Tuesday, 9 May 2017

Mwakyembe Kukalia Ripoti ya Clouds Ni Kujidhalilisha

Image result for photos of makonda and mwakyembe
Kwanza, nikiri. Namheshimu sana Dk Harrison Mwakyembe waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hakuna ubishi kuwa–kwa hali ilivyo–kufichwa kwa taarifa ya kuvamiwa kwa kituo cha Clouds cha jijini Dar Es Salaam unaodaiwa kufanywa na mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda kunamtia doa waziri Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alijijengea umaarufu kabla ya kuubomoa. Tunasema alibomoa umaarufu wake pale , kama mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, akijibishana na Lowassa mwaka 2008 aliyelalamika kuonewa, kusema; wasingeficha baadhi ya mambo, huenda serikali nzima ingeng’oka.  Na kweli, baada ya kumtoa kafala Lowassa, Mwakyembe aliteuliwa waziri.  Hapo ndipo wenye akili walianza kuhoji usafi wake. Hadi leo, watanzania walio wengi hawajui ni mambo gani; na kwanini tume ya Mwakyembe iliyaficha. Juzi, akiwa bungeni, alirudia maneno yake kwa kuwataka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waache kulalamika juu ya Lowassa vinginevyo angeacha kazi ili kumshughulikia Lowassa asijue naye yako mengi kwenye kashfa hiyo hiyo yanayoweza kutumika kumshughulikia kama anavyoshughulikiwa kwa kutwisha zigo kama hili la Clouds akishindwa kulishughulikia. Na wanaomjua vilivyo Mwakyembe ni kwamba hatalishughulikia. Kama alivyokaririwa hivi karibuni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) akisema kuwa Mwakyembe anajipendekeza kwa Magufuli, naye asipinge. Ukitaka kujua mengi aliyosema Lissu, nenda https://www.youtube.com/watch?v=GqSGcItCJt8
Mwakyembe alipoteza udhu na umaarufu na hata ithibati baada ya kukubali kupewa cheo, kama si kulipwa fadhila na wale wale waliotuhumiwa kwenye kashfa aliyochunguza na kuumiza wengine huku akiwaokoa wahalifu wachache wenye madaraka. Hata hivyo, wengi wanajiuliza: Kama Mwakyembe aliweza kuusaliti umma kwa kufukuzia cheo, atashindwa nini kutumiwa kwenye kashfa hii ambayo hadi sasa haijulikani itaisha lini? Kwa kuendelea kutumika, kuna wakati anatenda dhambi za Lowassa na wenzake ambao serikali yao ilifichiwa mambo ili isianguke ziwe ndogo kuliko aliyotenda Mwakyembe.
Kimsingi, kufichwa kwa taarifa ya tume hii iliyoundwa na Nape Nnauye mtangulizi wa Mwakyembe, ambayo inaendelea kuota mbawa kiasi cha kuanza kumuonyesha waziri kama kikaragosi kinachotumiwa kulinda maovu na uoza wa mtuhumiwa ambaye ni mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonde si jambo la kunyamazia wala kuvumiliwa. Sijui kwanini waziri anashindwa kusoma alama za nyakati kuwa kama mwenzake ameondolewa kwa kukataa kutumiwa  anayetumiwa  ni rahisi sana kutumiwa na kutupwa kama ganda la muwa. Kwanini Mwakyembe hataki kukubali kuwa kushushwa cheo (demotion) kulitokana na yeye kutekeleza wadhifa wake kwa kuwataka watanzania wasioe bila vyeti vya kuzaliwa jambo amri ambayo bosi wake alitengua hata bila kumpa nafasi mwenyewe afanye hivyo.
Kwa wanaomjua Mwakyembe hawashangai anachofanya sasa. Nani mara hii kasahau alivyochunguza kashfa ya Richmond na kuishia kuficha baadhi ya mambo jambo ambalo alikiri mwenyewe akaishia kupewa uwaziri kama zawadi ya kufanya hivyo. Nadhani hata huyu anayemshusha madaraka na hadhi anajua historia yake na namna ambavyo hawezi kuacha kutumika.
Inashangaza mtu mwenye PhD, tena ya sheria, kutumika hivi. Je taarifa ya tume husika itawasilishwa na kufanyiwa kazi lini? Na kama haitawasilishwa na kufanyiwa kazi  ni kwanini na kwa amri na faida ya nani?
Kama haitolewi, waziri awaambie watanzania hatua mbadala na stahiki ambazo atachukua. Niliwahi kumsikia akisema kuwa Makonda hakutendewa haki kwa vile hakusikilizwa wakati tume ilisema wazi wazi–bila ya yeye kukanusha–kuwa tume ilikwenda kumhoji akatokea mlango wa nyuma. Hii ni hoja ya ajabu na isiyo na mashiko tena ikitolewa na mtu aliyefanya kosa lile kwenye sakata la Richmond ambapo mtuhumiwa mkuu waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa hakusikilizwa; na Mwakyembe huyu huyu hakuona kama hili ni tatizo wala sababu ya kuahirisha uchunguzi kama anavyofanya kwenye sakata la sasa. Hii inafanya aonekane mtu wa ajabu kidogo.
Kitu kingine kinachoshangaza ni ile hali ya Mwakyembe kujifanya kuwa ni mlezi na mtetezi wa vyombo vya habari wakati vikivamiwa anatetea wahalifu wa kawaida tu. Mfano ulio hai ni kitendo chake cha kuendelea kuatamia ripoti ya uvamizi wa Clouds.
Bila kusema sana, Mwakyembe akiendelea na msimamo wake wa kufutika taarifa ya uchunguzi wa kashfa husika ili ijifie, hataeleweka ukiachia mbali kuendelea kupoteza imani na heshima ukiacha mbali kujenga dhana kuwa amekubali kutumiwa kwenye uchafu huu ambao mtu yeyote mwenye akili hasa kiongozi anayefaa hawezi kuutenda au kuufumbia macho hata kwa sekunde achilia mbali muda mrefu uliokwishapita. Tumshauri Mwakyembe kufanya maamuzi magumu. Akubali kulitumikia taifa au kujirahisi kutumiwa jambo ambalo, licha ya kutofaa, si stahiki yake kwa elimu na umri wake. Kwani, kama atakubali kutumiwa na yeyote awaye awe mtu au taasisi kufanya kile waingereza huita to do someone’s dirty laundry , tena mtu mwenyewe kijana mdogo na mjinga wa umri wa mwanae tena wa mwisho. Hataheshimika; hata kama ataendelea kuwa madarakani. Heshima ni kitu kidogo lakini chenye thamani tena kuliko fedha na ulaji wa madaraka. Atayakumbuka haya baada ya kumkuta yaliyowakuta watangulizi wake kuanzia Lowassa hadi Nape.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.
 

No comments: