Wednesday, 17 May 2017

Kijiwe: Wachunaji Wachague Dini au Siasa

            Kijiwe cha leo kinajikita kwenye mambo ambayo wengi huogopa kugusa hasa wakiwa si wanachama wa chama twawala. Hii si jingine bali kuzuka kwa mtindo wa baadhi ya matapeli kujiita wachungaji wa kondoo wa Bwana wakati ni wachunaji. Wanajiita viongozi wa kiroho wakati ni viongozi wa uroho. Wanasema wana roho mtakatifu wakati wana roho mtakakitu kama yule aliyemchukua mke wa kondoo wake akadai shetani aliyemtuma ni Mungu wakati yeye ni shetani mwenyewe.
            Mpemba leo ndiye anaanzisha mada. Baada ya kuamkua na kubwia kahawa yake anasema “ hivi wenzangu waona niyaonayo mie tokana na huu upuuzi uloanza kuzoeleka wa wachunaji kujifanya wachungaji huku wakitoa matamko ya kisiasa kukutana na viongozi wa vyama vya kisiasa kana kwamba na wao ni wanasiasa?”
            Mbwa Mwitu anajibu “unashangaa wachunaji kujiingiza kwenye siasa! Kwani hujui huko ndiko ulaji rahisi na wa dezo uliko? Hujui kuwa ukiwa mwanasiasa unaweza kuitumia kuchuma na kufichia njuluku zako?”
            Mgoshi Machungi anachomekea “hii kwei. Tinawaona wakigombea uishiwa na uhishimiwa huku wakijiita viongozi wa kioho badaa ya kujiita viongozi waroho wanaotumia neno la Bwana. Hukumuona yule mama kihiyo ajiitaye daktari alivyoula uishiwa wa dezo hivi karibuni baada ya kutimuliwa da Sofi?Utawaona wakijikomba kwa wenye ulaji wengi wakiandaa mikesha na matamasha ya kuiombea kaya wakati kuomba kwa kwei kwapaswa kuwa sii ya anayefanya hivyo na Mungu wake.”
            Kanji leo hangoji. Anakula mic “ sasa dini na ombaomba nakuwa biasara. Kila siku iko ona vatu najitokeza ombea kaya. Naombea kaya kwani nakufa? Baniani hapana ombaomba. Yeye nafanya biasara na kuchomwa moto kama nakufa.”
            Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu na mapema “nimependa analogue yako Mpemba. Kweli hawa ni wachunaji si wachungaji. Ni maaskopo na si maaskofu. Wanamilki mimali kibao isiyo na maelezo ukiachia mbali kutia kila aina ya shaka ya namna walivyoipata kama siyo kuwaibia kondoo au kuuza mibwibwi.”
            Kabla ya kuendelea Mipawa anampoka mic na kusema “ usemayo ni kweli. Huoni wengi wengine wavyoingia kwenye ligi na akina Bashite baada ya kuwaibua huku wakijitahidi kujifanya wanampenda muungu wake? Sijui hii vita nayo imeishia wapi? Maana sioni mapapa yakibakuliwa. Au ilikuwa ni nguvu ya soda kama siyo danganya toto ya kutaka misifa ya kibashiteshite au kuficha kashfa ya kughushi?”
            Da Sofia Lion aka Kanungaemba anakula mic “nakubaliana na wote wanaowaona hawa kama wachunaji waliomweka Mungu wa kweli kando kwa kumuabudu muungu wao yaani fedha na utajiri wa haramu na haraka. Nadhani kuna haya ya sirikali kuwabana waeleze walivyochuma huu utajiri ili kuepuka hatari ya kuwa na wauza unga waliojificha nyuma ya majoho na mimbari.”
            “Tuwe nao mara ngapi wakati tunao tena wengi tu. Kwa vile kaya yetu ni ya kishirikina na kibabaishaji, kila tapeli anaweza kuja na lake na kufanikiwa. Huoni namna kuombea kaya kulivyogeuzwa dili la wachunaji wanaoibukia kujiweka karibu na lisirikali ili wapate sifa na ulaji. Kila siku kuombea kaya. Mtafanya kazi lini? Acheni ujinga. Nenda kafanye kazi kwanza. Hata kauli mbiu ya rais wenu ni “Hapa Kazi Tu” lakini siyo “Hapa Kuomba Tu,” anajibu Kapende huku akimpa kipisi cha sigara kali Mijjinga anayempoka mic na kusema “hakuna kinachonikera kama watawala wetu kukumbatia wahalifu hawa. Sijui lao moja au nao ni sawa na wale kondoo wanaochunwa na kuraruriwa kila siku? Maana sioni mantiki ya wao kuendelea kuwaendekeza wahalifu kama hawa ambao mwisho wake wataangamiza kaya yetu. Hata Yesu alisema kuwa mchovu hataishi kwa mkate tu. Kuna haja ya kuibana sirikali ili nayo iwabane hawa wana hizaya wajalaana wanaofikiri kwa matumbo badala ya vichwa.”
            mheshimiwa Bwege aliyekuwa akisoma gazeti anaamua kutia guu. Anasema “mie sishangae huu ubwege unaofanywa na hawa mabwege. Kama kaya imejigeuza ya mabwege kwanini mabwege wasijifanyie ubwege watakavyo kiasi cha kuhatarisha usalama wake? Kama kaya inatawaliwa na akina Bashite huku wakikingiana vifua kwenye uovu, unataka hawa matapeli wakale lupango wakati mabwege wa kuingiza mkenge ni wengi? Hamkumsikia bwege aliyemchukua mke wa bwege mwenzie akidai eti kaambiwa na Mungu wakati ni ushetani mtupu unaotokana na ujuha, ubwege na utapeli wa kiroho unaotawaliwa na roho mtakakitu aitwaye mtakatifu? Wajinga ndiyo waliwao; waliasa wahenga. Japo hawa mabwege wanakera, hakuna namna ya kuwakomesha bali jamii nzima kubadilika ikaacha ushirikina na kutegemea kupata bila kutoa jasho wala kutumia akili na maarifa.”
            Kabla ya kuendelea mzee Maneno aliamua kumchomekea na kusema “mheshimwa Bwege hapa umeua kila kitu. Ni kweli sisi ni kaya ya mabwege tunaopaswa kubadilika. Vinginevyo huu utapeli usingeweza kufanikiwa kama jamii yetu isingekuwa ya kibwegebwege. Nakubaliana nawe; hawa si viongozi wa kiroho bali waroho tu wenye roho mtakachafu.”
            Kijiwe kikiwa kinachanganya si akaja mchunaji akijifanya anataka kutulisha neno. Acha tumlishe mingumi kabla ya ndata hawajaja kutibua move yetu.
Chanzo; Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: