukiondoa ‘O’  mbili na kuweka ‘A’ kwenye mkoa ulio jirani na kaya inayotawaliwa na imla mmoja kwa zaidi ya miaka 30 aitwaye M7 hivi karibuni, limenifanya nirejee kuandika masuala ya dini ambayo mara nyingi huwa sipendi kuyaandika bali kwa kulazimika. Katika taarifa toka kwenye gazeti moja la kila siku, ni kwamba mchungaji sorry mchunaji mmoja aitwaye Jaff Jose wa Kanisa la Huduma katika Kristo, aliamua kumuiba muumini wake aliyetajwa kwa jina la Domie  Domitie akidai alioteshwa na Mungu kufanya hivyo! Hivi kweli hili ni Kanisa la Huduma katika Kristo au kanisa la Hujuma kwa Kristo? Upuuzi mtupu. Mungu gani akuoteshe uzini wakati anakataza uzinzi? Ujinga mwingine unatia kinyaa.
            Pamoja na wahusika kusukumwa na ujinga na tamaa, kuna somo kwa kaya yetu kuwa tumegeuka kaya ya hovyo ambapo kila tapeli anaweza kuja na kuwabamiza mkenge walevi chini ya kisingizio cha kuhubiri neno la Mungu. Kaya yetu imebariki utapeli na ujinga huu ambao matapeli sasa wameugeuza chanzo cha utajiri wa kutisha.
            Kuhusiana na kadhia tajwa, ni bahati mbaya mwandishi aliyeiripoti hakufanya kazi yake vizuri. Kwani, pamoja na kupata majina ya wahusika, alishindwa kutaja kijiji au mji lilipotokea tukio hili la kishenzi na kishetani linalopaswa kulaaniwa huku mhusika akipaswa ashitakiwe kwa kosa la kubaka ili aozee kifungoni. Hata hivyo, tokana na wepesi wa mitandao ya kijamii inayoshutumiwa na watawala, tuliweza kupata jina la kijiji ambacho kinaitwa Nyabwexxx kata ya yenye jina kama mtoto wa ng’ombe. Bahati nzuri mkuu wa wilaya hiyo, Godfrey Mheruyyy aliamua kuingilia na kuamuru mhusika achukuliwe hatua za kisheria. Wapo wanaoweza kusema kuwa sakata hili si kosa la jinai. Ila ukiangalia mbinu ya kuoteshwa aliyotumia mchunaji kumshawishi muathirika wake, alichofanya hakina tofauti na kulazimisha ambako ni mojawapo ya sifa zinazokamilisha kosa la ubakaji.
            Je kama jamii tunao akina Josie wangapi wakiwahadaa akina Domie wetu wajinga kuwa wanawapa huduma ya kiroho wakati wakiwatumia kwa hujuma zao za kiroho? Je tutaendelea kuwa na upuuzi huu hadi lini? Hapa tunaongelea wachunaji waliojipachika uchungaji. Hatujagusia waganga wa kienyeji ambao wengi wao wanasifika kwa kuwabaka na kuwaibia wateja wao wajinga na washirikina sawa na wachunaji wanaojipachika vyeo vya kiroho wakati hawana chochote bali uroho. Hawa wanajifanya wana roho mtakatifu wakati wamejaa roho mtakakitu.
            Hawa wanaojipachia vyeo utawajua kirahisi. Wanapenda utajiri wakati Mwana wa Adam wanayemhubiri aliuchukia. Wanapenda sifa hadi kujipachia udaktari wa ajabu ajabu ilmradi waonekane wamesoma hata kama wengi wao ni vilaza na vihiyo walioghushi na kujipachia vyeo vya kidini na kisomi kama ilivyo kwa wengi. Wanapenda sifa kiasi cha kutumia mitandao, runinga, magazeti na kila liwezekanalo kutangaza biashara yao. Sikumbuki Mwana wa Maria akitangaza huduma yake. Kumbuka mtu aliyemponya ukoma. Kwa furaha alitaka kwenda kuwatangazia wenzake. Lakini Yesu alimkataza kufanya hivyo Luka 5:14. Hii maana yake ni kwamba Yesu hakupenda sifa. Alitaka ukweli ujitangaze wenyewe. Je hawa wanaotangaza hujuma yao kwenye vyombo vya habari tena kwa kuanzisha au kulipa mamilioni ya fedha, kwanza wanapata wapi? Je wanategemea kupata nini? Je hiyo pesa wanaipata wapi?
            Tokana na dini kutumika kuwaibia, kuwadhalilisha na kuwadhulumu watu wetu wengi wajinga, kuna haja ya kuibana sirikali kupiga marufuku uanzishwaji wa biashara hii ambayo sasa imegeuka tishio hasa wakati huu kaya inapopambana na tishio la ukimwi na umaskini ukiachia mbali ujinga. Tutaendelea kuwatoa sadaka walevi kwa mapapa na manyangumi wa utapeli wanaotumia neno la Mungu hadi lini?
            Matukio ya wahalifu wanaojipachika uchungaji kuchukua wake za watu, kutia mimba waumini wao hata kutorosha wake za wenzao yanazidi kuongezeka kayani huku sirikali ikiyafumbia macho. Je tunangoja walevi wajichukulie sheria mkononi kwa kuwachoma moto wahalifu hawa halafu tuanze kuwalaumu? Sidhani kama ni jambo jema kwa kaya kutaka watoa huduma nyingine wawe na taaluma ya huduma wanazotoa  lakini wakawaacha wachunaji na waganga wa kienyeji kuendelea kuharibu jamii yetu. Haiwezekani tuhakiki vyeti vya wahudumu wa umma lakini tuwaache hawa na wenzao wanasiasa akina Bashite wa Bashiit wa Koromija. Ni hasara na majuto kiasi gani kujikuta umemuamini shetani ukidhani ni malaika? Mchungaji anapogeuka mchunaji, kondoo wakae chonjo.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: