Wednesday, 17 May 2017

Magufuli asipuuzie shutuma za Kenya dhidi yake

Image result for photos of uhuru kenyatta and magufuli
            Hivi karibuni, mara mbili bila kuthibitisha madai yake ya ajabu, kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la taifa, Aden Duale, alikaririwa akiishutumu Tanzania kutaka kuingilia uchaguzi wa Kenya unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu. Duale alikariri akisema kuwa chama chake cha Jubilee kina taarifa kuwa Muungano wa Upinzani nchini humo ujulikanao kama National Super Alliance (NASA) una mpango wa kuunda kituo cha kudungua taarifa za uchaguzi ili kumpendelea mgombea wake Raila Odinga ambaye ni rafiki wa rais John Pombe Magufuli. Gazeti la kila siku la kiingereza la Kenya la Daily Nation (May 14, 2017) liliandika “wakati wa kumpitisha  rais Uhuru Kenyatta naibu rais  Uhuru Kenyatta  kama wagombea wa Jubilee,  kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la taifa Aden Duale alidai kuwa serikali ya rais John Magufuli ilikuwa imejitolea kuwa mwenyeji wa kituo sambamba cha upinzani cha kukusanyia kura.”
            Hata kama kweli Tanzania ingejitolea kuwa mwenyeji wa kituo tajwa, bado sheria ya Kenya inayotokana na hukumu ya hivi karibuni ya mahakama nchini mle, inaruhusu upinzani kukusanya matokeo yake ili kuepuka wizi wa kura. Hata hivyo, hili ni suala la ndani ya Kenya hata kama lipo kisheria ingawa ni tuhuma za hovyo, zisizo na mashiko.
            Tuhuma hizi mbali na kuwa za ajabu na kubwa, si za kunyamazia hasa ikizingatiwa; zinaweza kuathiri mahusiano ya mataifa haya mawili jirani yenye kutegemeana kwa mambo mengi. Hivyo, Magufuli na serikali ya Tanzania, rasmi waitake Kenya kuthibitisha au kuondoa madai yake huku wakiomba msamaha kwa Magufuli na Tanzania.
            Hakuna ubishi. Uhusiano wa Kenya na Tanzania si mzuri. Hii ni baada ya Kenya kutaka kutumia kivuli cha mgongo wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) inazozikutanisha nchi tano za ukanda huu zikiwemo nchi mbili tajwa. Hivi karibuni, kulikuwa na vuta ni kuvute kuhusiana na kusaini mkataba wa kibiashara na Jumuia ya Ulaya (EU) ambao ulipingwa vikali na Tanzania huku ukiungwa mkono na Kenya kwa sababu ya kutaka kulinda mahusiano na maslahi binafsi.
            Pili, kuna suala la nchi rafiki na jirani ya Uganda kukatiza mkataba wa kupitisha bomba la kusafirisha mafuta yake kwenye nje kupitia Kenya na badala yake kuamua bomba husika kupitia Tanzania. Si hilo tu, historia ya Ukanda huu haiwezi kukamilika bila kugusia kuuawa kwa Jumuia ya Afrika Mashariki ya Kwanza (EAC 1) ambayo ilikuwa na wanachama watatu yaani Kenya, Tanzania na Uganda iliyouawa mwaka 1977 baada ya Uganda–chini ya Idi Amin wakati ule–na Kenya kuihujumu na kuisababishia hasara kubwa Tanzania.
            Pamoja na hasara kubwa, Tanzania iliamua kusamehe na kuacha yaliyopita na kuganga yajayo. Lakini hali ilivyo, inaonyesha; bado Kenya wana ngoa  ya kihistoria ambayo mbali na mambo yaliyotajwa inatokana na kukataa kuunganisha nchi za Afrika Mashariki kuwa taifa moja. Hii ilitokana na hali ya Kenya kujiona kama iko mbele na mbali kuliko Tanzania jambo ambalo halina mantiki hata kidogo hasa ikizingatiwa; nchi zote mbili ni maskini zinazoishi kwa kutegemea wafadhili ukiachia mbali kukumbwa na matatizo mengine kama vile uchumi mdogo, ukosefu wa ajira, ongezeko la watu, majanga ya kijamii, kuwa nyuma kiteknolojia na kimaendeleo na mengine mengi yanayozikumba nchi changa.
            Kitu kinachoshangaza na kuchukiza ni ile hali ya kudai kuwa Tanzania ina mpango wa kuingilia na kuvuruga uchaguzi wa Kenya. Ili iweje na ipate nini? Kenya wanapaswa kuwa wakweli kuwa hali ya kisiasa cha muungano tawala wa Jubilee ni mbaya kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi ulizotoa; kushindwa kupambana na rushwa hasa wizi wa fedha za umma; unyakuzi wa ardhi; kupanda kwa bei za mahitaji muhimu na maisha kwa ujumla; na kukabiliwa na vita nchini Somalia kati ya mengi mengineyo yanayolikabili taifa hili.
            Tunasema; Tanzania isipuuzie tuhuma hizi hasa ikizingatiwa; akumulikaye mchana usiku hukuchoma. Pia inabidi ifahamike; kwa muungano wa Jubilee, kubakia madarakani kwa mbinu zozote ni bora kuliko maslahi ya taifa. Rejea namna tamaa ya madaraka ilipolitumbukiza taifa hili kwenye mauaji ya kikabila ya wenyewe kwa wenyewe almaarufu kama Post-Election Violence (PEV-2007) yaliyosababisha vifo vya zaidi ya raia 1,000 wasio na hatia.
            Badala ya Tanzania kunyamaza na kupuuza madai ya Kenya, iionye, na kutaka iyafute na kuomba msamaha huku muungano wa Jubilee na Kenya kwa ujumla zikiaswa zitatue matatizo yake ya ndani badala ya kutafuta visingizio. Je muungano wa Jubilee una mpango wa kuvuruga au kuiba uchaguzi kama ulivyoshutumiwa kufanya kwenye uchaguzi wa 2013?
            Muhimu, Tanzania iueleze ulimwengu; haina maslahi yoyote katika kuvuruga uchaguzi wa Kenya hata kama mgombea mmojawapo ni rafiki wa rais wa Tanzania. Mbali na hilo, Tanzania iionye Kenya kuacha kufanya chokochoko ambazo matokeo yake si mazuri kwa ukanda mzima.
            Tumalize kwa kushauri hekima na busara kutumika kwa pande mbili hasa ikizingatiwa kuwa unaweza kumchagua rafiki lakini si jirani. Bado nchi hizi mbili zinahitajiana hata kama zitakuwa chini ya serikali isiyotokana wala kuundwa na muungano wa Jubilee. Kenya ni zaidi ya Jubilee, Magufuli, Odinga na Kenya. Mungu ibariki Afrika.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: