Wednesday, 3 May 2017

Kijiwe chastukia zoezi la kuhakiki vyeti vya kibashite


Baada ya mbwembwe nyingi zilizoonyeshwa na watawala kwenye kupokea ripoti ya uhakiki wa vyeti vya feki au vya kibashite, Kijiwe kimestuka na kutoa angalizo.
Msomi Mkatatamaa anaingia akiwa amekula ndita wazi wazi. Anaamkua kama ada na kuronga “jamani mmeona sanaa za juzi kule Idodomya?”
Kabla ya kuendelea Mchunguliaji anauliza “Msomi hujui kuwa hii kaya ni ya sanaa; unaongelea sanaa gani wakati Idodomya ni jiji la sanaa kuanzia njengoni hadi ikuuni?”
Msomi anajibu “namaanisha ripoti ya kuhakiki vyeti vya kibashite iliyowasilishwa juzi huku Bashite na mabashite wengine wanaojulikana wasiwemo. Who is fooling whom hither? Haiwezekani njuluku lukuki zikatumika kuwaandama vidagaa na vihiyo wadogo wakati mapapa yakiendelea kutesa na kulipwa kodi zetu. Where is Bashite here? Tell me; where is Bashite. Please;  I want to know.”
Kabla ya kuendelea mzee Maneno anamkumbusha Msomi. Anasema “Dk Msomi angalia kikameruni hicho. Kumbuka uko Bongo siyo kwa mama.”
“Looh! Nilipitiwa. Unajua; nikipandisha mwenembago huwa naongea kitasha kwanza kuonyesha nimepiga buku na sikughushi wala kutumia cheti cha mchovu yoyote. Pili huwa nataka kuonyesha utaalamu wangu japo sina ajira wakati vihiyo na vibashite vikifaidi njuluku zetu,” anajitetea Msomi.
Mpemba anaamua kula mic “yakhe hii mada uloleta humu mwake Wallahi. Hata mie nliposikia kuwa zoezi lenyewe kumbe halihusishi viongozi nilishangaa. Kwanini hawahusishwi wakati nao wautumikia umma au kazi yao ni kuutumia na kuula umma? Haiwezekani wasiwemo wakati walipwa nshahara utokanao na kodi zetu. Au wataka kuwa kama madereva wa ngarawa ambao huongoza chombo kwa kukaa nyuma? Uongozi wa kweli ni kuwa nstari wa mbele na si kukaa nyuma. Hawa wapaswa kuimbiwa wimbo wa Remi Ongola wa ‘Mbele kwa mbele’. Wallahi mie naona huu unafiki tena uniotisha? Kwanini wafanyakazi wa umma wawe weledi wakati viongozi wao vibashite?”
Mijjinga anakula mic “sasa najua ni kwanini kaya yetu ni ombaomba. Haiwezekani watendaji wa umma wakawa wamepiga buku huku wanaosimamia asasi za kutoa maamuzi wakaruhusiwa kikatiba kuwa vihiyo wasipingane hata kuhujumiana? Huu hakika ni ukoloni wa  kinyumbani ambapo wakubwa wanajihudumia kwa kupinda sheria.”
Kabla ya kuendelea Mipawa anampoka mic na kusema “wale waliokuwa wakihoji na kushangaa kwanini katiba mpya iliuawa na kuacha hivi viraka sasa wamepata majibu. Jamaa wanataka waendelee kutesa huku wakiwatesa wahalifu wenzao walioghushi kama wao.”
Mgoshi Machungi anaamua kunchomekea Mipawa “Mgoshi usemayo ya kwei. Huoni wakubwa wanavyoipwa mabiioni wakati wavuja jasho wakiipwa kichee?  Kimsingi, huu ni mfumo wa kikooni ambao wakooni weusi waiuishi toka kwa mwingeeza. They aa the same the diffeence is the kaa. Yaani hawana  tofauti bali rangi.” Kijiwe hakina mbavu jinsi Mgoshi anavyokibukanya kimanga kwa kisambachi.
Sofia Lion aka Kanungaembe anabusu mic “ mie wala sishangai. Kwani tangu skandali ya Bashiit ilipofumka, kama hawa wanaotudharau na kutuona majuha wasingeendelea kuwa naye kwenye utumishi wa umma. Wana bahati mzee Mchonga alisharejesha namba. Kwani angewatolea uvivu. Tunapaswa kuandamana ili akina Bashite nao wahakikiwe. Wale waliokwishabainika kama Bashite mwenyewe wala hawahitaji kuhakikiwa bali kupelekwa kwa pilato ili wakapewa zawadi yao. Tumechoka na kugeuzwa mabunga na hamnazo na vihiyo na vibashite.”
Kabla ya kuendelea Kanji anamchomekea “mimi iko sangaa sana kwanini dokta ya jipu naogopa tumbua bashite. Kwanini hapana ona jinsi nachafua yeye kiasi cha vatu vote piga kelele u maskioni yake iko bovu? Yeye napaswa chukua hatua hapana wuta miguu au chelevesha bashitehe.”
Mheshimiwa Bwege aliyekuja na mtemba leo anaamua kutia guu “wote mmeongea; lakini mmesahau kitu kimoja muhimu. Japo sipendi kutumia sana kitasha, leo acha nivunje mwiko. Watasha husema ‘show me your friends; I’ll tell you who you are yaani nionyesha maswahiba zako nikwambie wewe ni nani. Hivyo, ukiona Kanywaji anamg’ang’ania Bashitehe ujue kuna namna. Maana haiwezekani msomi kama yeye akajifanya hasikii vilio vya wanakaya waliochoshwa na Bashiteism. Nadhani kuna haja ya kuwaambia wahusika kuacha ubwege. Kila kitu kiko wazi kuwa Bashite ni bomu tena la nyuklia. Kwanini kungoja lijitumbue na kuumiza wengi badala ya kulitumbulia mbali au nalo ni kaburi analoogopa jamaa kufukua asishindwe kufukia? What is going on behind the curtains? Mnatukwaza kiasi cha kushuku na kuwaza mengi. You know what I mean. Maana binadamu ni kiumbe dhaifu kweli kweli na lolote laweza kutokea hata wengi wasilotegemea kuhusiana na mazoea na tabia za wahusika. Lazima tujue hiki alichotoa Bashite hadi akakingiwa kifua kana kwamba ni bi Nkubwa wa dingi.”
Kijiwe kikiwa kinachangamka si likapita shumbwengu la Bashite likitokea Kariakoo! Acha tulitoe mkuku huku tukisema kwa sauti ya juu “vyeti, vyeti, vyeti, Bashite onyesha vyeti yaishe.”
Tukiwa tunamkaribia kumfanyia kitu mbaya ikiwamo kumkaba hadi aonyeshe vyeti si ndata wakaamua kuingilia kiasi cha kudhani tutatiana mtu kati! Tuliwaonea huruma. Hivyo, kuamua kuachana na jamaa ili tusiwaumize ndata bure ikawa soo.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: