Wednesday, 3 May 2017

Kughushi: Viongozi wa umma wachunguzwe

Image result for cartoons of forgery in africa
Hapo tarehe 28 Aprili 2017, rais John Magufuli alikabidhiwa na kupokea ripoti ya uhakiki wa wafanyakazi wa umma kule Dodoma iliyowasilishwa na waziri wa Ofisi ya Rais-Utumishi Angela Kairuki. Ripoti hii ilibaini wafanyakazi wasio na sifa, hewa na walioghushi wapatao 9,932 nchini. Kimsingi, namba hii si ndogo na ni ushahidi kuwa taifa lilikuwa likiibiwa na kudanganywa na wahusika jambo ambalo ni jinai ya wazi inayopaswa kushughulikiwa vilivyo kisheria na si kisiasa kama inavyoonyesha. Ni bahati mbaya kuwa taarifa haijasema na fedha kiasi gani taifa lilikuwa likipoteza kila mwezi na tatizo lilianza lini.
Baada ya kupokea ripoti hii, rais aliwaachisha kazi wahusika hapo hapo huku akitoa amri yenye utata. Rais alisema kuwa wale watakaojiondoa kufikia tarehe 15 Mei, wasipelekwe mahakamani huku watakaokaidi wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria. Hii si sawa. Je rais anawasamehe wahalifu hawa kwa mamlaka, misingi na sababu vipi wakati hana mamlaka kisheria? Rais siyo mahakama na kisheria hana mamlaka yoyote ya kusamehe au kuadhibu mtu. Aache vyombo husika vitimize wajibu wake. Pia tunamshauri rais ajitenge na zoezi hili  ili kujenga uwajibikaji wa pamoja.
Haiwezekani watu wapoteze muda na fedha kusaka elimu–na wengine wasipate ajira–wakati vihiyo wachache wakiajiriwa bila kuwa na sifa wala elimu stahiki. Tanzania si nchi ya kifalme. Inaendeshwa na kanuni, katiba na sheria na si utashi wala amri za rais. Hivyo, tushauri kuwa rais amemaliza kazi yake. Aache vyombo husika vitimize wajibu wake.
Ili kukata mzizi wa fitina, tunashauri yafuatayo:
Mosi, wote waliobainika kutenda jinai husika wafikishwe mahakamani bila kujali kama wamejiondoa au la. Sheria ya Tanzania haitoi mamlaka yoyote kwa rais au kiongozi yoyote kusamehe makosa ya jinai. Hivyo, kufanya hivyo, licha ya kuvunja sheria, ni kuendelea kukwamisha taifa.
Pili, warejeshe fedha zote walizochuma wahusika bila cha msalie mtume.
Tatu, waliochuma mali tokana na kupata malipo wasiyo nayo stahiki wataifishwe mali zote walizochuma kwa kipindi chote walichokuwa katika ajira ya umma bila kustahiki.
Nne, majina yao yatangazwe kwenye vyombo vya habari ili umma uwajue na kuwatahadhari.
Tano, Waziri Kairuki alikaririwa akisema kuwa zoezi la uhakiki wa wafanyakazi wa umma halikuwahusu viongozi wa umma. Hii ni ajabu kidogo. Kwani viongozi wa umma si watumishi wa umma?  Mbona wanalipwa mishahara tokana na kodi za umma? Tunajenga mfumo gani wa uongozi iwapo viongozi wanakuwa hawaguswi (untouchable au sacred cows)?
Sita, zoezi husika linapaswa kuwahusisha kada ya viongozi wa umma. Japo waziri alitumia katiba ibara ya 67 (1) kuwaondoa viongozi wa umma kwenye uhakiki huu, wanapaswa kuhakikiwa kwani nao ni watumishi wa umma. Pia wahusika wanapaswa kuwa na elimu hata kama si ubobezi au utaalamu. Katiba yetu iko wazi kuwa watanzania wote ni sawa. Sasa usawa huu uko wapi iwapo wapo watendaji wa umma tena viongozi wasiopaswa kuwa na elimu ya kutosha? Mbona rais anateua wengi wa watendaji wake kwa kuangalia elimu? Je kwa kuwatenga viongozi wa umma tunatoa picha gani kwa watanzania? Nadhani kuna haja ya vigezo vya elimu kuwahusisha watanzania wote ili kutoa motisha kwa wananchi kujiendeleza badala ya kutegemea kubebwa kwa kisingizio cha uongozi wa umma. Lazima viongozi waongoze kwa mfano na si kujipendelea. Kuendelea kuwatenga viongozi wa umma si chochote wala lolote bali kufanya ubaguzi na upendeleo vinavyoibua kigeugeu (double standard) cha hali ya juu. Haiwezekani tukawa na wafanyakazi wanaopaswa kuelimika kihalali vililvyo, lakini wakaongozwa na viongozi wasio na sifa kielimu. Hii italikwamisha taifa hasa ikizingatiwa kuwa wafanyakazi wa umma wenye elimu na taaluma watatoa ushauri wa viongozi vihiyo nao watakaidi kuchukua na kutumia ushauri huu wa kitaalamu.
Hivyo basi, waziri husika apeleke sheria bungeni kubadili kifungu cha katiba kinachowabagua watanzania kwenye masuala nyeti kama elimu na uwajibika. Hii itaondoa malalamika kama yanayoendelea dhidi ya mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda ambaye, kwa mujibu wa kauli ya waziri amesafishwa na kuacha watanzania vinywa wazi. Wananchi wanapaswa kutokubali kigeugeu hiki na ubaguzi huu vya wazi.
Kama taifa, Tanzania inapaswa kuendeshwa na kuongozwa na watanzania wenye  elimu na sifa vilivyopatikana kihalali na si kubebana wala kupendeleana.  Kwa nchi yenye uwajibikaji wa kweli usio wa kinafiki wala kisanii, kiongozi yoyote na wa ngazi yoyote, anapotuhumiwa kutenda uchafu, anapaswa kuwajibishwa mara moja ili achunguzwe na ukweli ujulikane ili haki itendeke na sheria na katiba vifuatwe.  Huwezi kuwa na sheria zinazotumika kwa vigezo tofauti ukaendeleza taifa. Ni aibu kuwa watuhumiwa wa kughushi walioko kwenye uongozi wa umma kuendelea kuwa kwenye ofisi za umma au wanaowakingia kifua kuendelea kufanya hivyo.  Hii nchi ni ya watanzania wote kwa usawa bila kujali nafasi zao au ushawishi wao au ukaribu na wenye madaraka yanayoanza kutumiwa vibaya wazi wazi.
Tumalizie kwa kuishauri serikali iondoe kigeugeu kilichojitokeza ili kurejesha heshima yake na kutoa nafasi kwa uwajibikaji wa kweli kama motisha kwa watanzania kuendesha maisha yao kwa kufuata sheria na kanuni na si ku-jump kama alivyosema rais Magufuli.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.Image result for cartoon of forgers

No comments: