Saturday, 13 May 2017

TPSF mnamuonea Magufuli bure

Image result for photos of tanzania private sector
          Malalamiko ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania au Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) ya hivi karibuni kuwa serikali inaminya sekta binafsi hayana msingi. Mtendaji mkuu wa TPSF Godfrey Simbeye alikaririwa na vyombo vya habari akisema “ni makosa kufikiri  hivyo kwani wafanyabiashara ni injini ya kukua uchumi na wao ndio wenye uwezo wa kufanya mambo mengi na kwa wingi wao huleta tija katika uchumi husika.” Hakuna asiyeelewa hili.  Hata hivyo, sidhani kama dhana hii ina mashiko; hasa ikizingatiwa kuwa biashara ni uwanja wa mashindano makali. Ni sawa na mashindano ya ngumi au mpira au michezo au sekta nyingi nyingine zenye ushindani wa hali ya juu. Bila kujiandaa, anayeshiriki haya mashindano ataishia kushindwa. Na hiyo ndiyo kanuni ya mchezo.
            Sidhani kama sheria ya Tanzania inazuia ushindani, uwe miongini mwa watu binafsi au baina yao na serikali. Asiyependa wala kuuweza au kuukubali ushindani ajiondoe kwenye biashara na kufanya shughuli nyingine badala ya kulalamika. Kwanini kuwa na ushindani kwenye sekta nyingine na iwe sawa lakini iwe tatizo inapokuja kwenye biashara ambayo asili yake ni ushindani?
            Kwanini kujali maslahi ya wafanyabiashara huku tukidharau au kukandamiza ya walaji ambao wengi ni watanzania? Mfano, kwa mujibu wa rais John Magufuli, ujenzi wa hosteli za Mabibo uligharimu shilingi bilioni 28 zaidi ya miaka kumi iliyopita, wakati hosteli za sasa za Chuo Kikuu zilizojengwa na Tanzania Buildings Agency (TBA) kwa jumla ya shilingi bilioni 10 tu. Rais alisema kuwa aliamua kuwapa TBA tenda ya ujenzi wa hosteli husika baada ya makampuni mengi kuja na qoutations za juu hadi bilioni 150. Hatuwezi kuendeleza business as usual huku tukiumiza uchumi na watu wetu eti kwa kulea sekta binafsi. Ushindani kati ya serikali na sekta binafsi si jambo baya kama lina tija kwa taifa. Hapa kwenye mkoa ninakoishi, serikali ina nyumba za kupangisha na ni za bei nafuu. Pamoja na hili, sijawahi kusikia wenye nyumba wakilalamika kuwa serikali inashusha bei na kuwanyima biashara. Hapa wanapenda na kukubali ushindani kama chachu ya kutoa huduma bora na nafuu kwa jamii. Hivyo, sekta binafsi ya Tanzania inapaswa kujifunza na kulikubali hili.
            Biashara yoyote inalenga kumpa faida mwenye kuifanya au kuianzisha. Hivyo, wanaotaka kujenga majengo ya serikali wanataka kupata faida huku na serikali nayo ikitaka kuokoa fedha nyingi ili kupata faida tokana na uwekezaji wake. Biashara haigombi. Hakuna ulazima wa serikali kuwapa kazi watu binafsi eti kwa vile wasiathirike kiuchumi. Kama wanataka kupata tenda basi watoe quotations zinazoingia akilini badala ya kuendekeza cha mbele.  Sidhani kama serikali itawanyima tenda wakati bei wanayotaka inalingana na thamani na matarajio ya miradi ambayo serikali inataka kuitekeleza bila kujali nani amepewa au kunyimwa tenda husika.
            Hata hivyo rais Magufuli alipingana na mawazo kuwa serikali ni adui wa wafanyabiashara kwa kusema  “tunajenga nchi na watu lazima waweke  uzalendo katika masuala haya ili nchi ipige hatua.”  Magufuli aliongeza kusema “choyo kwa kupata faida iliyopitiliza kutoka serikalini ndio ninachopinga na si kuwa adui wa wafanyabiashara ingawa inaonekana hivyo kwa watu wasio waaminifu.”
            Nadhani madai ya TPSF yanatokana na maozea ya kubebana ambayo yamelifikisha taifa hapa lilipo hasa ikizingatiwa kuwa tenda nyingi zilikuwa zikitolewa kwa rushwa huku thamani ya miradi ikiwa juu sana bila kulingana na kazi inayofanyika. Huu ni ufisadi uliolifikisha taifa hapa. Kimsingi, malalamiko ya TSFP ni ushahidi kuwa wengi wa watanzania hawajaelewa kasi ya rais Magufuli ya kuondoa mtindo wa mbovu na wa hovyo uliokuwa umejengeka kwenye kuhujumu taifa kwa faida ya kundi dogo la watu. Zama za mali ya umma haiumi nadhani zimekwisha. Laiti serikali ingewekeza hata kwenye nyumba za kupangisha za umma, nadhani wafanyakazi wengi wa serikali wasingeendelea kunyonywa na wenye nyumba binafsi huku nyumba nyingi za Msajili wa Majumba zikiendelea kukaliwa na tabaka moja la wenye fedha. Niliwahi kushauri serikali kuanzisha utaratibu wa kuwapa wafanyakazi wake nyumba za Msajili ili wafanyabiashara–ambao wengi wao wanaozikalia wana uwezo wa kujenga zao–wakajenge zao.
            Nani hajui kuwa hata wafanyabiashara, wengi wakiwa wa kihindi, ambao wanasemekana kuwa mabilionea wanaishi kwenye nyumba za Msajili huku walengwa wakiendelea kunyonywa na wenye nyumba binafsi, ukiachia mbali kuhangaika kulipa nauli kila uchao kwenda na kurudi makazini wakati nyumba zao zikifaidiwa na matajiri? Nadhani rais Magufuli anapaswa kuliona hili bila kusahau kurejesha nyumba za umma zilizotwaliwa na wakubwa wakati wa serikali ya awamu ya tatu.
            Tumalizie kwa kuwataka TPSF wajifunze kubadilika bila kusahau kukubali kuwa mambo yamebadilika. Japo binadamu mara nyingi hataki mabadiliko, yana tija pale yaliyolengwa kutimiza yanapotimia kama yalivyolengwa. Hivyo, si vibaya kusema kuwa TPSF wanamuonea Magufuli kwa kulaumu hatua zake za kuleta nafuu na huduma bora kwa wateja. Kama wanataka serikali ijiondoe kwenye biashara basi watoe huduma bora na kutoa quotations zinazoingia akilini badala ya kuigeza serikali shamba la bibi kama ilivyozoeleka chini ya awamu zilizopita ambapo watu walipewa tenda hata bila uwezo wa kuzikamilisha.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili kesho.

No comments: