Wednesday, 24 May 2017

Nani anakumbuka mauji ya kipumbavu kama ya Mvumi?

 Image result for picha za wahanga wa iringa mvumi
Tukio la kusikitisha la kinyamana na kipumbavu lilotokea Oktoba 1, 2016 huko kijijini Iringa Mvumi lilistua na kuchukiza wengi ukiachia mbali kwa taifa. Wataalamu wawili wa  Udongo na dereva wao toka kwenye kituo cha Seliani mkoani Arusha waliuawa eti kwa kudhaniwa ni wanyonya damu au mumiani.  Hii maana yake ni kwamba bado tunajenga taifa la watu mbumbumbu, washirikina na wakatili wanaoweza hata kuondoa uhai bila kujiridhisha kuwa kile wanachoshuku ni kweli au siyo. Tukio hili lilitangazwa na kulaaniwa nchi nzima wakati ule. Hata hivyo, baada ya kujitokeza upungufu wa namna hii kwenye uelewa na imani za wananchi wetu, wahanga walizikwa na huo ukawa ndiyo mwisho wa habari yao. Hatujui nini kilitokea kwa familia za wahanga kuhusiana na stahiki zao kama mafao, fidia na mengine kama haya. Leo kwa makusudi mazima, tunajikumbusha tukio hili la kikatili na kutisha lau kukumbushana kama jamii na taifa ili kuepuka kurudiwa mahali pengine nchini.
Kwanza, tunajitahidi kuvaa viatu vya wahanga au wapendwa wao kuona nini tungetaka tufanyiwe baada ya kukumbana na mkasa kama huu ambao bila shaka mwenye kulaumiwa ni serikali kwa kutowaelimisha watu wake vya kutosha ukiachia mbali kutokuwa na mfumo wa haraka wa mawasiliano ambao ungeweza kuepusha vifo hivi vya wataalamu na hasara ambayo taifa lilipata tokana na ujima na upumbavu huu.
Ni bahati mbaya kuwa wahanga wa kadhi ahii walikuwa wakipambana na kutumia ujuzi wao kuwasaidia hawa hawa waliowaua kutokana na hisia na imani za kipumbavu. Ni hasara na unyama kiasi gani? Tunashauri serikali ieleze namna ambavyo ilizifidia familia za wahanga wa ujinga wa taifa unaotishia kuliteketeza taifa letu. Kama haijafanya hivyo, tunaandika kuikumbusha wajibu wake hasa ikizingatiwa kuwa wahanga waliacha wapendwa wao waliokuwa wakiwategemea.
 Inashangaza kuona baadhi ya watu wetu wakishabikia na kushiriki mauaji ya kujichukulia sheria mikononi kama vile kuchoma moto vibaka wakati wakiabudia na kuvumilia mibaka mikubwa tu. Lazima tuseme wazi kuwa kosa hili si la wauaji wa Iringa Mvumi pekee bali taifa kwa ujumla hasa wale walioteka uhuru wetu na kuwajaza watu wetu ushirikina na ujinga. Kusema ukweli, tuna mfumo mbovu wa kishirikina na kipumbavu ambapo matapeli wachache huruhusiwa kuhubiri sumu ima kupitia dini au uganga wa kienyeji. Rejea mauaji ya mara kwa mara ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Je sasa nini kifanyike? Tutaotoa baadhi ya maangalizo hapa ili kuepusha kurudiwa kwa aibu na unyama huu ambavyo ni pigo kwa taifa:
Mosi, wataalamu au watu wetu wanaoingia kwenye maeneo mageni ima wapewe ulinzi wa askari au waruhusiwe kupeperusha bendera ya taifa kwenye magari yao. Kwani, watu wetu wamezoeshwa kuogopa bendera kama alama ya serikali.
            Pili, wananchi wetu waelimishwe namna ya kuheshimu na kutumia sheria. Inasikitisha kuona kwenye karne ya 21 bado Tanzania ina watu wasiojua hata namna ya kuripoti matukio au watu wanaowashuku hadi wanajichukulia sheria mikononi kama ilivyotokea hivi karibuni huko kwenye kijiji cha Iringa Mvumi mkoani Dodoma.  Jambo linaloonyesha kuwa tumefika pabaya sana kimfumo na kijamii ni ile hali ya serikali kuchukulia mauaji husika kwa wepesi sana. Kama ingekuwa inachukulia kadhia kama hii kwa uzito, tungesikia lau bungeni suala kama hili likijadiliwa na wabunge ili kuangalia nini kifanyike. Wahanga wa Iringa Mvumi wamesahaulika; na hakuna anayewaongelea ili kuepusha kadhia kama hii kutokea tena nchini.
            Sijui kama waziri wa mambo ya ndani analo tena kwenye kumbukumbu zake hasa wakati huu mauaji mengine kama yanayoendelea Kibiti yanaposhamiri. Vinginevyo, tungesikia lau wamepewa hata nishani au zawadi za utumishi bora katika mazingira hatarishi ambayo yaliwagharimu maisha yao. Lazima wahanga wakumbukwe kwa namna ya pekee. Kwani walikufa kazini wakitekeleza kauli ya “Hapa Kazi Tu” ya rais John Magufuli ingawa hakuliona hilo. Namuuomba na kumshauri rais aliangalie hili kwa uzito wa pekee ili kujua namna familia za marehemu zinavyoendelea.  
            Mwisho, katika kuwakumbuka wahanga wa Iringa Mvumi, serikali iangalie namna nyingine ya kukomesha kadhia hii ni kwa serikali kuwachukulia hatua watendaji wake waliowezesha kujengeka mazingira ya uhasama na kutoaminiana miongoni mwa wanakijiji uaji ambao inasemekana walishachoshwa na mauaji yanayodaiwa kutekelezwa kwa maagizo ya mwanakijiji mwenzao aliyekuwa akilindwa na wakubwa wilayani Chamwino kama gazeti moja la kila siku lilivyofichua. Hawa walipaswa kuwa korokoroni huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kupata ufumbuzi wa kudumu.   Hii ndiyo namna ya pekee ya kuwafariji jamaa za marehemu na kuwaenzi marehemu waliokufa kutokana na ujinga ulioachiwa kutamalaki nchini ukiachia mbali imani za kishirikina ambacho ni chanzo kizuri cha mauaji haya. Hivi kweli Tanzania bado kuna mumiani katika karne ya 21? Ni aibu kiasi gani!     
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: