Tuesday, 30 May 2017

Magufuli: Mwalimu wa maendeleo Afrika?

Image result for photos magufuli mkapa, kikwete and mwinyi
            Kitendo cha hivi karibuni cha rais John Magufuli kufukua makaburi yaliyozika maendeleo ya Tanzania, hata Afrika, ni cha kupongezwa na kupigiwa mfano. Baada ya kustukia wizi wa ajabu na kikatili ambao umefanyika kwa miaka nenda rudi, Magufuli aliunda kamati ya kuchunguza usafarishaji wa michanga yenye madini au makinikia. Tume hiyo iliibua mambo mengi ya kukatisha tamaa na kutia moyo kwa wakati mmoja kama Afrika itakubali kubadilika, kuwajibika na kutumia akili badala ya utumbo.
            Kamati hiyo iliyoongozwa na profesa Abdulkarim Mrumu iliundwa na wataalamu wa madini, kemia pamoja na mengine. Wataalamu hawa licha ya kuonyesha umahiri katika taaluma yao, walionyesha uzalendo wa hali ya juu. Kwani, kama alivyosema rais Magufuli, kulikuwa na kila mbinu ya kuwahonga ili wasifichue wizi huu wa kikatili unaofanywa na makampuni ya kimataifa yakisaidiana na watanzania wasio na utu wala uzalendo.
            Kitendo cha Magufuli kinatoa masomo mengi mojawapo yakiwa:
            Mosi, kuna watanzania waliosomeshwa kwa fedha ya umma wanaoitumia kuuhujumu umma huo huo uliwasomesha na kuwaajiri.
            Pili, kumbe Tanzania na nchi nyingine nyingi za kiafrika zilizojaliwa raslimali lukuki ni maskini wa ima kujitakiwa au kusikinishwa na mfumo kandamizi na nyonyaji  na wa kikoloni wa kimataifa ambapo nchi zinazodaiwa kuendelea zimekuwa zikitajirika kwa kuziibia nchi maskini. Mfano mdogo ni kwamba, tokana na makontena 277 ambayo ni shehena ya mwezi mmoja, Tanzania ilikuwa ikipoteza kiasi cha takriban shilingi 1.441 trilioni sawa na dola za Kimarekani 644,137,499 ambazo ukizidisha mara 12 yaani mwaka mmoja na ukazidisha mara miaka 19 unapata jumla ya dola 146, 863,349,772 ambazo licha ya kuwa kiwango kikikubwa ajabu kwa nchi maskini kama Tanzania, ni mara takriban kumi ya deni la Tanzania la takriban dola 14,120,000,000 hadi hapo 31 Decemba, 2014. Na huu ni wizi wa kampuni moja na mgodi mmoja tu wa dhahabu. Je kwa makampuni yote makubwa na madogo yaliyotapakaa nchini yakichimba dhahabu na madini mengine ya thamani, Tanzania na Afrika imeishapoteza utajiri kiasi gani?
            Kwa kuangalia mahesabu hayo hapo juu, ni ukweli usiopingika kuwa Tanzania haikupaswa kuwa nchi ombaomba bali ya kutoa misaada kwa nchi nyingine duniani. Hivyo basi, kama Afrika itakubali kubadilika na kujifunza tokana na mfano wa Magufuli, uwezo wa kugeuka bara tajiri kuliko yote kimaendeleo ni mkubwa na si jambo la kama inawezekana bali ni ukweli ulio wazi.
            Katika kitabu chake cha Africa Reunite or Perish, mwandishi wa makala hii anayadurusu matatizo makubwa ya Afrika kuwa ni ukosefu wa uongozi wenye akili timamu za kawaida yaani common sense kwa kiingereza. Kwani, anachofanya Magufuli ni kutumia common sense ikichangiwa na uzalendo na uchungu wake kwa Tanzania na Afrika ukiachia mbali hamu yake ya kubadili mfumo uliopo na kuleta maendeleo yenye kulenga kuinua hadhi ya mtanzania na mwafrika popote alipo.
            Sasa tuangalie baadhi ya masomo tunayoweza kupata tokana na mfano huu adimu na adhimu wa Magufuli.
            Mosi, si chuku. Inaonekana Magufuli ameamua kubadili msimamo wake dhidi ya kufukua makaburi aliyosema alikuwa akiogopa kuyafukia. Bila shaka, kwa safari aliyoianza, makaburi hayatanusurika hasa ikizingatiwa kuwa wizi huu uliasisiwa na wale waliojidanganya kuwa wanaweza kupona. Hapa lazima wote waliowahi kuwa mawaziri wa Nishati na Madini tangia mwaka 1998 wakae mkao wa kuliwa. Kama Magufuli atataka kukata mzizi wa fitina, lazima achunguze watangulizi wake ambao waliwapa fursa marafiki na wateule wao kuuza taifa kwa kuingia na kuridhia mikataba ya kijambazi iliyozaa wizi huu usio na huruma.
            Mbali na hili, kama nchi za kiafrika zikatkuwa nyepesi kujifunza, Magufuli anaingia kwenye vitabu vya historia kama kiongozi aliyejaribu na kuanzisha somo halisi la ukombozi wa Afrika litakaloiwezesha kutumia na kufaidi raslimali zake.
            Je Magufuli atafanikishaje somo hili? Hapa lazima awe tayari kuweka kujuana, urafiki na ukaribu kando ili kuweza kutenda haki na kufanikisha kile anacholenga kufanikisha. Hii maana yake ni kwamba, hataangalia sura ya au cheo, wala ukaribu wa mtu.
            Tumalizie kwa kuwataka waafrika na viongozi wao kutoona aibu wala kuchelewa kuanza kujifunza somo hili la ukombozi ambalo chimbuko lake ni Tanzania.  Wahusika wanapaswa kushirikiana na viongozi wao kutunga sheria zitakazowawezesha kusimamia mali zao huku wakitunga sheria kali za kupambana na wale wote wanaoibia bara letu wawe wananchi wenyewe au washirika wao toka ughaibuni. Wakati wa Afrika kuwa shamba la bibi unapaswa kuwa historia.
            Kimsingi, alichofanya Magufuli ni kujibu swali l a kwanini Afrika iwe tajiri wa raslimali lakini sambamba na hili iwe maskini kimaisha. Nadhani jibu limok wenye matendo ya kupongezwa na kujivunia ya rais Magufuli. Heko rais Magufuli. Je Magufuli atakumbukwa kama gwiji na mwalimu wa ukombozi na maendeleo ya Afrika? Mwenye macho haambiwi tazama.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.

No comments: