Saturday, 27 May 2017

Makaburi, makinikia, Magufuli na Muhongo

Image result for photos of magufuli and muhongo
            Japo rais John Magufuli aligoma kufukua makaburi kwa hofu kuwa angeshindwa kuyafukia, sasa makaburi yanajifukua yenyewe ili watanzania wayachunguzee; na baadaye wayafukie. Tukio la hivi karibuni la kumtumbua rafiki yake kipenzi profesa Sospeter Muhongo aliyetuhumiwa kunufaika na fedha za wizi katika kashfa ya mabilioni ya Escrow ni ushahidi tosha kuwa sasa makaburi yanaanza kujifukua ili watanzania wayafukie.
            Hata alipoonywa kuwa Muhongo ni jipu, tena la kunuka, Magufuli alitumia mabavu na madaraka yake kumsafisha na kumteua tena asijue la kufa halina ubani. Abyssus aabyssus invocat walatini walisema yaani jehanamu huita wa jehanamu! Tusisitize hapa: Kama siyo kutumia ubabe, rais Magufuli hakupaswa kumrejesha profesa Muhongo tena kwa kumzawadia nafasi tena nono na nyeti ili aendelee kufanya mambo yake kwa mazoea. Marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere aliwahi kusema: Kwa mke wa Kaisari kosa si kutenda kosa bali hata kutuhumiwa. Hata hivyo, hongera kwa kumtimua Muhongo na pole kwa kumteua hata alipotuhumiwa.
            Sasa ukweli umeishadhihiri shahidi. Je nini kifanyike katika kushughulikia haya makaburi ambayo rais anayaogopa kuyafukua kwa vile atashindwa kuyafukia? Tunapendekeza yafuatayo:
             Mosi, wahusika wote waliosababisha hasara hii ya mabilioni wunguliwe mashtaka kuanzia mwaka 1998 wote waliowahi kutumikia wadhifa huu ili haki kwao na kwa watanzania itendeke. Kwani wanajulikana na wapo tena wana ukwasi usioweza kutolewa maelezo.
            Pili, mali zote zinazomilkiwa na watuhumiwa au washirika zao zikamatwe na kutaifishwa wakati uchunguzi wa namna walivyozipata ukiendelea.
            Tatu, kwa wale waliokwisha kustaafu na kufa, warithi wao wanyang’anywe mali zote walizopata au kurithi toka kwa marehemu.
            Nne, serikali itekeleze ushauri wote wa tume iliyochunguza sakata hili huku ikihakikisha vyombo vya usalama vinajikita kwenye kulinda mali za umma badala ya kuhangaishwa na masuala ya kisiasa likiacha nchi ikiibiwa kana kwamba haina vyombo vya usalama.
            Tano, mikataba yote ya madini ikaguliwe na kuangalia kama imekidhi viwango na itakayokutwa inaruhusu wizi huu wa ajabu ifutiliwe mbali huku wahusika wakilazimika kuingia mikataba mipya au kupigwa marufuku kufanya biashara nchini. Hili suala si la mchezo. Ni suala la usalama wa taifa. Hivyo, wale wanaojidai kutetea uwekezaji wa kijambazi kama huu wasisikilizwe zaidi ya kuchunguzwa kama kuna namna wanavyonufaika na jinai hii kwa taifa.
            Hebu tujiulize kama taifa sakata hili limetupa somo gani ukiachia mbali kuacha maswali mengi bila majibu kama vile:       
            Je tumeishaibiwa kiasi gani kwa miaka yote hii ambayo mambo yamekuwa yakijiendea? Na fedha hiyo ingeweza kulisogeza mbele kimaendeleo kiasi gani? Je wahusika ni nani? Lazima wasakwe na kutangazwa kwenye vyombo vya umma ili umma uwajue na kuweza kutoa ushahidi pale serikali itakapohitaji taarifa zao. Pia ni vizuri kujua wahusika wana mali kiasi gani iliyotokana na ujambazi huu wa wazi ili kuweza kujua ni kiasi gani kilitoroshewa nje na washirika wao kwenye jinai hii ambao pia tunaweza kuwaandama warejeshe fedha zetu; na wakigoma tunashika mitambo na mali zao walizo nazo nchini.
            Pia lazima serikali itunge sheria za kuepusha kurudi au kuendelea mchezo huu wa kuligeuza taifa shamba la chizi siyo la bibi maana shamba la bibi angalau hubakiza mabaki kwa ajili ya wajukuu.
Takukuru na usalama wa taifa ni wa nini na wanafanya nini? Hapa lazima wachunguze hii syndicate nzima na wanufaika wakamatwe na kutaifishwa tena haraka sana kabla hawajavuruga ushahidi au wengine kukimbia nchi hasa ikizingatiwa wengi ni wageni.
            Lazima, kama taifa tutoe somo kwa nchi nyingine za kiafrika ambazo viongozi wake hupoteza muda na fedha nyingi kwende kujidhalilisha kuomba wakati makampuni ya kimataifa yanayotufanyia hivi yanatoka kwenye nchi. Hapa bila shaka lazima Magufuli afukue makaburi.
            Mbali na yaliyotajwa hapo juu, kuna haja ya kuangalia na sekta nyingine kama vile viwanda, mashamba, vitalu vya kuwindia na kila aina ya biashara inayohusiana na mali ya umma bila kusahau kuziba mianya iliyotamalaki mipakani ambapo mali nyingi za taifa hupitishwa wakati zikitoroshwa nje kwenda ng’ambo au nchi jirani ambazo nyingi zinajisifu kuwa wazalisha wa madini ambayo hazina hata chimbo moja.
            Mbali na wizi wa madini yetu, taarifa za kamati ni kwamba hata scanners zilizofungwa bandarini ni bomu. Je nani walinunua scanners hizi; kwa fedha kiasi gani, toka nchi gani na zilianza kufanya kazi lini? Hii itasaidia kutathmini ni kiasi gani Tanzania imeishaibiwa ili hata itakapochukua hatua dhidhi ya wahusika ijue ukubwa wa hasara inayoshughulika nao. Pia kuna haja ya kuyabana makampuni au watu walionufaika na wizi huu ndani na nje ili warejeshe fedha yetu tena ikiwa na interests juu. Je wamelitia taifa hasara kiasi gani? Nao wakamatwe na kushughulikiwa baada ya kutaifisha mali wanazomilki.
            Tumalize kwa kuipongeza serikali angalau kwa kuamka usingizini na viongozi wake kuonyesha uzalendo wa hali ya juu. Tunadhani huu ni mwanzo ambao utasambaa nchi nzima katika sekta zote zenye kutia shaka ili kubadili na kuliendeleza taifa kwa kutumia raslimali lilizojaliwa na Mungu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: